Tuesday 29 December 2015

UBOMOAJI WA MAENEO YA WAZI UNG'ATE PANDE ZOTE


HIVI karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametaja maeneo ya wazi 180 yaliyopo jijini Dar es Salaam ambayo yamevamiwa. Manispaa ya Kinondoni ndiyo inayoongoza kwani imebainika maeneo yake ya wazi 111 yamevamiwa, ikifuatiwa na Ilala ambayo maeneo yake ya wazi 50 yamevamiwa.


Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ndiyo yenye unafuu kidogo ambayo maeneo yake 19 yamevamiwa. Tunafahamu maeneo hayo ya wazi yamevamiwa na kujengwa nyumba za makazi, biashara, gereji, maeneo ya starehe na cha ajabu baadhi yao wamiliki wake wana ofa na hati ikimaanisha wanamiliki kihalali ingawa kwenye ramani ya mipango miji inaonesha ni maeneo ya wazi.
Wengi wa ‘wamiliki’ wa maeneo hayo ya wazi ni wenye fedha ambapo kwa kutumia fedha zao wameweza kuwarubuni maofisa ardhi wasio waaminifu na wakawasaidia kupata hati na vibali vya ujenzi. Wapo wengine waliowatumia wanasiasa hasa madiwani na kwa ushawishi wao wakawasaidia kupata maeneo hayo ya wazi na kujenga au kuweka vitega uchumi vyao.
Kutokana na uvamizi huo sasa tunaona watoto wetu wakikosa maeneo ya kuchezea lakini pia wananchi kukosa hata maeneo ya kupumzika. Kutokana na takwimu hizo alizotoa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, tunaamini kuanzia Januari mwakani tutashuhudia maeneo hayo yakirejea katika matumizi yake yaliyokusudiwa yaani kubaki kuwa ya wazi.
Tunamuomba Waziri na watendaji wengine kwenye hili la bomoabomoa kwenye maeneo ya wazi haki itendeke. Nyumba au biashara zilizowekwa kwenye maeneo hayo hata kama yana thamani ya gharama kubwa kifedha yabomolewe na kusiwe na kuoneana aibu wala kufikiria mara mbilimbili.
Ikiwa wale wa mabondeni hasa bonde la Mto Msimbazi kwenye maeneo ya Kinondoni Mkwajuni na kwingineko, bomoabomoa ilifanyika bila simile basi na wanapoishi matajiri na wenye fedha nako wabomolewe bila huruma.
Sisi tunaona kubomolewa pekee haitoshi bali na watendaji wa Halmashauri waliohusika kwa namna moja au nyingine kubadilisha matumizi ya maeneo hayo wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani na si kuwahamisha vituo vya kazi.
Kuwaacha watendaji kutawafanya waendelee na ujanjaujanja huo na mwingine kwani watajiona mkono wa sheria hauwezi kuwagusa. Wakati ubomoaji huo unafanyika, serikali ichukue jukumu la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuogopa kumilikishwa maeneo ya wazi na yaliyo kwenye vyanzo vya maji.
Tunaamini maeneo hayo ni muhimu kwa wananchi hivyo bila kupoteza muda sasa yaboreshwe na watoto wapate sehemu za kuchezea kama ilivyokuwa miaka ya nyuma lakini pia wananchi wapate maeneo ya kupumzika na hata kufanyia shughuli za mtaa.
Tuige nchi za wenzetu kama hapo Kenya, maeneo mengi ya wazi yanatunzwa na halmashauri husika ambapo kunatengenezwa bustani na watu wanakaa kwenye viti wakipumzika lakini pia inasaidia kuboresha mandhari ya mji.
Sisi tunaamini hakuna linaloshindikana hivyo ni wakati sasa kwa viburi vya watendaji na wenye pesa vifike mwisho wake, kila mtu aheshimu mipango miji na ardhi itumike kwa kusudio lililopangwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!