BAADA ya wabunge kuthibitisha jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (55) aliyeteuliwa na Rais John Magufuli jana, wabunge wameelezea kufurahishwa na uteuzi huo na kusema anastahili kwa kuwa hana kashfa za kimaadili.
Naibu Waziri huyo katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, anashika wadhifa huo katika Serikali ya Awamu ya Tano huku uteuzi wake ukiwa siri kubwa na wabunge walikiri usiri mkubwa ulitawala, na hawakubaini au kubashiri kuteuliwa kwake.
Wakizungumzia uteuzi huo, baadhi ya wabunge walisema uteuzi wa Majaliwa ni wa haki na anastahili wadhifa huo kwa sababu ya utendaji kazi wake aliouonesha wakati wa uongozi wake ndani ya serikali ya awamu iliyopita.
“Tulimtaka mtu asiye na makandokando, asiye na makundi na kweli rais katuletea mtu anayestahili, kwani uongozi wake huku awali ulionekana,” alisema Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jaffo (CCM).
Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), alisema amefurahi kwa uteuzi huo kwani Waziri Majaliwa ni mchapakazi, mpole, asiye na makundi, na kiongozi mfuatiliaji ambaye amefanya naye kazi.
No comments:
Post a Comment