Thursday 3 December 2015

HABARI KAMILI KUHUSU AJALI YA BASI LA TAKBIR


Watu 12 wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa vibaya mkoani Singida, baada ya basi la Taqbir kupata ajali  katika Kijiji cha Kizonzo Kata ya Shelui Wilaya ya Iramba.


 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, alisema ajali hiyo ilitokea juzi katika eneo hilo kwenye Barabara Kuu ya Singida-Nzega majira ya saa 1:30 usiku, kwa kuhusisha basi hilo lenye namba za usajili T 240 BRJ aina ya Scania ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda jijini Mwanza.
 
Sedoyeka alisema ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa basi hilo akijaribu kulipita gari la Kampuni ya Coca Cola lililokwa mbele, kabla ya kugongana na lori la mafuta lililokuwa linakuja mbele yake kisha kupoteza mwelekeo na kuparamia gari lingine.
 
Kamanda Sedoyeka aliwataja majeruhi 18 wa ajali ya hiyo kuwa ni Godriver Simon (40) mkazi wa Chato, Veronica Mathias (25) wa Igunga, Peter Lusangaje (38) wa Geita, Rhoda Mbata (42) wa Geita na Osca Kusenza (46) wa Katoro.
 
Wengine ni Yusufu Elisha (32) wa Kahama, Edwin Mgeta (25) wa Dar es Salaam, Maria Thomas (37) wa Nanga Tabora, James Godavi (32) wa Singida, Maria Ibisi (52) wa Igunga, Magrath Busanda (24) wa Masumbwe na Baraka Yusufu (miaka miwili) wa Kahama. Majeruhi wengine ni Sophia Thomas (32) wa Igunga, Seth Paul (22) wa Nyakanazi, Lucas Joseph (mwaka mmoja) mkazi wa Igunga Tabora, Hamisi Masudi (60) mkazi wa Igunga , Anasitazia Musa (22) wa Igoma Mwanza na Theresia Nyanga (70) wa Igunga mkoani Tabora.
 
Hata hivyo Sedoyeka alisema kuwa, majina ya marehemu waliokufa katika ajali hiyo bado hayajafahamika lakini Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kuwatambua. Akielezea hali halisi ilivyokuwa Kamanda Sedoyeka alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi, kwa kukosa umakini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
 
Kamanda huyo alisema basi hilo limeharibika vibaya upande wa kulia jambo ambalo limesababisha vifo vya watu 12 wakiwamo watoto wadogo watatu, huku majeruhi wakiwa 18 ambao wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Iramba iliyopo Kiomboi mjini na kwamba hali zao zimeelezwa kuwa ni mbaya.
 
 Kamanda Sedoyeka, alisema licha ya dereva wa basi kujitahidi kulidhibiti basi hilo umbali wa zaidi ya mita 300, lakini kutokana na upande wa kulia kuharibika vibaya (kuchanwa), ndiko kulikochangia kutokea kwa vifo na majeruhi hao. 
 
Akizungumzia majeruhi aliyowapokea, Kaimu Mganga Mfawidhi katika hospitali hiyo, Dk. Timoth Sumbe, alisema hali zao si za kuridhisha, na kwamba wengine wamekatika baadhi ya viungo vyao.
 
Katika hatua nyingine, Dk. Sumbe, alisema chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo ni changamoto kubwa, hivyo wamejikuta maiti nyingi zikiwa chini ya sakafu hali ambayo zitalazimika kuhamishia Hospitali ya Mkoa ili kutambuliwa na ndugu na jamaa zao.
 
Kamanda Sedoyeka alisema kuwa dereva wa basi hilo hadi sasa hajapatikana baada ya kutoroka mara baada ya ajali hiyo kutokea na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada ya kumtafuta ili kumfikisha mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!