Monday, 14 December 2015

MUHONGO: TATIZO LA UMEME NI UCHAKAVU WA MITAMBO

 ”Si kwamba majibu ya matatizo ya umeme hatuna,
 ”Si kwamba majibu ya matatizo ya umeme hatuna,
Tanga. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema tatizo la uzalishaji umeme kwenye mabwawa ni uchakavu wa mitambo baada ya kufanya ziara na naibu wake, Dk Menard Kalemani kwenye vituo vya New Pangani na Hale mkoani Tanga.


Profesa Muhongo, ambaye amerejeshwa kwenye wizara hiyo baada ya kulazimika kujiuzulu mapema mwaka jana kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, alitoa kauli hiyo baada ya kukutana na wakuu wa Shirika la Umeme (Tanesco) na baadaye kutembelea vituo hivyo vinavyozalisha umeme wa maji.

“Tumejigawa,” alisema Profesa Muhongo akizungumzia mpango kazi wake na Dk Kalemani jana.
“Naibu wangu yeye kesho (leo) atatembelea mtambo wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam. Mimi natembelea vituo sanjari na kuangalia hali ya mabwawa.”
Alisema ameamua kufanya ziara hiyo ya wiki moja katika vituo vyote vinavyozalisha umeme na kujua hali ya umeme nchini.
Alisema hataki kuingiza siasa katika masuala ya umeme na kwamba akisema mtambo fulani utazalisha megawati kadhaa, kuwe na kweli na si kuwadanganya Watanzania.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Rais John Magufuli aliituhumu Tanesco kuwa inamuhujumu kwa kukata umeme, na kutaka viongozi wajiandae kuondoka.
Na katika hotuba yake ya kuzindua Bunge mwezi uliopita, Dk Magufuli alisema kuna njama za kuruhusu maji kutoka Bwawa la Mtera ili wasingizie mitambo haiwezi kuzalisha umeme kwa kuwa hakuna maji, na hivyo kutengeneza soko wafanyabiashara kuuza jenereta.
Lakini jana, Profesa Muhongo alisema matatizo ya umeme yanasababishwa na mambo mawili.
Alisema sababu ya kwanza ni uchakavu mitambo na ya pili ni wananchi kuchepusha mkondo wa maji unaoelekea kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme.
“Tumekuwa tukishikana mashati, tukigombana na kutuhumiana huko nje, lakini ukweli ni huu; baadhi ya mitambo imechakaa na inahitaji kufanyiwa ukarabati,” alisema Profesa Muhongo akitofautiana na tuhuma za Rais Magufuli.
Alisema ni wakati mwafaka kwa Taifa kuacha kutegemea vyanzo vya umeme wa maji, badala yake lijaribu kutumia vyanzo vingine kama umeme wa makaa ya mawe.
Alisema mwezi ujao watafufua mashine ya pili ya kituo cha Hale, baada ya kupata mkopo kutoka Serikali ya Sweden, hatua ambayo itawezesha kituo hicho kuzalisha umeme kwa ufanisi.
Mramba alisema mashine hiyo ya pili ikianza kufanya kazi, itazalisha jumla ya megawati 21 zitakazoingizwa gridi ya taifa.
Kuhusu kuchepusha maji ya mabwawa ya uzalishaji umeme, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Esterina Kilasi alimuahidi Profesa Muhongo kulishughulikia jambo hilo ili kuhakikisha maji hayo yanatumika kama yalivyokusudiwa.
“Maji ni muhimu kwa wakulima, Lakini hata umeme pia ni lazima tuangalie namna ya matumizi sahihi ya maji haya,” alisema Kilasi.
Katika ziara hiyo, pia alikuwapo mkurugenzi mtendaji wa Tanesco, Felichesmi Mramba.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!