Friday, 27 November 2015

WAZIRI MKUU MAJALIWA KASSIM MAJALIWA ASIMAMISHA KAZI VIGOGO WA TRA NA KUAGIZA WAKAMATWE KWA UPOTEVU MABILIONI YA KODI


Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akigonga kengelle kuashiria uzinduzi wa ununuzi wa  hisa za Benki ya Walimu- MCB kwenye soko la hisa la Dar es Salaam. Uzinduzi huo ulifanyika  jijini humo.




Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua uuzaji wa hisa za Benki ya Walimu MCB kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, uliofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 27, 2015.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akiteta na baadhi ya Viongozi wa Benki ya Walimu-MCB baada ya kuzindua uuzaji wa hisa za Benki hiyo katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua uuzaji wa hisa za Benki ya Walimu MCB kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, uliofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 27, 2015.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua uuzaji wa hisa za Benki ya Walimu MCB kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, uliofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 27, 2015.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akiteta na baadhi ya Viongozi wa Benki ya Walimu-MCB baada ya kuzindua uuzaji wa hisa za Benki hiyo katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile baada ya kuzindua mpango wa Benki ya Walimu MCB - MCB kuanza kuuza hisa zake kwenye soko la hisa la Dar es Salaam Novemba 27, 2015. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akisalimiana na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade na Naibu wake, Lusekelo Mwaseba (wa pili kulia) baada ya kuwasili kwenye bandari ya Dar es Salaam kutaka maelezo kuhusu upotevu wa makontena 349 yenye kodi ya serikali ya thamani ya shilingi Bilioni 80, Novemba 27, 2015.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akimwonyesha orodha ya makontena 349 yenye kodi ya serikali ya thamani ya shilingi Bilioni 80 yaliyotoka kwenye bandari ya Dar es Salaam bila kulipiwa kodi, Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Rished Bade wakati alipotaka maelezo kuhusu upotevu  wa makontena hayo, bandarini jijini Dar es Salaam Novemba 27, 2015.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akimwonyesha orodha ya makontena 349 yenye kodi ya serikali ya thamani ya shilingi Bilioni 80 yaliyotoka kwenye bandari ya Dar es Salaam bila kulipiwa kodi, Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Rished Bade wakati alipotaka maelezo kuhusu upotevu  wa makontena hayo, bandarini jijini Dar es Salaam Novemba 27, 2015.



Waziri Mkuu, Majliwa Kassim Majaliwa akizungumza kwenye bandari ya Dar es Salaam alikokwenda Novemba 27, 2015 kutaka maelezo ya makontena 349 yaliyotoka kwenye bandari ya Dar es Salaam bila kulipiwa kodi na kuikosesha serikali shilingi Bilioni 80.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam, Awadh Massawe na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade baada ya kuzungumza na uongozi wa TRA na Bandari ya Dar es Salaam Novemba 27, 2015. Mheshimiwa Majaliwa alikwenda kwenye bandari ya Dar kutaka maelezo juu ya makontena 349 yaliyotoka kwenye bandari ya Dar es Salaam bila kulipiwa kodi ya serikali ya shilingi Bilioni 80. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA KAZI MAAFISA

WATANO WA TRA
*Ni kwa upotevu wa makontena 349, yana thamani ya sh. Bilioni 80/-

WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maafisa watano na watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Akizungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari pamoja na viongozi wa TRA katika ziara ya kushtukiza leo mchana (Ijumaa, Novemba 27, 2015), Waziri Mkuu amewataka Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Rished Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Lusekelo Mwaseba wahahakikishe wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na kwamba fedha hizo zinapatikana na zinarudi Serikalini.

Akitangaza uamuzi huo baada ya kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, Waziri Mkuu aliwataja maafisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Bw. Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Bw. Habibu Mponezya.

“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Waziri Mkuu.

Maafisa wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa kitengo cha TEHAMA, Bw. Haruni Mpande, Bw. Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani), na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Bw. Eliachi Mrema. “Hawa wanasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia wawe mikononi mwa polisi,” alisema.

Pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani. Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw. Robert Nyoni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho, kuhakikisha kuwa anapeleka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) haraka iwezekanavyo ili wakakague mifumo ya taarifa na kubaini jinsi ambavyo wizi huo unafanyika.

“Ninataka uchunguzi uanze kufanyika mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs. Nataka hayo makontena yatafutwe hadi yajulikane yako wapi, na fedha hiyo ihakikishwe inarudi serikalini,” alisema.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Bw. Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya DSM, Suleiman Kova, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Bw. Awadh Massawe na viongozi mbalimbali kutoka TRA na TPA.

Mapema akijibu maswali ya Waziri Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Bade alikiri kwamba kuna upotevu wa makontena ambao huwa unafanyika kati ya bandarini na ICDs na hasa ICD ya Ubungo. Akitoa ufafanuzi, alisema kwamba walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia za wizi. “Hata hivyo, tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka na kufikia 327. Tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na TAKUKURU. Mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa faini sh. bilioni 12.6/- na ameshalipa sh. bilioni 2.4/-,” alifafanua.

Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana majina ya watumishi wanaohusika na wizi huo, Bw. Bade akakiri kwamba anayo lakini siyo kwa wakati huo labda ayapate kutoka kwa wasaidizi wake. Ndipo Waziri Mkuu akamuonyesha orodha ya makontena 349 yenye taarifa zote hadi namba za magari yaliyobeba mizigo hiyo na Bw. Bade akakiri kwamba orodha hiyo ni ya kweli.

“Kwa utaratibu huo hatuwezi kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini”. Ndipo akaanza kutaja majina ya maafisa hao waliosimamishwa kazi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!