Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya jumla ya Sh. bilioni 11.1 hadi kufikia jana ikiwa ni kodi ambazo wafanyabiashara wamelipa baada ya kubainika kukwepa kulipa ushuru wa makontena 329 yaliyoondoshwa bandarini bila kulipiwa.
Fedha hizo zimeongezeka kwa muda wa siku mbili, kwani hadi Jumamosi iliyopita, TRA ilikuwa imekusanya Sh. bilioni 10.6 tu.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu kiasi kilichokusanywa hadi kufikia jana.
Mwishoni mwa wiki TRA iliwataka wafanyabiashara hao kulipa fedha hizo kabla ya kuwachukulia hatua kali za kisheria kufuatia agizo la siku saba la Rais John Magufuli kumalizika Desemba 11, mwaka huu.
TRA ilisema itaanza msako mkali kwa wafanyabiashara ambao wamekiuka agizo hilo kufuatia siku saba za kujisalimisha kulipa kodi hiyo bila ya kuchukuliwa hatua za kisheria kumalizika.
Wafanyabiashara ambao walikuwa hawajalipa kodi hadi Jumamosi walikuwa ni 15 na kiasi walichokuwa wanadaiwa ni Sh. bilioni 3.75, huku wale waliokuwa wamelipa deni lote wakiwa 13 ambao walilipa kiasi cha Sh. bilioni 4.16.
Aidha, wafanyabiashara 15 walilipa Sh. bilioni 2.3 ikiwa ni sehemu ya deni walilokuwa wanadaiwa la Sh. bilioni 16.44.
No comments:
Post a Comment