Wednesday, 16 December 2015

DHAMANA YA VIGOGO TRA NI SH2.16 BILLIONI

Washtakiwa wanaodaiwa kula njama na

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa masharti magumu ya dhamana kwa vigogo watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kati ya washtakiwa wanane wa kesi ya uhujumu uchumi, kutokana na sakata la makontena yaliyoondolewa katika Bandari Kavu ya Azam bila kulipa kodi.


Washtakiwa hao ni aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru, Tiagi Masamaki (56), Meneja wa Huduma za Ushuru, Habib Mponezya (45) na Meneja Msimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton Mponezya (51).
Ili kupata dhamana, washtakiwa hao wanatakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh2.16 bilioni wote kwa pamoja, au hati za mali zisizohamishika, zenye thamani sawa na kiasi hicho.
Washtakiwa hao wametakiwa kuwasilisha fedha hizo au hati za mali zenye thamani sawa na kiasi hicho, ambacho ni sehemu ya nusu ya hasara wanayodaiwa kuisababishia Serikali (Sh12.7bil). Nusu ya hasara hiyo ni zaidi ya Sh6.3 bilioni.
Masharti mengine ni kuwasilisha hati zao za kusafiria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako ndiko wanakokabiliwa na kesi hiyo, kuwa na wadhamini wawili, ambao mmojawao ni mtumishi wa umma.
Pia, wanatakiwa kuripoti kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa kila baada ya majuma mawili, kutokutoka nje ya Dar es Salaam bila idhini ya Mahakama ya Kisutu.
Uamuzi wa washtakiwa hao kupewa dhamana na masharti yake ulitolewa jana na Jaji Winfrida Korosso kutokana na maombi waliyoyawasilisha mahakamani hapo kupitia kwa mawakili wao, Majura Magafu na Alex Mgongolwa.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Korosso aliwataka washtakiwa hao wawasilishe hati hizo za dhamana, vitambulisho na barua za utambulisho wa wadhamini kwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya uhakiki ambao unapaswa kufanyika ndani ya saa 24, tangu kuwasilishwa.
Licha ya Mahakama kuridhia maombi yao ya dhamana, washtakiwa hao walirejeshwa mahabusu wakisubiri kukamilika kwa uhakiki wa nyaraka hizo.
Washtakiwa hao waliwasilisha maombi hayo ya dhamana Mahakama Kuu, kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walikofunguliwa mashtaka kwa hatua za awali, kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo jana, mawakili wa washtakiwa hao, Mgongolwa na Magafu waliieleza Mahakama kuwa wanaomba dhamana kwa wateja wao kwa kuwa ni haki yao kwa mujibu wa sheria na kwamba hawajawekewa pingamizi lolote.
Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Timon alisema mjibu maombi hana pingamizi dhidi ya maombi hayo kwa sababu makosa yanayowakabili yanadhaminika ili mradi washtakiwa watimize masharti ya dhamana watakayopewa.
Katika kesi ya msingi inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya uhujumu uchumi, wakidaiwa kula njama na kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.7 bilioni.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha ICD Azam, Eliachi Mrema (31); Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamis Omary (48), Haroun Mpande (28) wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta (ICT); Meneja wa Operesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Adolf Louis (39) na Meneja wa Azam ICD, Ashraf Khan (59).
Wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 17, walikula njama kwa kuidanganya Serikali kuwa makontena 329 yaliyokuwapo ICD ya Azam (AICD) yalitolewa baada ya kodi zote kufanyika wakati wakijua si kweli.
Katika shtaka la pili, wanadaiwa kuwa katika kipindi hichohicho, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.7 bilioni.
Walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa ajili ya hatua za awali, juma lililopita, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo hawakutakiwa kujibu lolote na badala yake Hakimu Shaidi aliwashauri kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Kesi hiyo ya msingi imepangwa kuendelea tena Mahakama ya Kisutu Desemba 17, 2015, kwa kutajwa kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!