KAULI na dhamira ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma ya kuwasaka wanaume waliotelekeza familia na kuwaburuza mahakamani, haina budi kuungwa mkono na kisha kuigwa katika maeneo mengine ya nchi.
Kamanda David Misime anasema wana kesi nyingi ambazo zinatokana na wanaume kutelekeza familia kwa kisingizio cha kwenda kutafuta kazi. Hii ni tabia ambayo haiwezi kuvumiliwa katika jamii kwani mbali ya mwanamume kuwa kichwa cha familia, ni wajibu wake kuhakikisha familia yake inaishi kwa amani yeye akiwa mlinzi mkuu.
Haiingii akilini kwamba mwanamume anaenda kutafuta kazi mbali na familia yake huku akijua ameiacha haina mbadala wa kuilinda na kuihudumia kiuchumi. Tunapenda kusisitiza kwamba dhamira ya Kamanda Misime isambae kwa wakuu wengine wa Polisi wa mikoa kwani hili ni tatizo la kitaifa ambalo sasa limefikia hatua inayohitaji matumizi ya sheria ili kulidhibiti.
Wanaume wengi wamekuwa na visingizio lukuki alimradi wakwepe majukumu yao likiwemo la kutunza familia. Watoto wengi waliozaliwa na wanaume wanaokwepa majukumu ya ulezi wamekosa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kukosa kwenda shule, matibabu, kula chakula bora, kuvaa na haki zao nyingine nyingi ambapo majukumu mengi mara nyingi huchukuliwa na akinamama.
Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, ni vyema wenye mamlaka wengine, mbali na makamanda, wayatumie kuthibiti vitendo hivi lakini pia waangalie namna ya kuwarudisha wanaume waliokimbia majukumu ya familia zao.
Tunachukua fursa hii pia kumuasa kila mwanamume aliyejaaliwa kuzaa mtoto kujua kwamba analo jukumu la kulea mwanawe au wanawe, ije mvua lije jua, na si kumwachia jukumu hilo mama wa mtoto peke yake.
Tunalipongeza Jeshi la Polisi nchini kuandaa utaratibu wa kuweka madawati ya kijinsia ambayo kwa kiasi kikubwa yamewezesha akinamama kupata mahali pa kukimbilia pindi wanapopatwa na unyanyasaji kutoka kwa watu wenye mtazamo wa mfumo dume ambao kwao hakuna haki wala usawa wa kijinsia.
Pamoja na jitihada za Serikali za kuhakikisha inapambana vilivyo kukomesha unyanyasaji wa kijinsia, yapo maeneo ambayo yamekuwa hayakubali kubadilika na kwenda na hali halisi.
Bado kuna ukeketaji kwa watoto wa kike, wanaume kupiga wake zao, watoto wenye umri mdogo kufanyishwa kazi za suluba, mambo ambayo yanahitaji nguvu ya ushirikiano wa jamii nzima.
Ndio maana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa akasema jukumu la kufichua wanyanyasaji wa kijinsia wakiwemo wanaokimbia majukumu ya ulezi wa familia lisiachwe kwa Jeshi la Polisi tu bali jamii nzima haina budi kufichua kila aina ya unyanyasaji wa kijinsia ambao uko ndani ya jamii husika.
Kinachohitajika katika kudhibiti vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia ni taarifa sahihi kutoka kwa wanajamii kwenda kwa vyombo husika. Na hii inawezekana kwani tayari vyombo vya kuwezesha waliofanyiwa ukatili vipo kuanzia kwenye ofisi za Serikali za Mitaa, madawati yaliyotengwa katika vituo vya Polisi na Mahakama.
No comments:
Post a Comment