Thursday 24 December 2015

JAMII INAVYOPASWA KUHUDUMIA WALEMAVU!


NINA hakika sote tunajivunia siku hii, ambayo ningependa tuitumie kutafakari juu ya changamoto zinazowakabili watu wenye aina mbalimbali za ulemavu na kuweka mikakati ya pamoja ya kujenga jamii ya watu walio huru na sawa.” Hiyo ni kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ambayo kitaifa ilifanyika jijini Mwanza.

Hii ni sherehe pekee iliyoruhusiwa na Rais Magufuli baada ya kufuta sherehe zote za kitaifa kwa lengo la wananchi kuzitumia sherehe hizo katika kufanya kazi.
Kwenye sherehe hiyo, Rais aliishukuru kamati ya maandalizi ya mkoa wa Mwanza, Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (Shivyawata), taasisi mbalimbali na wadau wa masuala ya ulemavu kwa maandalizi mazuri yaliyofana ya sherehe hizo. Baadhi ya sherehe zilizofutwa na Rais Magufuli ni pamoja na ile ya uhuru ambayo aliagiza watu waitumie katika kufanya usafi kwenye maeneo yao na maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani.
Aidha ameelekeza fedha ambazo zingetumiwa kwenye maadhimisho zitumike kuwasaidia waathirika wa Ukimwi kwa kuwanunulia dawa, lishe na huduma nyingine muhimu.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na watu wenye ulemavu wa aina zote kutoka mikoa yote nchini, wakuu wa wilaya, viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu, viongozi wa madhehebu ya dini za Kikristo na Kiislamu, wanasiasa na wananchi. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ilikuwa ni “Ujumuishaji ni muhimu; ufikiaji na uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu, wanao uwezo wa kutenda mambo ya aina moja au nyingine wakiwezeshwa na kupewa fursa sawa katika jamii.”
Dk Magufuli anasema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2011, takribani watu bilioni moja wana changamoto za ulemavu wa aina mbalimbali. Kati ya hao, anasema asilimia 80 wanaishi katika nchi zinazoendelea na zenye uchumi wa kati. Anaongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya watu wenye ulemavu 2,641,802 sawa na asilimia 5.8 ya wananchi wote.
Kati yao, watu wenye ualibino ni 16,477 sawa na asilimia 0.04 ya watu wote, wasioona ni 848,530 sawa na asilimia 1.93, kusikia 425,322 sawa na asilimia 0.97, kujongea 525,019 sawa na asilimia 1.19, kukumbuka 401,931 sawa na asilimia 0.91, ulemavu wa kujihudumia 324,725 sawa na asilimia 0.74 na ulemavu mwingine 99,798 ikiwa ni sawa na asilimia 0.23.
Rais anazitaja sababu zinazochangia ulemavu huo ni pamoja na urithi, magonjwa ya kuambikiza na yasiyo ya kuambukiza, ajali, athari za dawa na pombe pamoja na changamoto katika upatikanaji wa huduma za afya. Rais anasema kauli mbiu ya mwaka huu inaakisi matakwa ya Sheria ya Watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 pamoja na sera, miongozo na mipango mbalimbali ya serikali kuhusu huduma za watu wenye ulemavu.
“Serikali yangu ya awamu ya tano itahakikisha kuwa haki, ufikiaji na uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu nchini vinatekelezwa kwa vitendo”, anasema.
Kuhusu changamoto za watu wenye ulemavu, Rais anasema serikali imezipokea changamoto hizo ambazo ni kukosekana kwa watu wenye ulemavu kwenye vikao vya maamuzi, kukosekana ofisi ya kudumu ya Shivyawata, miundombinu ya majengo isiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu na kukosekana kwa alama maalumu za barabarani ambazo zingefanya watumiaji wa barabara waziheshimu ili kuwezesha watu wenye ulemavu wazitumie.
“Tumepokea mapendekezo yote ya watu wenye ulemavu na tunaahidi kuyafanyia kazi kwa kuzingatia sheria na sera zinazosimamia utumishi wa umma na utoaji wa huduma za kijamii,” anasema na kuongeza:
“Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha makundi mbalimbali ya jamii yanapata huduma bora za afya bila ubaguzi wala unyanyapaa wa aina yoyote”, anasema.
Anasema ili kufikia azma hiyo, hatua mbalimbali zitachukuliwa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya kwa kila kata, hospitali kwa kila halmashauri na hospitali ya rufaa kwa ngazi ya mikoa.
“Serikali itahakikisha upatikanaji wa wataalamu wa afya katika ngazi zote pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika taasisi hizo za afya nchini na sanjari na kukamilisha mwongozo wa uchangiaji wa huduma za afya nchini utakaotoa utaratibu wa upatikanaji wa huduma,” anasema.
Anasema kuhusu ukatili na unyanyasaji na mauaji ya watu wenye ualbino ambayo yamekuwa yakichochewa na imani za kishirikina ambapo baadhi ya watu wanaamini wakipata viungo vya watu wenye ualbino watatajirika na kupata vyeo au tiba kwa magonjwa sugu kama vile Ukimwi.
“Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa vitendo hivi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda lakini tusibweteke na mafanikio haya badala yake juhudi hizi ziongezwe ili tatizo hili liwe la kihistoria,” anasema.
Akisoma risala ya watu wenye ulemavu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Shivyawata, Blandina Sembu aliishukuru Serikali kwa kusaini na kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu wenye ulemavu wa mwaka 2006 na kwa kupitisha Sheria Na. 9 ya haki za watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 na kanuni zake.
Anaishukuru serikali kwa kuwateua watu 20 wenye ulemavu kujumuika na wabunge wengine kwenye Bunge Maalumu la Katiba na kuwezeshwa kumalizika kwa Katiba inayopendekezwa kukabidhiwa kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Dk Jakaya Kikwete.
Anasema pamoja na mafanikio hayo, watu wenye ulemavu bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa vikwazo katika kuzifikia huduma muhimu za kijamii na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo.
Anazitaja changamoto hizo kuwa ni upatikanaji wa taarifa muhimu katika mifumo isiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu, kukosa kwa taarifa muhimu zinazotangazwa kwa watu wenye ulemavu wa kusikia kupitia luninga kutokana na kukosa kwa wakalimani wa lugha ya alama.
Changamoto nyingine kwa mujibu wake ni kuendelea kwa vitendo vya kikatili kama vile mauaji na ukatwaji viungo kwa watu wenye ualbino, kundi ambalo limeelezwa kufikwa na madhila mengi ya kikatili.
“Pia kukosekana kwa uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika vyombo vingi vya maamuzi kuanzia ngazi za Serikali za mitaa hadi serikali kuu na hivyo kusababisha mahitaji ya watu wenye ulemavu kusahaulika,” anasema.
Mapendekezo serikalini Sembu alisema kuwa Shivyawata kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya ulemavu imependekeza mambo manne muhimu serikalini ili serikali iyashughulikie.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuitaka serikali kuhimiza uwepo wa wakalimani wa kutosha wa lugha ya alama kwenye vyombo vyote vya habari nchini, kukomesha vitendo vya ukatili vya mauaji ya watu wenye ualbino unaosababishwa na imani potofu.
Awali Mwenyekiti wa Shivyawata nchini Amon Mpanju licha ya kumshukuru Rais Magufuli kwa kuanza kazi kwa kasi ya ajabu, anamshukuru pia kwa kuruhusu kufanyika kwa sherehe za watu wenye ulemavu nchini hali ambayo alisema ameonesha upendo mkubwa kwao.
“Tunajua Rais amefuta maadhimisho ya sherehe na sikukuu nyingi, lakini kutokana na upendo wake kwetu, ameturuhusu kushiriki katika maadhimisho, hii ni dalili kuwa anatujali na kututhamini,” alisema, na kuongeza, “Tunamshukuru Rais kwa kuruhusu wakurugenzi watendaji nchini kutusafirisha kwenye maadhimisho haya, hii kwetu ni ishara ya yale aliyoahidi wakati wa kampeni kuwa atayashughulikia matatizo ya watu wenye ulemavu na ameanza kuyatekeleza, tunamshukuru sana Rais wetu.”
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Rabikira Mushi alisema Serikali imefanya mambo mengi ya kujivunia kimataifa katika kuwapatia maendeleo endelevu watu wenye ulemavu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Rais Magufuli alitoa zawadi za viti vinne (wheel chair), mafuta ya kupaka (lotion) 88, fimbo nyeupe 50, kofia 232 na miavuli minne kwa watu wenye ulemavu na ualbino.
Aidha Rais kwenye maadhimisho hayo alizawadiwa zawadi maalumu ya shati kutoka kwa fundi mkuu wa ushonaji nguo kutoka kundi la walemavu wasioona, Abdalla Ngalu ambaye aliomba zawadi hiyo akabidhiwe Rais mwenyewe.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!