Kauli ya Tibaigana inakuja takribani miezi 15 tangu aliposema anatamani kuiona Tanzania ikimpata rais dikteta kwa kuwa nchi haiwezi kupiga hatua iwapo mkuu wa nchi hataweza kukemea na kutoa amri watu wakatii.
Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili nyumbani kwake katika Kijiji cha Katare, wilayani Muleba Mkoa wa Kagera, hivi karibuni, Tibaigana alisema anaamini changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania zitatatuliwa na Rais Magufuli.
Akitolea mfano utaratibu wa Rais Magufuli wa kufanya ziara za ghafla kwenye sekta mbalimbali za umma, Tibaigana alisema: “Watu hawafanyi kazi na viongozi ni waoga wa kutoa uamuzi, ziara ya Rais Magufuli (Hospitali ya) Muhimbili imesababisha hospitali nyingi kuboresha huduma, siyo lazima afike kila mahali akitoa kauli hatua ichukuliwe.”
Kamanda huyo mstaafu alisema hata uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta safari za nje kwa viongozi wa umma mpaka kwa kibali maalumu, umekuja wakati mwafaka kwa kuwa baadhi ya safari hazikuwa na masilahi kwa taifa.
“Safari zinatumia pesa nyingi na nyingine huwa siyo za lazima, kwa uzoefu wangu wa kukaa Serikalini hata baadhi ya wafanyakazi wa ndani hulipwa kama waajiriwa kwa kufanyiwa mipango na mabosi wao,’’ alisema.
Tibaigana ambaye aliwahi kugombea ubunge Jimbo la Muleba Kusini miaka mitano iliyopita kupitia CCM na kushindwa kwenye kura ya maoni, alipendekeza Bunge la 11 kufanyia marekebisho baadhi ya sheria ili ziwe kali kwa watu wanaohujumu uchumi.
Maagizo yatekelezwa
Kauli ya Tibaigana imekuja wakati Rais Magufuli ameanza kazi ya kutafuta na kuziba mianya ya upotevu wa fedha, alianzia Hazina na kupiga marufuku safari zote za nje kwa viongozi na kusema zitakuwa zinaruhusiwa kwa kibali maalumu.
Dk Magufuli pia aliamuru mashine za MRI na CT-Scan katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zitengenezwe na kuagiza Sh3bilioni zitolewa kugharimia matengenezo kati ya Sh7bilioni zilizokuwa zinahitajika.
Vilevile, aliagiza Sh4bilioni zilizokuwa zitumike katika Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru Desemba 9, kutumika kupanua barabara ya Morocco kwenda Mwenge, kazi ambayo utekelezaji wake unaendelea.
Rais huyo wa Awamu ya Tano na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti walitembelea maeneo muhimu kwa uchumi wa nchi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bandari na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kuibua vitendo vya ufisadi na ukwepaji wa kodi.
Akizungumzia hali hiyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema kinachoonekana ni uzembe au udhaifu kwa watumishi wa umma ambao mbali na kuwa wazito katika kutoa uamuzi, lakini ni wazito katika kutambua uzito wa tatizo.
Alisema lipo tatizo kubwa kwa viongozi wengi kukosa uwajibikaji licha ya dhamana kubwa walizopewa na kusema wakati umefika wa kuangalia upya mfumo wa uteuzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali nchini.
“Hii ni dalili ya kuwa na viongozi wasiowajibika…maana haiwezekani mashine muhimu inaharibika na mkurugenzi na madaktari wake wanakaa kimya tu kama vile hakuna kilichotokea… hii inaonyesha kuwa tabia ya uwajibikaji haipo serikalini,” alisema Dk Bana.
Alisema kama ambavyo wafanyakazi wa Serikali wanaweza kudai mishahara kwa kugoma, kunapotokea kukosekana kwa vitendea kazi, watumie nguvu ileile kudai ili waweze kufanya kazi.
Alisema haiingii akilini kuona baadhi ya watendaji wa Serikali wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya na hata makatibu wakuu kukaa kimya licha ya Rais kuonyesha njia kipindi kifupi tangu ashike nafasi hiyo.
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema uchapaji kazi wa viongozi katika eneo lolote unategemea na umakini na ufuatiliaji wa kiongozi mkuu.
“Baba katika familia akiamua mambo yaende yataenda tu… ni kawaida katika mabadiliko, binadamu kujaribu wakiona huna mchezo watafanya kazi wakiona ni nguvu ya soda mtarudi kule kule” alisema Profesa Shumbusho.
Alisema watendaji walio wengi walionekana kulala na kufanya kazi kwa mazoea kutokana na wakuu wao na akasema sasa wameanza kuamka kutokana na kasi ya mtendaji mpya na akasema kasi ya utendaji inaweza ikawa kubwa zaidi endapo rais naye ataendelea kuonyesha njia.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment