Siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kufanya ziara ya kushtukiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, hali imebadilika ghafla ambapo huduma za matibabu zimeanza kutolewa haraka na kwa ufanisi.
Aidha, uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya mazungumzo na kampuni ya Philips kutengeneza mashine mbili za CT-Scan na MRI za vipimo mbalimbali vya magonjwa.
Juzi, Rais Dk. Magufuli alivamia ghafla hospitalini hapo kisha kumuondoa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Hussein Kidanto pamoja na kuivunja Bodi ya Hospitali baada ya kutoridhishwa na utendaji wao wa kazi.
Nafasi yake imechukuliwa na Profesa Lawrance Mseru, ambaye alianza kazi hiyo jana saa 4:00 kwa kufanya vikao na Menejimenti na Kamati Tendaji ya Hospitali.
KUANZA KUKARABATI MASHINE
Akizungumza na Nipashe, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya mazungunzo na kampuni ya Philips kwa ajili ya kutengeneza mashine zilizoharibika.
Alisema kazi hiyo itafanyika hivi karibuni baada ya wataalam wa kampuni hiyo kuwasili kwa kazi hiyo.
Alisema wana matumaini ya mashine hizo kufanya kazi kwa muda waliopewa na Rais Magufuli.
“Tutakamilisha kazi hii ndani ya kipindi tulichopewa, tunachofanya sasa ni kuzungumza na kampuni husika waje kuzitengeneza ili tuanze kutoa huduma haraka kwa wagonjwa,” alisema Aligaesha.
PROFESA MSERU AANZA KAZI
Akizungumzia Mkurugenzi mpya, Aligaesha alisema kwamba Profeza Mseru aliripoti jana saa 4:00 asubuhi na kuitisha vikao mbalimbali kwa ajili ya kujua utendaji kazi wa hospitali hiyo.
Alisema baada ya kukamilisha kazi ya kukutana na makundi mbalimbali ya wafanyakazi, atazungumza na vyombo vya habari kuelezea kazi yake hiyo mpya.
HALI ILIVYO SASA
Gazeti hili liliwashuhudia madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo wakifanya kazi kwa kasi tofauti na siku za nyuma.
Wodi nyingi zilionekana kuwa na madaktari muda wote, kitu ambacho wagonjwa walieleza kwamba kimewafurahisha.
Hata hivyo, katika daftari la mahudhurio, imeelezwa madaktari bingwa kwa mara ya kwanza wamejihorodhesha mapema asubuhi.
“Ninachokuambia leo ni mchakamchaka kila mtu anawajibika, kwa mara ya kwanza madaktari bingwa wamesaini daftari la maudhurio,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
AGIZO LA MAGUFULI LATEKELEZWA
Mgonjwa Chacha Makange, ambaye Rais Magufuli aliagiza apatiwe matibabu pamoja na vipimo, alisema ndani ya dakika sita zimebadilisha maisha yake na wagonjwa wengine.
Chacha ambaye anafahamika kutokana na kuishi ndani ya handaki kwa miaka mitano maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema jana alipatiwa vipimo katika kituo binafsi cha kupimia magonjwa cha Besta kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Alisema anamshukuru Mungu kumkutanisha na Rais Magufuli na kusababisha maisha yake kubadilika ghafla.
Chacha alisema alipomuona Dk. Magufuli, alimuomba aongee naye dakika tano, lakini Rais alimpa dakika moja ya kuzungumza.
Hata hivyo, baada ya kuguswa na matatizo yake, kiongozi huyo alimuongezea dakika nyingine tano na kuwa sita ambazo hatimaye zilibadilisha mfumo mzima wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Nilipoanza kuongea, Rais aliguswa, aliniangalia na kuniambia niendelee, nilitumia dakika sita kueleza matatizo yetu, namshukuru Mungu amepanga haya yote yatokee kwa ajili ya Watanzania,” alisema Chacha.
Aliomba jamii ishirikiane katika kufarijiana na kusema bila hiyo hakuna upendo wa kweli.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk. Othman Kiloloma, alisema mgonjwa huyo amefanyiwa vipimo vyote na kitu kilichobaki ni kuvisoma na kumpatia tiba sahihi.
Alisema Chacha anasumbuliwa na matatizo ya mgongo, hivyo matibabu yake yananahitaji umakini na muda mrefu.
“Tumetekeleza agizo la Rais, leo (jana) tulimpeleka mgonjwa katika vipimo vyote, tunachoangalia hapa ni kufanya matibabu yake yanayoendana na matatizo aliyokuwa nayo,” alisema Dk. Kaloloma.
Akizungumzia tatizo la wagonjwa kulala chini, Dk. Kaloloma alisema litaondoka baada ya kufunguliwa kwa jengo jipya kutokana na wodi zilizopo kutohimili idadi kubwa ya watu wanaohitaji kupata huduma.
No comments:
Post a Comment