Sunday 13 December 2015

LUKUVI ATANGAZA BOMOA BOMOA NCHI NZIMA



Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvu amewataka wale wote ambao wamevamia maeneo ya wazi kuondoka mara moja na wasisubiri bomoa bomoa.




Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akihojiwa na waandishi wa habari, baada ya kuapishwa Ikulu, ambapo alieleza kuwa atafanyaka kazi zake kwa kuzingatia kasi ya Rais Dk. John Magufuli.

Waziri Lukuvi, alisema waliokiuka sheria za ardhi na kujenga kwenye fukwe za bahari, maeneo ya wazi na maeneo ya wananchi wajiandae kuondoka kwani kwa sasa amepewa rungu.

Alisema ataendelea na kasi yake ya kutetea watu wa hali ya chini ambao wamekuwa wakinyanyasika kwa muda mrefu.

“Wasisubiri nguvu zangu maana safari hii nina nguvu zaidi hivyo waliotumia fedha kupora maeneo ya watu ama kuvamia maeneo ya wazi ama ya ufukwe nitawaondoa,” alisema.

Lukuvi alisema kama Rais alivyofanya kwenye Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA) na yeye amejipanga kufanya hivyo hivyo kwenye maeneo yaliyoporwa.

Lukuvi alisema anatengeneza utaratibu maalum ambao utamwezesha mwananchi kuwasiliana naye moja kwa moja kuhusiana na tatizo la ardhi.

Aidha, alisema kipindi kilichopita alikuwa anapita na kuzungumza na wananchi, hivyo kwa sasa atatoa namba maalum ili watu wote waweze kusaidiwa matatizo yao katika ardhi.

“Lengo ni kuhakikisha Watanzania wenye shida ama walioonewa kwenye ardhi wanasaidiwa…. haiwezekani wenye fedha muwaonee wanyonge nawataka muondoke sehemu mlizovamia maana sasa nina rungu,” alisema Lukuvi.

Naye Naibu Waziri wake, Angelina Mabula alisema atajitahidi kufanya kazi kuendana na kasi ya Rais kwa kuwa ameonyesha kumwamini.

Alisema amepewa wizara ngumu yenye changamoto nyingi za migogoro ya ardhi, lakini ameahidi kulishughulikia suala hilo katika kuhakikisha wananchi wanapata haki zao.

Mabula alisema kuna baadhi ya viongozi wa serikali za mtaa wanakiuka miiko yao hali ambayo inasababishia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!