Thursday, 31 December 2015

MWAKA 2015 ULISHUHUDIA SHILINGI IKITUMBUKIA "SHIMONI"



Tofauti na miaka minne iliyopita, wakati mwaka 2015 unaanza ilikuwa ikifahamika bayana kuwa ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu.


Kupitia tukio hilo la kidemokrasia, sehemu kubwa ya Watanzania walikuwa na shauku ya kuchagua viongozi ambao wangewaondolea dhiki inayowakabili, kwa kuchangia kukuza uchumi kwa sera na mikakati mipya.

Hata hivyo, wakati wakisubiria mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli aliyechaguliwa Oktoba 25, baadhi ya masuala ya biashara na uchumi hayakutaka kusubiri mchakato huo, yaliendelea kutokea.
Kuanzia Januari, matukio mbalimbali yametokea ambayo ama yalishusha au kuchangia kukua kwa uchumi na hatimaye kusababisha mafanikio au madhara yenye uzito unaofanana katika maisha ya kawaida ya wananchi.
Mwandishi wetu anapitia baadhi ya matukio makubwa ya kukumbukwa mwaka 2015 likiwamo tukio la kihistoria la kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani hadi kufikia Sh2,400 mwishoni mwa Juni.
Kushuka kwa thamani ya Shilingi
Kwa mara kwanza katika historia tangu Tanzania ipate uhuru, thamani ya shilingi ilishuka hadi kufikia kati ya Sh2,300 na Sh2,400 dhidi ya Dola ya Marekani katika baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha jijini Dar es Salaam.
Mwenendo wa kushuka kwa thamani ya shilingi ulianza kuonekana mapema Januari wakati baadhi ya maduka yalipokuwa yakiuza Dola ya Marekani kati ya Sh1,750 na Sh1,800 lakini hali ilizidi kuzorota zaidi mwanzoni mwa Mei wakati Dola ilikuwa ikiuzwa kwa zaidi ya Sh2,000.
Tishio hilo la kushuka kwa thamani ya Shilingi kuliwafanya baadhi ya wabunge kupaza sauti wakati mkutano wa Bajeti, wakiitaka Serikali kuingilia kati hali hiyo ili kuwanusuru Watanzania na kupanda kwa gharama za maisha.
Hata hivyo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema hakukuwa na namna ambayo Serikali ingefanya, kwa kuwa sarafu karibu zote barani Afrika zilikuwa zikishuka thamani kwa kuwa Dola ya Marekani ilikuwa ikipanda thamani.
Shilingi baadaye ilianza kuimarika taratibu hadi sasa kufikia Sh2,150 hadi Sh2,170 kwa Dola ya Marekani katika baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha hali iliyopunguza kidogo maumivu kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa ndani na hatimaye kupunguza kidogo gharama za maisha.
Kuongeza mapato na kudhibiti wakwepa kodi
Kuingia kwa Serikali ya Dk Magufuli kumefanya mwaka huu uishe kwa neema katika upande wa ukusanyaji wa mapato. Baada ya kuapishwa Novemba 5, Rais alianza kutekeleza mikakati yake ya kubana matumizi serikalini, huku akiziba mianya yote ya upotevu wa mapato ikiwamo ya kudhibiti wakwepaji wa kodi.
Mikakati hiyo ilihusisha kufuta safari za nje ya nchi kwa watumishi wa umma isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka Ikulu, kupunguza gharama za sherehe na vikao na kusafisha ukwepaji kodi bandarini.
Kwa pamoja, jitihada hizo zimesaidia Serikali kuokoa mabilioni ya shilingi na kuifanya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvunja historia ya ukusanyaji mapato hadi kufikia Sh1.3 trilioni kwa mwezi Novemba.
Ukuaji wa Uchumi
Kasi ya ukuaji uchumi iliendelea kuwa ndani ya wastani wa asilimia saba kwa mujibu wa ripoti za robo mbili za kwanza zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Hata hivyo, ukuaji upo chini ukilinganisha na robo mbili za awali kwa mwaka uliopita.
Robo ya kwanza ya Januari hadi Machi, ilishuhudia uchumi ukikua kwa kiwango cha asilimia 6.5 ikiwa ni asilimia 2.1 chini ya kipindi kama hicho mwaka jana wakati robo ya pili ilishuhudia ukuaji wa asilimia 7.9 kutoka asilimia 10.1 mwaka 2014.
Ripoti ya Benki ya Dunia ijulikanayo ‘Africa’s Pulse’ iliyotolewa Oktoba ilibainisha kuwa Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo uchumi wake ungeendelea kuimarika mwaka huu na hata kuzidi wastani wa sasa wa ukuaji wa pato halisi la taifa wa asilimia saba.
Kasi ya ukuaji huo ungeendelea hadi mwaka 2017 kutokana uwekezaji mkubwa katika sekta za nishati, matumizi ya kawaida ya wananchi na katika rasilimali za asilia.
Mtikisiko wa misaada
Kama ilivyokuwa mwaka jana, Serikali imetikiswa na wahisani wa maendeleo mwaka huu baada ya Shirika la Changamoto ya Milenia (MCC) la Marekani kuahirisha kutoa msaada wa Dola 472 milioni za Marekani (Sh1 trilioni) kwa ajili ya ukuzaji wa sekta ya nishati nchini. Bodi ya wakurugenzi wa MCC ilifikia uamuzi huo wiki iliyopita baada ya Serikali kushindwa kutatua mgogoro wa Uchaguzi Mkuu unaoendelea Zanzibar na kutangaza kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 haitatumika nchini kukandamiza uhuru wa msingi wa kukutana na kujieleza.
Mgogoro wa Zanzibar uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo Oktoba 28 kutokana na kuvunjwa kwa sheria na taratibu za uchaguzi.
Kama haitoshi, mwaka huu ulianza vibaya kwa athari za wahisani wa maendeleo kutoka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kuendelea kushikilia kwa muda takriban Sh1
Sakata la ufisadi la hatifungani
Sakata la ufisadi wa kufanikisha mkopo wa Sh1.3 trilioni kupitia hatifungani kutoka Benki ya Standard ya Uingereza kwa Serikali lililoibuliwa mwishoni mwa Novemba na Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya ufisadi ya Uingereza (SFO), limefanya mwaka umalizike vibaya.Katika sakata hilo watumishi wasio wamiinifu wa Stanbic, benki tanzu ya Benki ya Standard, waliingiza hasara Serikali kwa kutaka kuchota kifisadi asilimia moja ya Dola 600 milioni za Marekani sawa na Dola 6 milioni za Marekani kama sehemu ya ada ya kufanikisha mkopo huo mwaka 2013.
Mahakama ya Southwark Crown ya Uingereza iliyokuwa ikisikiliza shauri hilo iliitaka Benki ya Standard kuilipa fidia Tanzania Sh13 bilioni ambazo asasi ya kiraia ya kimataifa ya Corruption Watch imeona ni kidogo ikieleza ilistahili iwe Sh170 bilioni kufidia athari za kibiashara na uchumi zilizotokana na sakata hilo nchini.
Bajeti yazitema sigara, pombe
Kwa mara ya kwanza mwaka huu, Watanzania walishuhudia Serikali ikiachana na utegemezi wa bajeti ya pombe na sigara, badala yake ilipandisha kodi kwenye mafuta na kuminya uingizaji wa bidhaa nchini ambazo upo uwezo wa kutengenezwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
Bajeti hiyo iliyokuwa ya lala salama kwa utawala wa awamu ya nne, pia ilivunja historia ya utegemezi kutoka kwa wahisani kwa kupunguza kutoka asilimia 14.8 mwaka uliopita hadi asilimia 8.4 katika mwaka wa fedha unaoendelea.
Mwaka 2015 ndiyo unakatika, je, mwaka 2016 utakuwaje? Dk Magufuli atadhibiti mfumuko wa bei uendelee kuwa ndani ya tarakimu moja?

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!