Thursday 3 December 2015

MSAADA WA DHARURA: MWANAMAMA ANAYEPIGA DANADANA UWANJA WA TAIFA AMWAGIWA MAJI YA MOTO AHITAJI MSAADA HARAKA!


MSAADA WA DHARURA;
 
Kama wewe ni mdau wa mpira wa miguu Tanzania bila shaka unamfahamu Hazala Charles Mnjeja. Yawezekana usimtambue kwa jina lake lakini ukamtambua kwa sura na shughuli ambayo amekuwa akiifanya uwanjani kabla ya mechi na wakati wa mapumziko.


Dada huyu ni maarufu sana kwa kupiga danadana uwanjani wakati wa mechi za soka. Shughuli hii imemwezesha kualikwa katika matamasha kadhaa, na hata amepata kusafiri kwenda nje ya nchi kutumbuiza watazamaji wa soka hasa wakati wa mapumziko.
Pamoja na umaarufu wake na kutumika sana katika mabonanza ya michezo na burudani, bado Hazala amekuwa akiishi maisha ya kutegemea ndugu. Kama angekuwa anaishi katika nchi ambazo wananchi wake wanathamini vipaji vya wananchi wenzao, Hazala asingekuwa katika hali ya maisha iliyomsababisha apatwe na mitihani ambayo imemwaribu mwili wake.

Hazala Charles ni mkazi wa Tandale Kwa Mtogole jijini Dar es salaam. Amekuwa akiishi katika nyumba ya mama yake mdogo eneo hilo. Hazala ni mama wa watoto kadhaa na watoto hao kwa sasa wanaishi na mama yake Hazala huko Chalinze mkoani Pwani.
Kutokana na kazi yake ya kupiga danadana iliyompelekea kusafiri hadi nje ya nchi, ndugu anaoishi nao waliweka matarajio makubwa sana juu yake kuliko uhalisia. Ukweli ni kwamba, kipato chake hakilingani na umaarufu wake. Kuwa na kipato kidogo ndiko kulikowafanya ndugu anaoishi nao kuanza kumwandama na hata kumtaka ahame kwani hawakuamini kuwa shughuli yake haimpatii fedha nyingi. 

Kwa kuwa hakuwa na pakwenda, Hazala aliendelea kubaki nyumbani hapo. Siku ya Jumamosi tarehe 28 Novemba 2015, ndugu hawa waliamua kumshambulia kwa kipigo na kummwagia maji ya moto ambapo aliungua vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.

Hazala amelazwa katika wodi namba tatu, wanawake, katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es salaam.
Kutokana na hali hiyo, Hazala anasema, “Kwa kweli ninatamani nihame nitakaporuhusiwa kutoka hospitalini. Yaliyonipata ni makubwa na pengine wanaweza kunifanyia makubwa zaidi ya haya. Ninawaomba wadau wanisaidie ili nipate sehemu ya kuishi.”
Akizungumzia kuhusu msaada aliokwishapewa hadi sasa, Hazala anasema, “kwa kweli msaada mkubwa niliopata mpaka sasa ni wahusika kukamatwa"

Pia Hazala anawashukuru wote waliomkimbiza hospitali kuokoa maisha yake. Anasema "walionisaidia kunileta hospitalini, nao ni msaada ambao kwa dhati nawashukuru wote walionisaidia. Lakini nikisaidiwa kuanza maisha mapya nitashukuru zaidi, kwani kwa hali hii sidhani kama nitaweza tena kucheza danadana. Nina watoto wanaonitegemea pamoja na mama kule Chalinze, sijui itakuwaje baada ya hapa.”

Kama umeguswa na ungependa kumsaidia Hazala fika Mwananyamala Hospitali wodi namba 3, wanawake utampata na kuwasilisha msaada wako, wakati huohuo tunaendelea kutafuta namba yake ya simu.

KWA HISANI YA BLOG YA WANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!