Siku chache baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, kupiga marufuku matangazo ya tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, waganga wa tiba hizo wameibuka na kupinga hatua hiyo.
Aidha, wamepinga uamuzi Wizara wa kutoa tamko hilo kupitia vyombo vya habari kwa madai kuwa wapo kisheria hivyo serikali ilipaswa kueleza uamuzi wake kwa kuwashirikisha kabla ya kutangaza.
Wakitoa tamko lao mbele ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, waganga hao walisema hatua iliyochukuliwa inadhihirisha kuwa serikali inawadharau na kutojali mchango wao.
“Hatukubaliani na utaratibu ambao haujatushirikisha, tunaomba tupewe elimu na miongozo ya kisheria kuhusu jambo hili kwa kuwa tunatambulika kisheria na kamati ya uongozi ambayo inaendelea na vikao itazingatia busara ya maneno yaliyoamuliwa katika mkutano huo,” alisema mmoja wa waratibu wa mkutano huo ambaye pia anahusika na utoaji wa tiba asili, Boniventura Mwalongo. Naye Mkurugenzi wa Rahabu Ulcers Clinic, Dk. Rahabu Rubago, alisema: “Nilipata mshtuko baada ya kupata taarifa za kukatazwa kurusha matangazo hadi kusababisha kulazwa kwa sababu nilikuwa nimetoka kulipia matangazo katika kituo kimoja cha runinga kwa muda wa mwaka mmoja.” Alisema kazi hiyo anaitegemea kwa kila kitu kwenye maisha yake ikiwamo kusomesha watoto na kwamba kutolewa kwa taarifa hiyo ameona anarudishwa nyuma. Kwa upande wake, Simon Rusigwa, wa Sure Herbal Clinic, alisema serikali imetoa agizo hilo bila kuwaeleza wadau sababu za kufanya hivyo na kwamba huko ni kuwaonea na kutofuata taratibu za tiba asili.
“Hatuendi nje ya sheria, tunataka sheria ifuatwe kwa kila kiongozi anayeingia madarakani,siyo kila anayekuja alete yake. Tusiposema hatutasikika, hivyo maagizo yaliyotolewa nadhani kila mmoja ameona hapo ndani wajumbe wote wa kikao chetu cha leo wameyakataa,” alisema Rusigwa.
Akizungumzia na Nipashe kuhusiana na tamko hilo la waganga, Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alisema tamko hilo la serikali limetolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni za afya. “Hakuna jambo jipya hata moja tulilofanya, kilichofanyika ni kusimamia Sheria Namba 23 ya mwaka 2002.
Licha ya kuwa tunawatambua wenzetu wa tiba za asili, lakini pia kuna sheria na kanuni wanapaswa kuzifuata kama kutojitangaza kwa namna yoyote ile.” Alifafanua kuwa kilichotokea kwa waganga hao ni kutokuelewa maana ya serikali hivyo walipaswa kufika wizarani kuomba ufafanuzi na wangekaa pamoja ili kuwekana sawa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Kuhusiana na matangazo ya waganga hao kuendelea kuruka katika vyombo mbalimbali vya habari alisema, hairuhusiwi na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao kwa kukiuka agizo la serikali.
“Hata hivyo, wengi tunatambua kuwa zipo changamoto mbalimbali katika utoaji wa tiba hizo na ni wajibu wetu kama Wizara kuhakikisha tunatatua changamoto hizi ili kuboresha sekta hiyo na kumaliza kasoro zilizopo,” alisema.
Desemba 24, mwaka huu, Dk. Kigwangalla alipiga marufuku matangazo yote yanayohusu tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kuwataka wenye vibali na matangazo yao waviwasilishe kwenye Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili vifanyiwe mapitio.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment