Saturday, 5 December 2015

KASI YA MAGUFULI YAREJESHA BILIONI 5/- TRA.



Wafanyabiashara mbalimbali waliokwepa kulipa kodi kwa kupitisha kinyemela mizigo bandarini, wamelipa jumla ya Sh. bilioni 5.2 kwa Mamlaka ya Mapato Nchini, huku fedha zaidi zikitarajiwa kuendelea kurejeshwa kwa TRA leo.
 
Tangu aingie madarakani kuchukua hatamu za serikali ya awamu ya tano Novemba 5, Rais John Magufuli ameweka mkazo katika kupiga vita ukwepaji kodi wa wafanyabiashara wakubwa, na juzi aliwapa siku saba waliokwepa kulipa bila adhabu. 
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Philip Mpango, alisema kampuni nne zimewasilisha fedha hizo, ikiwemo Said Salim Bakhresa and Company Limited ambayo imelipa Sh. bilioni 2.1.
 
Dk. Mpango alisema kampuni ya Bakhresa inalipia fedha hizo kwa sababu ilikuwa na dhamana ya makontena hayo kupitia Bandari Kavu (ICD) ya Azam.
 
Serikali ilimtaka alipie Sh. bilioni 12.6.
 
Aliyataja makampuni mengine kuwa ni Tuff Tyres Centre Co Ltd ambayo ililipa Sh. bilioni 1 mwanzoni mwa mwezi huu kati ya kodi aliyokadiriwa, Binslum Tyres Co. Ltd ililipa Sh. bilioni 1.4 Jumatano na ilipofika juzi alimalizia deni lake la Sh. bilioni 1.1.
 
Alisema kampuni ya Kiungi Trading Co. Ltd imelipia Sh milioni 506.7 Jumatano ikiwa ni jumla ya kodi iliyokadiriwa.
 
“Mchana huu  (jana) tunatarajia  Said Salim Bakhresa and Co. Limited atalipa Sh.bilioni 2 za nyongeza,” alisema Dk. Mpango.
 
Dk. Mpango alisema kuwa makontena hayo 329 yalianza kutoka tangu Julai mwaka huu hadi yalipobainika kuwa yamekwepa kodi baada ya Waziri Mkuu kufanya ziara ya kushtukiza Novemba 27 bandarini hapo.
 
Alisema kuwa baada ya zoezi hilo kumalizika watarudi miezi ya nyuma kuanzia Juni kuangalia wote ambao walikwepa kodi ili fedha zitakazobainika kuibwa kwa ukwepaji kodi ziweze kurejeshwa mara serikalini.
 
Aidha, alisema wote waliohusika na uondoshwaji wa makontena kutoka bandari kavu kinyume cha taratibu wajitokeze kwa hiyari yao kulipa kiasi cha kodi  yote inayodaiwa mara moja kabla ya muda wa siku saba za huruma zilizotolewa na Rais Magufuli kuanzia juzi kumalizika.
 
“Kwa mujibu wa Rais Magufuli amewataka wahusika wote kujitokeza na kulipa kodi zote wanazodaiwa ndani ya siku saba kinyume na hapo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
 
Aidha, Dk. Mpango alisema watumishi wa TRA wameagizwa kuwasilisha taarifa sahihi ya orodha ya mali zote wanazomiliki kwa ajili ya uhakiki wa kina.
 
Alisema mwisho wa zoezi hilo ni Desemba 15 mwaka huu na taarifa hizo zinatakiwa kuwasilishwa kwa uongozi wa juu ili ziaze kuhakikiwa mara moja.
 
Dk. Mpango alisema serikali ina mkono mrefu hivyo watakaodanganya taarifa za mali zao watajisumbua kwani watatumia vyombo vyote vya dola katika kufanya uhakiki.
 
“Zikiwasilishwa taarifa ambazo si zenyewe tutawachukulia hatua hapa tunataka kuona haki ya Waanzania inaonekana... ni dhambi kumiliki mali kwa kutumia nafasi ya umma uliyopewa badala ya kutafuta kihalali,” alisema
Wakati huo huo, Makontena tisa yaliyokamatwa katika eneo la Mbezi Tangi Bovu jijini Dar es Salaam imebainika kuwa mmiliki alikwepa kodi ya Sh milioni 58.4.
 
Fedha hizo ni pamoja na ada ya Forodha Sh. 3,665,708.80, tozo ya kuendeleza reli Sh. 8,201,738.30 na kodi ya pango la forodha Sh. 46,609,344.
 
Ilieleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mizigo yote ya EPZ hairuhusiwi kwenda kukaa kwenye bohari yoyote isiyo chini ya uangalizi wa Kamishna wa Forodha bila idhini.
 
Taarifa ya TRA, ilieleza kuwa kitendo cha kuondolewa makontena hayo kutoka bandari kavu ya PMM kwenda mtaani ni kinyume cha taratibu za Forodha.
 
Dk. Mpango alisema tozo zote zilizoainishwa ni za halali kisheria na zinastahili kulipwa na mwekezaji pamoja na faini.
 
”Mamlaka itakusanya mapato haya ya serikali kwa mujibu wa Sheria na kitendo cha kuondoa shehena hiyo ambayo imesamehewa kodi kwa ajili ya kutumika kwenye eneo maalum la EPZ, na kuipeleka eneo lingine kinatia shaka kama kweli shehena hiyo ingetumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na serikali,” alisema Dk. Mpango.
 
Shehena hiyo iliyokuwa na vifaa vya ujenzi wa kiwanda cha nguo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani inamilikiwa na Heritage Empire Company Limited. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!