skip to main |
skip to sidebar
Hatimaye almasi ya pinki ya Mwadui yauzwa bilioni 21 ($-10m) huko Ubelgiji
Almasi Adimu ya rangi ya Pinki iliyochimbwa nchini mwezi Novemba, 2015, katika mgodi wa Williamson unaomilikiwa na Kampuni ya Dhahabu ya Petra Diamond Mwadui, Shinyanga, imeuzwa katika mnada jijini Antwerp Ubelgiji kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 10,050,000, ambazo ni zaidi ya shilingi Bilioni 21 za kitanzania.
Kampuni ya Madini ya Petra iliuza Almasi hiyo adimu ya Pinki yenye uzito wa carat 23.16, tarehe 9 Disemba, 2015, kwa kampuni ya Golden Yellow Diamonds ambayo ilinunua kwa niaba ya Kampuni ya M.A Anavi Diamond, kampuni kongwe inayoongoza katika kutengeneza almasi zenye ukubwa na rangi za kipekee.
Katika mauzo hayo ambayo pia yalishuhudiwa na Afisa Mthamini Mwandamizi kutoka Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almas (TANSORT), Wizara ya Nishati na Madini, kampuni ya Petra iliuza almasi hiyo kwa kiasi cha Dola za Marekani 433,938 kwa kila carat, ikiwemo kubakiwa na riba ya asilimia 20 ya mauzo.Akizungumza baada ya mauzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Petra, Johan Dippenaar, alisema kuwa,
"Matokeo ya mauzo haya yanaendelea kuthibitisha kuwa soko la almasii za rangi zenye ubora wa juu inabaki kuwa imara. Almasi yenye ukubwa huu ni nadra sana kupatikana lakini Williamson inajulikana kwa kuzalisha madini ya aina hiyo kwa vipindi tofauti," alisema Dippenaar.
Taarifa kutoka kampuni hiyo imeeleza kuwa, Almasi ya rangi ya Pinki ya kwanza kuzalishwa katika mgodi wa Williamson ilipatikana mwaka 1947 ambapo inatajwa kuwa ya pekee kuwahi kutokea ikiwa na uzito wa carat 54. Mmiliki wa mgodi kwa kipindi hicho, alikuwa Mjiolojia raia wa Canada, Dkt. John Williams ambaye alitoa Almasi hiyo kama zawadi ya harusi kwa Malkia Elizabeth wa Uingereza.
Nchini Tanzania, Kampuni ya Petra, ni pekee inayozalisha madini ya almasi ambapo inamiliki eneo la kiasi cha hekta 146 Mwadui Shinyanga. Mbali na Tanzania, Kampuni hiyo inamiliki migodi minne katika nchi ya Afrika Kusini, vilevile inaendesha mpango wa utafiti katika nchi ya Botswana.
Almasi za mgodi wa Williamson na almasi nyingine kutoka nchi mbalimbali duniani huuzwa katika mnada wa madini hayo uliopo jijini Antwerp, nchini Ubelgiji. Vilevile, mgodi huo huzalisha almasi zenye ubora wa hali ya juu zinazofikia wastani wa thamani ya Dola za Marekani 298 kwa karat moja kama ilivyoshuhudiwa katika mwaka 2015.
Kumbe Tanzania tuna madini ya maana sana na hawa wachimbaji wanapata faida kubwa Ingawa makampuni mengi ya uchimbaji madini yanajifanyaga hayajapata faida kila yakitakiwa kutoa kodi.
Almasi yenyewe ndio hii hapa kwa picha.
Last edited by MeinKempf; Today at 12:20.
No comments:
Post a Comment