Saturday, 12 December 2015

SURA 17 MPYA NDANI YA BARAZA LA JPM

Rais John Magufuli akifurahia jambo na Katibu

Miongoni mwa mawaziri na manaibu waziri walioteuliwa kwenye baraza jipya la Rais John Magufuli, zimo sura mpya 17 ambazo zimeteuliwa kwa mara ya kwanza.


Sura mpya hizo za mawaziri katika baraza hilo ambalo uteuzi wake umechukua muda mrefu ni Nape Nnauye ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo.
Nape ambaye alishinda ubunge katika jimbo la Mtama katika Uchaguzi Mkuu kwa mwaka huu ameteuliwa kuwa waziri kwa mara ya kwanza katika Serikali ya awamu ya tano.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM, ataitumukia wizara hiyo pamoja na naibu wake Anastazia Wambura ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu wanawake wa chama hicho.
Naibu Waziri aliyeteuliwa kusimamia Wizara ya Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala bora ni Jafo Seleiman Said ambaye pia ni mbunge wa Kisarawe.
Katika Wizara ya Ofisi ya Makamo wa Rais inayoshughulikia Muungano na Mazingira, Rais Magufuli amemteua Luhaga Mpina kuwa naibu waziri wa wizara hiyo.
Mpina amekuwa mbunge wa Jimbo la Kisesa tangu mwaka 2005.
Chini ya Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Rais Magufuli ameteua manaibu waziri wawili kusimamia wizara hiyo.
Manaibu hao ni Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Possy Abdallah ambaye pia ameteuliwa kuwa mbunge, mwingine ni Anthony Mavunde, mbunge wa Dodoma Mjini.
Hata hivyo, Mei mwaka huu Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimteua Mavunde kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa.
Katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi naibu waziri atakayesimamia ni mbunge wa Ngorongoro William Ole Nasha huku Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani.
Rais Magufuli amemteua Dk Ashantu Kizachi kuwa naibu waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango na Dk Medard Karemaligo kuwa naibu waziri wa Nishati na Madini.
Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, aliyeingia kwenye ulingo huo kwa mara ya kwanza ni Dk Augustine Mahiga.
Dk Mahiga alikuwa miongoni mwa makada wa CCM aliyetangaza kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akimtangaza jana Rais Magufuli alimteua pia kuwa mbunge, huku akimtaja Dk Suzan Alphonce ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu kuwa naibu wa wizara hiyo mpya.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naibu waziri aliyeteuliwa kusimamia ni Angelina Mabula ambaye ni mbunge wa Ilemela, Mwanza.
Katika Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo haijapata waziri, Rais Magufuli amemteua Mhandisi Ramon Makani kuwa naibu waziri wa.
Sura nyingine mpya ni ya Mhandisi Stella Manyanya ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Dk Khamisi Kigwangalla ambaye alikuwa mmoja wa makada wa CCM waliotangaza nia ya kuwania nafasi ya urais, ametuliwa kuwa naibu waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto huku Mhandisi Isack Kamwela (mbunge wa Katavi) akiteuliwa kuwa naibu waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!