Kasi ya utendaji wa Rais John Magufuli, imeibua upya sakata la ubomoaji wa jengo la ghorofa 16 ambalo serikali iliamuru libomolewe baada ya kutokidhi viwango lakini viongozi walionekana kulega lega katika utekelezaji wa agizo hilo.
Azma ya kubomolewa kwa jengo hilo lililopo mtaa wa Indira Ghand na Kisutu, kunafuatia tukio la Machi 29 mwaka 2013 baada kuporomoka kwa jengo pacha lililosababisha vifo vya watu 36, na kujeruhi wengine 18.
Hata hivyo, kazi ya kubomoa imeonekana ikisuasua kwa miaka mitatu kutokana na wakandarasi wanaopewa kazi hiyo kujitoa katika hatua ya mwisho wakitoa sababu mbalimbali.
Manispaa ya Ilala sasa imetangaza kufanya kazi hiyo haraka na tayari kampuni tatu za kimataifa zimejitokeza kufanya kazi hiyo.
Akizungumza na Nipashe, Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala, David Langa alisema Halmashauri hiyo ipo katika hatua ya mwisho ya kumpata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo.
Alisema mpaka sasa katika zabuni iliyotangazwa kuna kampuni tatu zilizojitokeza kutaka kazi hiyo na wako katika hatua za mwisho mwisho kumpata mshidi wa zabuni hiyo.
“Kuna mambo mengi ya kuangalia kabla ya kubomoa jengo, lazima tujiridhishe athari zitakazojitokeza katika usalama wa watu, mazingira na mali zingine,” alisema Langa.
“Muda si mrefu tutataja jina la kampuni itakayopewa kazi, ” aliongeza Langa.
Jengo hilo linamilikiwa kwa pamoja kati ya Shirika la la Nyumba la Taifa (NHC) na Ali Raza Investment, awali lilitakiwa kuvunjwa na kampuni ya kichina ya CRJ lakini ilishindikana.
NJIA YA KUBOMOA
Mtaalam mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema ubomoaji wa jengo la aina hiyo ni kazi ngumu na hapa nchini kuna kampuni na taasisi chache zenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Alisema kuna aina mbalimbali za ubomoaji salama wa majengo ya aina hiyo, lakini ina gharama kubwa.
Mtaalam huyo alisema kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha jengo hilo linaporomoshwa kwa kushuka chini na si vinginevyo kwa ajili ya kuepuka madhara.
Alizitaja njia hizo kuwa ni kubomoa kwa kuondoa ghorofa moja moja kutoka juu, lakini alionya njia hiyo ina hatari ya kukosea kisha sehemu ya ghorofa kuangukia makazi ya watu.
Alisema njia nyingine ni kutumia vyombo maalum vya kukatia na kuondoa vifusi.
“Kwa kutumia njia hii inakuwa rahisi kidogo, lakini mara nyingi kunahitajika vyombo na utaalamu wa hali ya juu ambao kwa nchi yetu ni vigumu kupata,” alisema mtaalam huyo.
Alitaja njia inayofaa na yenye madhara kidogo ni ubomoaji wa mabomu ambayo inapolipuka inaporomosha jengo kwa kulishusha chini.
Alisema mabomu hayo yanategwa kulingana na urefu wa jengo, kisha yanalipuliwa kufuata mtitiriko maalum ambao hautasababisha jengo kukatika na kuanguka.
“Mabomu haya yanategwa katika nguzo za kila ghorofa, halafu yanalipuliwa kuanzia juu kushuka chini, hivyo jengo litashuka chini na halitatawanyika,” alisema mtaalam huyo.
Hata hivyo alieleza kwamba njia hiyo inawezekana pale kazi hiyo itafanywa na vikosi vya Jeshi la Ulinzi au kampuni iliyothibitika inaweza kutumia utaalam huo.
HALI HALISI
Wakazi wanaoishi jirani na jengo hilo walisema kuchelewa kubomolewa inawazidishia hofu juu ya usalama wao na mali zao.
Hafidh Haroon alisema shughuli za biashara katika eneo hilo zimekuwa za mashaka kutokana na wasiwasi wa kuangukwa na jengo hilo.
“Tunafanya kazi zetu tukiwa na wasiwasi pengine linaweza kuanguka muda wowote tunaomba serikali kuingilia kati haraka kufanya kazi hiyo,” alisema Haroon.
Mwandishi wa gazeti hili alishuhudia majengo yaliyozunguka jengo hilo yakiwa hayana watu baada ya kuhama kunusuru maisha yao.
Hata hivyo baadhi ya maduka na huduma zingine za biashara zilizo jirani zilionekana kuendelea kutoa huduma kama kawaida.
Mara baada ya tukio hilo, la Machi 29, Aprili 5 mwaka 2013, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyeambatana na wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira walitembelea eneo hilo na kutoa siku 30 kwa mmiliki wa jengo hilo, Ally Raza kulibomoa baada ya kubainika kujengwa chini ya kiwango na sehemu isiyo zingatia mipango miji.
Kulingana na sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999, kifungu cha 44 na 45 na pia kanuni za ardhi za 2001 inaelekeza mhusika aliyekiuka masharti ya uendelezaji anapaswa kupewa ilani ya kubomoa na akiendelea kukaidi amri analipa faini ya asilimia mbili.
Hata hivyo, mmiliki huyo alikimbilia mahakamani kufungua kesi ya kupinga kubomolewa, kesi ambayo iliisha kutolewa hukumu ya jengo hilo linapaswa kubomolewa.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment