Watu zaidi wameendelea kutoroka mji wa Bujumbura nchini Burundi baada ya kuongezeka kwa mapigano.
Jumatano, watu wanne waliuawa katika mitaa miwili ya mji huo mkuu. Maafisa wa serikali wanasema wawili waliuawa kwenye ufyatulianaji wa risasi kati ya makundi ya watu wenye silaha na maafisa wa polisi usiku.
Mtu wa tatu aliuawa na watu wenye silaha, ambao polisi wamesema walikuwa waasi. Bado haijabainika ni nini kilichomuua mtu wa nne.
Mauaji yamekuwa yakitokea nchini Burundi tangu Aprili baada ya kuanza kwa maandamano ya kupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Rais huyo ameahidi kuwasaka na kuwaadhibu wanaosababisha mauaji hayo.
Mitaa ya Mutakura na Cibitoke ilifahamika sana kwa maandamano ya kupinga hatua ya Bw Nkurunziza kuwania urais tena.
Aliapishwa mwezi Julai kwa muhula wa tatu, ambao wapinzani wake wanasema ni kinyume na katiba
Tangu wakati huo, visa vimekuwa vikiripotiwa vya mauaji ya wafuasi na wapinzani wa serikali.
Rais huyo amewapa watu wenye silaya makataa ya hadi Jumamosi kuzisalimisha la sivyo maafisa wa usalama watatumia kila njia kusitisha mapigano hayo.
Mwandishi wa BBC mjini Bujumbura Prime Ndikumagenge anasema wengi wa wanaotoroka makwao walionekana wamebeba godoro na nyungu za kupikia wakiondoka.
Baadhi wanasema wanahofia yatakayojiri baada ya makataa hayo ya rais kupita Jumamosi.
No comments:
Post a Comment