Thursday, 26 November 2015
Serikali yafuta Mikutano ya Viongozi wa Umma, Sasa kufanywa kwa Mifumo ya Tehama
Serikali imesema haitagharamia uendeshaji wa vikao kwa watendaji wake kama kukodi ukumbi, usafiri na muda unaotumika nje ya maeneo yao ya kazi badala yake watumie teknolojia ya habari na mawasiliano ya TEHAMA. Hatua hiyo ina lengo la kupunguza matumizi ya serikali. Pia miundombinu hiyo itaratibiwa na serikali. Hayo yamesemwa na mkuu wa kitengo cha TEHAMA nchini, Florence Temba.
SERIKALI ya Awamu ya Tano imeazimia kufanya mikutano yake yote kwa kutumia Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kupunguza gharama na kuokoa fedha ambazo zilikuwa zikitumika katika shughuli hizo. Miongoni mwa sababu za kusitisha mfumo uliokuwa ukitumika awali ni pamoja na muda wanaotumia viongozi kwenda kwenye mikutano hiyo na kuacha Ofisi zao zikiwa hazina watendaji. Taarifa iliyotolewa jana, Novemba 25, 2015 Jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Florence Temba, kwa vyombo vya habari, imefafanua kwamba Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya safari, posho na hata muda mwingi na wafanyakazi kuwa nje ya vituo vyao vya kazi. Kwa mujibu wa Temba, mikoa yote nchini hadi sasa inavyo vifaa na mitambo ya Tehama kwa ajili ya kufanyia mikutano kwa njia hiyo isipokuwa mikoa mipya ya Geita, Simiyu na Njombe ambayo itatumia mikoa iliyopo jirani kufanyia mikutano yao. “Serikali haitaingia gharama mbalimbali ili kuendesha vikao kazi na watendaji wake, gharama ambazo Serikali imekuwa ikiingia ni pamoja na kukodi kumbi, kusafiri na muda unaotumika kwa maofisa wake kuwa nje ya vituo vya kazi” alikaririwa na FikraPevu. Amefafanua kwamba hatua hiyo ni matokeo ya Serikali kuanza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kuendesha vikao kazi vinavyohusu watendaji wake katika utekelezaji wa majukumu yao. Walengwa wakuu wa vikao kazi ni pamoja na Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Maofisa Utumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Akizungumza na FikraPevu, Mkurugenzi wa Mifumo ya Tehama, Priscas Kiwango, amesema kuwa kila mkoa lazima uwe na wataalamu wa Tehama ili kufanikisha mikutano yote ya Serikali na kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Uanzishaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini utaboresha na kuongeza ufanisi wenye tija ambao utapunguza gharama za utendaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kupitia utaratibu huu wa vikao kazi ambavyo vitaendeshwa kwa kutumia mfumo wa mawasiliano ya video ambapo kikao kimoja kitaunganisha kwa pamoja washiriki kutoka mikoa nane ambapo mada huwasilishwa na kutoa fursa ya kuwasiliana moja kwa moja kwa maswali na ufafanuzi. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Florence Temba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya TEHAMA katika kupunguza gharama za uendeshaji vikao kazi.
Mfumo wa mawasiliano ya video ni teknolojia inayowezesha mawasilano kutoka vituo mbalimbali kuwasiliana kwa njia ya sauti na picha kwa njia ya kielekroniki bila kuhitaji kukutana eneo moja.
"Teknolojia hii ya kutumia mfumo wa mawasiliano ya video itapunguza gharama mbalimbali za uendeshaji vikao Serikalini ambazo ni pamoja na kukodi kumbi za mikutano, usafiri na muda ambao hutumika nje ya vituo vya kazi" alisema Temba.
Aidha, Bw. Temba alisema kuwa utaratibu wa vikao ni rasmi kama ilivyo mikutano mingine ya kazi ambao ni salama kwa kuwa miundo mbinu yake inaratibiwa na Serikali.
Bw. Temba aliendelea kusema kuwa mwongozo wa mawasiliano kwa njia ya video umetolewa na unapatikana katika tovuti ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, "Mwangozo huu unahusu wajibu wa Wizara, idara, Wakala za Serikali na Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika kuboresha mawasiliano kwa njia ya video" aliongeza Bw.Temba.
Pia mwongozo huo unaainisha mazingira na vifaa ya kuendesha mawasiliano kwa njia ya video kuzingatia sifa na viwango vya chini na kuhakiki mfumo huo kabla ya matumizi.
Mfumo huo ulianzishwa na Serikali mwaka 2013/2014 katika mikoa ya Kilimanjaro, Kagera, Morogoro na Iringa kati ya utumishi na mamlaka za Serikali za mitaa ambapo kwa sasa mawasiliano hayo yanapatikana nchi nzima isipokuwa mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Katavi na Njombe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment