Tuesday 8 December 2015

BOMOA BOMOA MPYA YALIZA MAMIA DAR


Zaidi ya nyumba 100 zilizopo King’azi kata ya Kwembe Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, zimevunjwa na kusababisha wakazi zaidi ya 300 kukosa makazi.
 
Tukio hilo la kuvunja nyumba hizo lilifanyika jana na uongozi unaodaiwa kuwa ni kutoka Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ambao ulifika katika eneo hilo asubuhi na kuanza kubomoa nyumba hizo.
 
Katika bomoa bomoa hiyo, maofisa hao waliongozana na gari mbili za polisi, watu zaidi ya 50 wa jamii ya Kimasai waliobeba marungu, mapanga na sime.
 
Kabla ya kuanza kuvunja nyumba hizo, kuliibuka vurugu  kati ya wakazi wa eneo hilo na wa jamii ya Kimasai ambao walikuwa wanazuia nyumba zao kuvunjwa huku lakini watu hao waliovalia nguo kama za jamii ya Wamasai, wakiwafukuza kwa kutumia nyenzo hizo.
 
Akizungumza na Nipashe Mwenyekiti wa mtaa huo wa King’azi, Selemani Beho, alisema eneo hilo lilikuwa na mgogoro na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Aneth Nkinda na kesi ilikuwa inaendelea jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini kabla ya hukumu kutolewa, nyumba hizo zikavunjiwa.
 
Alisema kesi hiyo ilitarajiwa kupangiwa tena tarehe ya kusikilizwa Januari 19, mwakani.
 
Beho alisema yeye hakuwa na taarifa za kuvunjwa kwa nyumba hizo jana na pia anashangaa kazi hiyo kufanywa na uongozi kutoka katika wilaya nyingine.
 
Alisema jumla ya nyumba anazofahamu kuwapo katika eneo hilo ni 180 na zote zimevunjwa.
 
Alisema aliwasiliana na Polisi wa Kituo cha Kimara ambao walisema hawana taarifa yoyote kuhusiana na uvunjwaji wa nyumba hizo.
Aidha, alisema hakuna mali yoyote iliyoikolewa katika nyumba hizo.
 
Pia alisema wakati watu hao wakivunja nyumba hizo, inahofiwa watoto wawili wa familia moja walifariki dunia.
 
Alisema watoto hao waliachwa na wazazi wao ndani ya nyumba  hiyo na hadi kufikia jana jioni walikuwa hawajajulikani mahali walipo.
 
Baba wa watoto hao, Saimoni Kelakela, alisema aliondoka nyumbani tangu asubuhi na kuwaacha watoto hao wakiwa na mama yao.
 
Hata hivyo, alisema mama yao aliondoka kabla nyumba yao haijavunjwa na kuwaacha watoto hao na aliporudi alikuta imebomolewa. 
 
Mjumbe wa mtaa huo, Dickson Kweka, alisema zaidi ya watu 10 wameumia kwa kukatwa mapanga na watu hao wanaodhaniwa kuwa ni jamii ya Wamasai wakati wakijaribu kuzuia nyumba zao kubomolewa.
 
Mmoja wa walijeruhiwa kwa mapanga na watu hao, Ezron Madete, alisema alikutwa na mkasa huo wakati akijaribu kuzuia nyumba yake kubomolewa.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Kimara,  ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema hakuwa na taarifa yeyote ya bomoabomoa hiyo.
 
Akizungumza na wananchi hao, alisema anawasiliana na uongozi wa juu kuangalia utaratibu utakaoendelea wa kuwasaidia waathirika hao ikiwamo kuangalia namna ya kuwapatia misaada ya kibinadamu.

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!