Sunday 27 December 2015

CHURA KIUMBE ANAYEVUTA HEWA KUNYWA MAJI KUPITIA NGOZI YAKE


Chura ni viumbe wasiokuwa na mkia ambaye kisayansi amepangwa katika kundi la amphibia, ana uwezo wa kuishi majini na nchi kavu. 

Kiumbe huyu ana miguu mirefu ya nyuma, mwili mfupi, macho yaliyotokeza kwa nje, vidole vilivyounganishwa kwa utando mithiri ya miguu ya bata na mwenye mwendo wa kuruka ruka.
Miguu ya nyuma ni mirefu, imara  na yenye nguvu humsaidia chura kuruka vizuri na kusafiri umbali mrefu kwa mwendo wake huo wa kuruka ruka.
Chura ana ngozi ngumu lakini yenye hali ya utepetepe ambayo humuwezesha kuishi hata kwenye maeneo yenye unyevunyevu au kwenye maji.
Ingawa chura ana uwezo mkubwa wa kupiga mbizi ndani ya maji, anaweza kusafiri kirahisi zaidi nchi kavu kuliko ndani ya maji.
Kwa kawaida chura hutaga mayai yake majini hasa katika maji yaliyotulia kama vile katika bwawa, madimbwi au ziwani.
Mayai ya chura yanapoanguliwa, kabla ya kuwa chura kamili hupitia katika hatua kadhaa za ukuaji.
Awali punde tu baada ya mayai ya chura kuanguliwa hutokea viumbe vyenye vichwa vikubwa vikiwa na mkia mwembamba lakini mrefu kiasi.
Viumbe hivyo kisayansi huitwa lava ingawa kwa lugha ya kitaalamu zaidi ‘tadpoles’ yaani viluwiluwi, ambavyo huendelea kukua vikiwa ndani ya maji hadi pale vinapokatika mikia na kuwa chura kamili.
Chakula kikuu cha vyura ni nyama ya viumbe wengine kama vile wadudu walio katika kundi la arthropoda hivyo kisayansi kujikuta wakiangukia katika kundi la wanyama wanaokula nyama ambalo huitwa carnivorous.
Mtawanyiko wa vyura katika uso wa dunia umesambaa katika maeneo yote yenye hali ya kitropiki hadi pembezoni mwa ncha za dunia za kusini na kaskazini, lakini aina nyingi za wanyama hawa zinapatikana kwenye maeneo ya kitropiki ambayo kwa kawaida huwa na misitu na mvua nyingi kwa mwaka.
Vyura ni wanyama wenye uti wa mgongo ambao wamefanyiwa utafiti na kubainika kuwa kuna  zaidi ya aina 5,000 za wanyama hawa, ingawa wanasayansi wamewagawanya katika makundi mawili makubwa ambayo yanajulikana zaidi kwa majina ya ‘frogs’ na ‘toads’ kutokana na mwonekano wao.
Vyura wanachukua zaidi ya asilimia 88 ya wanyama walio katika kundi la amphifia na sehemu iliyobaki inaundwa na aina chache za wanyama kama vile salamanda na caecilians ambao pia kisayansi wamepangwa katika kundi hili la Amfibia.
Hata hivyo kundi la chura ndilo la wanyama wasio wa kawaida katika kundi hili la amfibia kulinganisha na aina hizo nyingine za wanyama wa kundi hili kutokana na kutokuwa na mkia katika hatua yake ya ukubwa (adult stage), huku miguu yake ikiwa na uwezo wa kuruka badala ya kutembea.
Sifa nyingine ya chura isiyokuwa ya kawaida ni uwezo wake wa kuvuta hewa ya oksijeni na na kupumua kwa kutumia ngozi yake. Ngozi ya chura ina uwezo wa kuingiza oksijeni ndani ya mwili wake na hewa hiyo kuingia moja kwa moja kwenye mishipa ya damu.
Kwa kuwa chura hutakiwa kuingiza mwilini hewa ya oksijeni kwa kutumia ngozi yake, ngozi hiyo hutakiwa kuwa katika hali ya unyevunyevu muda wote ili kuwa rahisi kwake kuvuta hewa hiyo.
Maumbile ya vyura hutofautiana kulingana na aina au jamii ya vyura ambapo vyura wenye umbile dogo kabisa wanapokuwa tayari wamekomaa wana urefu wa milimeta kumi na wanapatikana kwa wingi nchini Brazil na Cuba.
Mpenzi msomaji na mfuatiliaji wa safu hii, Chura ni mnyama mwenye mambo mengi ambayo kwa leo siwezi kuyaeleza yote kutokana na ufinyu wa nafasi, kwa sasa naomba niishie hapa lakini nikualike wiki ijayo kwa ajili ya kujipatia sehemu ya pili na ya mwisho kuhusiana na mnyama huyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!