Wednesday, 16 December 2015

POLISI WATAHADHARISHA USALAMA KIPINDI CHA MWAKA MPYA

 

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuimarisha ulinzi, amani na usalama katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.
  
Aidha, limewataka wafanyabiashara na wamiliki wa hoteli nchini kuweka kamera zenye uwezo wa kufuatilia mienendo ya wateja wao wanaoingia na kutoka katika maeneo hayo, ili kuwabaini wahalifu na uhalifu kwa haraka.
Rai hiyo ilitolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa jeshi hilo, Advera Bulimba, wakati akitoa tahadhari ya usalama jana ofisini kwake  makao makuu ya jeshi hilo, jijini Dar es Salaam.
Alisema uzoefu unaonyesha kipindi cha kuelekea mwisho wa mwaka baadhi ya watu hutumia fursa hiyo kujipatia kipato kwa njia isiyo halali kwa kufanya udanganyifu, wizi utapeli, ujambazi na uhalifu mwingine katika maeneo mbalimbali na kuwataka  wananchi kuwa makini katika shughuli zao za kila siku ili kujiepusha na watu hao.
Hata hivyo, Bulimba alisema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kwa kufanya doria katika maeneo yote ili kuhakikisha wananchi wanasheherekea na kumaliza mwaka kwa amani na usalama.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu kupitia namba za bure za simu ambazo ni  111 na 112.ambazo ni za dharura 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!