Sunday 1 November 2015

UFAULU WA DARASA LA SABA WAONGEZEKA



Baraza la Mitihani Tanzania, limetangaza matokeo ya Darasa la Saba huku ufaulu kwa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani ukiongezeka kwa asilimia 10.85.



Akitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini, Dk. Charles Msonde, alisema jumla ya wahitimu 518,034 kati ya 763,602 waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Alisema ufaulu huo ni sawa na asilimia 67.84 kutoka asilimia 56.99 wa mwaka jana, hivyo umepanda kwa asilimia 10.85. 

Hata hivyo, Dk. Msonde alisema watahiniwa 11,667 sawa na asilimia 1.50 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo utoro na ugonjwa.

Dk. Msonde alisema jumla ya wanafunzi 775, 273 waliosajiliwa kufanya mtihani wasichana walikuwa 413,966 sawa na asilimia 53.40 na wavulana 361,307 sawa na asilimia 46.60.

Hata hivyo, alisema waliofanya mtihani huo walikuwa 763,606 sawa na asilimia 98.0 ya waliosajiliwa, huku kati yao wasichana wakiwa ni 408,900 sawa na asilimia 98.78 wakati wavulana wakiwa ni 354,706 sawa na asilimia 98.17.

Alisema wasichana waliofaulu ni 264,130 ambao ni sawa na asilimia 64.60 huku wavulana wakiwa 253,904 sawa na asilimia 71.58.

Dk. Msonde alisema kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, 683 walikuwa ni wenye uono hafifu na 75 wasioona.

Aidha, alisema takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 4.61 na 17.22 ikilinganishwa na mwaka 2014.

Alisema watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili kwa asilimia 77.20 na somo walilofaulu kwa kiwango cha chini zaidi ni Kiingereza lenye ufaulu wa asilimia 48.56.

Dk. Msonde alisema watahiniwa walioingia katika kumi bora kitaifa  ni wale ambao wamepata alama nyingi zaidi kuliko wenzao kwenye masomo matano.

Aliwaja kuwa ni Jaffar Matange kutoka Shule ya Hazina jijini Dar es Salaam, Karim Seyn (Hazina), Teddy Range (Mugini mkoani Mwanza), Paulina Gervas (Mugini, Mwanza) na Nyegoro Amos (Mugini).

Wengine ni Juster Mgarula (Mugini, Mwanza), Janeth George (Mugini, Mwanza), Ibrahim Kondo (Rocken Hill, Shinyanga), Godbless Hhayuma (Twibhoki, Mara) na David Mtelemwa (Twibhoki, Mara).

Aliwataja wasichana ambao wameingia kumi bora kitaifa (kwenye mabano ni shule aliyotoka) Teddy Range (Mugini, Mwanza), Paulina Gervas (Mugini, Mwanza), Nyegoro Amos (Mugini, Mwanza), Juster Mgarula (Mugini, Mwanza), Janeth George (Mugini, Mwanza), na Rachel Masanja (Mugini, Mwanza).

Wengine ni Perine Kandisso  (Mugini, Mwanza), Irene Michael  (Twibhoki, Mara), Pappiness Chacha (Twibhoki, Mara) na Philimina Philimatus (Little Flower, Mara).

Wavulana walioingia kumi bora kitaifa ni ni Jaffar Matange (Hazina, DSM), Karim Seyn (Hazina, DSM), Ibrahim Kondo (Rocken Hill, Shinyanga), Godbless Hhayuma (Twibhoki, Mara) na David  Mtalemwa (Twibhoki, Mara).

Wengine ni Ismail Sigera (Hazina, DSM), Rajabu Mohammed (Hazina, DSM), Henry Chamatata (Rocken Hill, Mara), Kelvin Joseph (Little Flower, Mara) na Gemystone Thompson (Rocken Hill, Mara).

Aidha, Dk. Msonde alizitaja shule ambazo zimeingia kumi bora kwa ufaulu kuwa ni, Waja Springs (Geita), Enyamai (Mara), Twibhoki (Mara), Mugina (Mwanza), Rocken Hill (Shinyanga), Karume (Kagera), Alliance (Mwanza), Little Flower (Mara), Palikas (Shinyanga) na Mtakatifu Caroli (Mwanza).

Kadhalika alizitaja shule 10 ambazo hazikufanya vizuri kuwa ni shule ya msingi ya Mwashigini (Shinyanga), Mabambasa (Simiyu), Mwangu (Lindi), Mohedagew (Arusha), Kwale (Pwani), Njoro (Arusha), Gomhungile (Dodoma), Makole (Tanga), Kitengu (Morogoro) na Koloni  (Morogoro).

Alisema mikoa kumi ambayo inaongoza kwa ufaulu kitaifa ni Katavi, Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Geita, Kagera, Tanga, Njombe na Iringa.

Dk. Msonde alizitaja halmashauri kumi zinazoongoza kwa ufaulu kitaifa kuwa ni Mpanda Mji (Katavi), Arusha (M) (Arusha), Biharamulo (Kagera), Hai (Kilimanjaro), Ukerewe (Mwanza), Korogwe (Tanga),  Arusha (Arusha), Moshi (M) (Kilimanjaro),  Kinondoni (Dar es Salaam) na Ilemela (Mwanza).

Aidha, alisema Baraza la Mitihani limezuia kutoa matokeo ya wahitimu wanne ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo.

Alisema watahiniwa hao wamepewa fursa ya kurudia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2016.

“Ninawapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015, na kuwataka kuendeleza juhudi hizo katika ngazi ya sekondari,” alisema Dk Msonde.

Pia, Baraza la Mitihani limetoa wito kwa walimu na wanafunzi kuendeleza juhudi katika ufundishaji na kwa upande wa maafisa elimu wa mkoa na wilaya wadhibiti ubora wa elimu kufanya ufuatiliaji katika kuhakikisha ufundishaji na kujifunza shuleni unatiliwa mkazo ili kuongeza kiwango cha ufaulu.

Kadhalika Dk. Msonde aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa na ushirikiano na walimu ili kuboresha mazingira ya ufundishaji pamoja na kuwafuatilia watoto wao ili kuwawezesha kupata elimu inayotakiwa.

Wakati huo huo, Baraza hilo limesema jumla ya watahiniwa 448,358 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne kesho.

Alisema maandalizi kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa mtihani, vitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote Tanzania Bara na visiwani.

Aidha, Dk Msonde alisema baraza halina taarifa zozote za kuathiri kufanyika kwa mtihani huko visiwani Zanzibar na kuwa mtihani utafanyika kwa amani na utulivu, kwani kupo salama.

“Baraza linapenda kutoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na wilaya kufuata taratibu zote za mitihani zinazotakiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu,” alisema
Aliwataka wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali.

“Wasimamizi wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya taifa,” alisema.

Alisema Baraza la Mitihani halitasita kuchukua hatua kwa yoyote aliyejihusisha  na udanganyifu wa mitihani ikiwa ni pamoja na kuwafutia matokeo  kwa watahiniwa wote watakaobainika.

Aidha, aliwaomba wadau kutoa taarifa katika vyombo vya habari watakapobaini mtu ama kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa mitihani ili hatua zichukuliwe.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!