Moshi. Watu watatu wanaodaiwa kuwa ni majambazi wameiba mkate wa Sh2,500 baada ya kufyatua risasi mbili hewani kwa bastola.
Tukio hilo lilitokea juzi saa tatu usiku katika Mtaa wa Bonite wakati vijana hao waliokuwa na pikipiki, walipompora mwanamke mmoja mfuko wakidhani kuna fedha.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Vicent Asenga alisema jana kuwa washukiwa hao wa ujambazi inaonekana walipewa taarifa zisizo sahihi kuwa mwanamke huyo alikuwa amebeba mfuko wenye fedha.
“Yule dada alipofika getini, tena nyumbani kwake ghafla walitokea vijana watatu na kufyatua risasi mbili hewani wakimtaka awape ule mfuko.
“Akawarushia wakaondoka na kutokomea kusikojulikana,” alisema na kuongeza kwa mujibu wa mwanamke huyo mfuko huo ulikuwa na mkate mmoja.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema watu hao walimpiga risasi ya mguu dereva wa bodaboda aliyekuwa amebeba mwanamke huyo hadi kwake, huku akisema anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.
Katika tukio hilo, Diwani mteule wa Kata ya Shirimatunda, Francis Shio na wenzake wawili walipinduka na gari baada ya kufyatuliwa risasi wakati wakiwafukuza watuhumiwa hao wa ujambazi.
“Tukiwa tunajadiliana ghafla zikatokea pikipiki mbili, ya mbele ndiyo ilikuwa na taa ya nyuma haikuwashwa. Diwani mteule akaamuru tuwasimamishe, lakini ile ya mbele ilifanikiwa kupita,” alisema Asenga.
Alisema diwani pamoja na watu wengine waliamua kuifukuza pikipiki iliyofanikiwa kupita na walipoikaribia, aliyekuwa amepakiwa nyuma alifyatua mlipuko ambao uliwachanganya.
“Ile gari ya diwani mteule ikayumba na kupinduka mara tatu, lakini ikasimama, pikipiki za watuhumiwa hao zikapinduka na wao kuumia,” alisema.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa washukiwa hao wa ujambazi wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC chini ya ulinzi wa polisi, huku mmoja akiwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kutokana na majeraha ya ajali.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani kuzungumzia tuhuma hizo hakupatikana.
Asenga aliendelea kudai kuwa jana asubuhi walipofika eneo la tukio na polisi walikuta ganda moja la risasi linalofafana na yale yaliyookotwa siku ya tukio usiku.
Diwani mteule, Shio alikiri kutokea kwa tukio hilo, akisema alipata majeraha kidogo ila suala hilo tayari linashughulikiwa na polisi.
“Hili tukio ni zito kwa sababu linahusisha matumizi ya silaha za moto (bastola) ni lazima tulichukulie kwa uzito unaostahili. Polisi wanaendelea na uchunguzi na sisi tunaendelea kukusanya taarifa,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti, diwani mteule na baadhi ya wananchi walikutana ili kuangalia namna ya kutokomeza matukio ya uhalifu
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment