Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imesema kuwa ina uwezo wa kufungua maduka ya dawa katika hospitali za rufaa na mikoa nchini kama ilivyoagizwa na Rais John Magufuli.
Imesema mwanzoni mwa wiki ijayo, itafungua maduka ya dawa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru iliyoko Mkoa wa Arusha na Bugando ya jijini Mwanza.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli.
Alisema MSD itahakikisha maduka hayo pia yanakuwa na dawa za kutosha ili wagonjwa wasisumbuke kwenda kutafuta dawa mitaani.
Nipashe ilitaka kujua uwezekano wa kutekeleza agizo hilo wakati MSD ikiidai Serikali zaidi ya Sh. bilioni 120, deni ambalo imedaiwa limepunguza uwezo wa chombo hicho kujiendesha.
Alisema katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, wanatarajia kufungua duka hilo mwishoni mwa mwezi huu.
Aidha, alisema kwa sasa MSD inasubiri kupokea maombi ya dawa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwani ndiyo inayofahamu mahitaji ya dawa katika hospitali hizo nchini.
Bwanakunu alisema msongamano wa wateja uliopo katika duka la dawa la Muhimbili umetokana na kuwa hospitali pekee ambayo inauza dawa jijini Dar es Salaam.
“Sisi MSD mteja wetu tunayemuuzia dawa ni Muhimbili na yeye analeta maombi kulingana na mahitaji ya hospitali zote nchini na tumeweka utaratibu kwamba hakuna mgonjwa atakayeuziwa dawa bila ya kuwa na karatasi maalum kutoka kwa daktari,” alisema.
Bwanakunu alisema kuna changamoto ya uchelewaji wa dawa kufika nchini kutokana na dawa hizo kuagizwa nje ya nchi na kupitia mchakato mrefu.
“Tunaagiza dawa kutoka nje hivyo katika ‘item’ 600 zinaweza zikafika 200 na uagizaji huo una mchakato mrefu wa manunuzi na kutolewa kwa zabuni kwa waagizaji,” alisema Bwanakunu.
Hatua ya MSD ya kufungua maduka ya dawa katika hospitali za serikali inatokana na lengo la Rais Magufuli kurahisishia upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa hospitalini pamoja na kudhibiti vitendo vya wizi wa dawa za serikali.
No comments:
Post a Comment