Thursday 24 December 2015

TANESCO YAAGIZWA KUKAMILISHA MIUNDO MBINU YA KUSAMBAZA UMEME JIJINI DAR ILI KUPUNGUZA TATIZO LA UMEME


Serikali imeliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kukamilisha mradi wa kukuza miundo mbinu ya kusafirisha umeme 
unaosimamiwa na Kampuni ya kutengeneza vipozeo(Transformer) ya Italy (SAE) ili kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Agizo hilo limetolewa leo jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kaleman katika ziara yake ya kutembelea mradi huo katika vituo vya Mbagala, Kurasini , Gongo la Mboto na kipawa.

Amesema kuwa ni vema hadi kufikia Februari mwakani Tanesco wawe wamekamilisha mradi huo na wananchi waweze kupatiwa huduma ya umeme haraka iwezekanavyo.

Aidha Dkt. Kalemani aliagiza kuwa kutokana na kesi ya fidia  ya wananchi wote ambao wameondolewa kwenye maeneo yao ili kupisha mradi huo  ni vema wawe wamelipwa kufika Januari 2016.

Akitoa maelezo kwa Naibu Waziri huyo ,Meneja Mradi wa Tanesco Mhandisi Frank Mashalo amesema kuwa kulingana na mkataba walioingia na Kampuni ya SAE mradi huo ulipaswa kukamilika kwa kipindi cha miezi 18 lakini bado haujakamilika kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo sakata la fidia na kuchelewa kwa vipozeo vya umeme  kufika kwenye vituo hivyo.

Ameongeza kuwa jumla ya dola milioni 34.252 zinatarajiwa kutumika ili kukamilisha mradi huo ambapo kati ya hizo tayari Dola milioni 28 zimeshalipwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!