Damu zikiwa zimetapaa eneo la tukio.
WATU wanaokisiwa kuwa ni majambazi wamewavamia watu wanne waliokuwa ndani ya gari moja ndogo na kuwaibia fedha kisha kutimka nazo kusipojulikana.
Tukio hilo la kikatili lilitokea mchana wa leo majira ya saa sita maeneo ya Mwenge karibu na Baa ya Hongera ambapo taarifa zinasema kwamba watu hao walikuwa wakitoka benki kuchukua fedha zilizoibwa ambazo ni zaidi ya shilingi milioni nne.
Akizungumzia tukio hilo la aina yake lililochukua dakika mbili tu, shuhuda aliyekuwa mahali hapo alisema kwamba wakati gari hilo lilikuwa likitoka maeneo ya Sayansi kupitia njia ya mkato kwa ajili ya kuingia Barabara ya Shekilango, ndipo wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki wakaziba njia na mmoja kuteremka na bunduki.
Mashuhuda wakiwa katika eneo la tukio.
“Inaonekana kwamba jamaa walijua kilichokuwa kikiendelea na inawezekana waliwafuatilia kwa kipindi kirefu. Walipofika maeneo haya, tuliona wakifunga njia kisha mwanaume mmoja kuteremka na bunduki na kumtaka dereva afungue kioo na kuwakabidhi fedha, vinginevyo wangewaua,” alisema shuhuda huyo.
Hata alipoonyeshewa bunduki, dereva wa gari hiyo ndogo hakutaka kushusha kioo cha dirisha na hivyo kumlazimu jambazi huyo kuvunja kioo kile kwa risasi ambayo ilimpata dereva kwenye mkono wake wa kushoto.
“Kioo kilipovunjwa, hapo wakaufungua mlango, dereva akateremka huku akipiga kelele za maumivu, yule jambazi akachukua mfuko wa hela, alitaka kummalizia dereva yule ila kwa bahati akawa amejificha kwenye gari jingine hivyo jambazi kupanda kwenye pikipiki na kuondoka huku akiwa na mfuko wa hela,” aliongezea shuhuda wa tukio hilo.
Mara baada ya kutokea kwa tukio hilo lililokusanya watu wengi, wasamaria wema wakaamua kumsaidia jamaa aliyejeruhiwa kwa kumkimbiza katika Hospitali ya Marie Stopes ambayo haipo mbali kutoka eneo la tukio.
Na Nyemo Chilongani / GPL
No comments:
Post a Comment