Matokeo Ya Ajabu; Algeria Vs Germany 1982, Na Algeria Vs Tanzania 2015!
Ndugu zangu,
Nimeshuhudia mechi ya usiku wa leo tulipokuwa tukiangamizwa na Algeria. Mpaka naamua kuinuka kitini tulikuwa tumeshapigwa saba bila. Ukweli tulizidiwa, na kuna wakati nilimuuliza aliyekaa karibu yangu kama Mbwana Samatta yumo uwanjani au Kocha Mkwassa ameshamuweka benchi. Hapana, nilijibiwa kuwa yumo uwanjani!
Naam, hata nyota wetu Mbwana Samatta leo alikuwa wa kumtafuta kwa kuvaa miwani ya macho. Hakuonekana.
Nilichokiona kikubwa; Tanzania tunahitaji kuruhusu uraia pacha ili nasi tuweze kuwaleta vijana wetu wa Kitanzania wanaocheza ughaibuni na waliochukua uraia wa nchi hizo. Maana, kwa soka ya sasa, ni vigumu kwenda Kombe la Dunia kwa kuwa kikosini na akina Samatta wawili na waliobaki ni wa kutoka Ligi ya nyumbani.
Na hakika matokeo ya leo yalikuwa ni ya ajabu pia. Sikufikiri kwa soka ile tuliyocheza Dar tungekwenda Algeria kucheza ' mediocre football' na kutoka na matokeo yale. Nilitarajia tufanye miujiza, maana soka inayo ya kwake. Na Algeria wenzetu wamewahi kufanya miujiza dhidi ya taifa kubwa kisoka la Ujerumani.
Ndio, itakumbukwa Algeria iliwahi kufanya miujiza katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1982. Ni pale ilipowafunga Ujerumani kwa mabao 2-1 kwenye mechi ya ufunguzi katika kundi lao. Walikuwa wachezaji nyota wa Algeria kama vile Assad na Madjer walionyesha kandanda safi na la kuvutia.
Katika pambano hilo kipa wa Ujerumani Schumacher alitoka uwanjani akiwa ameinamisha kichwa. Maana alitamka kabla ya mechi, kuwa kama Algeria watawafunga Wajerumani, basi atafanya operesheni ya kubadili sura yake!
Pamoja na Algeria kuwafunga Wajerumani, njama zilifanyika kwa Ujerumani na Austria katika kundi lao. Kwa namna moja au nyingine matokeo yalipangwa ili Algeria isipate nafasi ya kusonga mbele. Ujerumani iliibuka mshindi kwa bao 1-0 matokeo ambayo yalizifanya Ujerumani na Austria kusonga mbele kwa pamoja kutoka kwenye kundi lao.
Jambo hilo lilidhihirishwa mara tu baada ya Ujerumani kupachika bao lao. Mpira ukaonekana 'kufa'. Wachezaji wa timu zote mbili walionekana kucheza wakisubiri kipenga cha mwamuzi cha kumaliza mchezo. Hakika hii yaweza kabisa kusemwa ni moja ya kashfa zilizopata kutokea katika historia ya fainali za Kombe la Dunia.
Kikabaki kimya hata baada ya matokeo hayo ya kushangaza. Hayakuandikwa mengi kwenye kurasa za michezo za magazetini. Kwenye moja ya magazeti ya Austria walitenga ukurasa mzima bila kuandika habari za mechi hiyo. Walichofanya ni kuandika orodha ya wachezaji waliocheza pambano hilo kwa pande zote mbili.
Kwa mchezo ule uliokuwa na matokeo ya ajabu na kutatanisha baina ya Ujerumani na Austria , Chama Cha Soka cha Algeria kiliitaka FIFA izitoe Ujerumani na Austria katika ushiriki wao wa mashindano hayo. Jambo hilo halikufanyika.
Maggid,
No comments:
Post a Comment