Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA) imetaifisha madini aina ya Tanzanite yenye thamani ya Sh2.5 bilioni yaliyokamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati yakisafirishwa kwenda nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema madini hayo yenye uzito wa gramu 2,871 yalikamatwa Desemba 15, wakati Jain Anarungi, raia wa India alipojaribu kuyatorosha kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria.
“Madini yana thamani ya Sh 2.5 bilioni na tumeyataifisha kwa mujibu wa kifungu namba 6(4) cha sheria ya madini ya mwaka 2010, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 ” alisema Dk Kalemani.
Alisema katika kipindi cha kuanzia Julai 2012 hadi Novemba 2015, ukaguzi wa madini uliofanywa katika viwanja vya ndege kwa kushirikiana na vyombo vingine vya udhibiti, umebaini madini aina hiyo, dhahabu, fedha na madini mengine ya vito yenye uzito wa kilo 2,871 yenye thamani ya Sh16.4 bilioni katika matukio 87.
“Kuanzia Julai 2012 hadi Desemba mwaka huu thamani ya madini yaliyotoroshwa kwenda nje ya nchi kupitia viwanja vya ndege ni Sh 18.9 bilioni,” aliongeza.
Dk Kalemani alisema sekta ya madini nchini inachangia asilimia 3.5 ya uchumi na kwamba hadi kufikia mwaka 2025, uchumi wa sekta hiyo utakua kwa asilimia 10.
No comments:
Post a Comment