Tuesday, 17 November 2015

SERIKALI KUWABEBA WALIOFELI KIDATO CHA PILI NA NNE.


Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde 

Kwa ufupi

Utaratibu huo mpya uliotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, unafuta rasmi utaratibu wa awali ambao Serikali iliwataka wanafunzi wanaofeli mtihani huo kukariri darasa wakishindwa kufikisha wastani wa alama 30.


Dar es Salaam
Wakati wanafunzi wa kidato cha pili wakianza mitihani jana, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza kwamba wanafunzi watakaofeli mtihani huo hawatorudia darasa, bali wataandaliwa utaratibu maalumu wa masomo ya jioni ili kuwawezesha kitaaluma.

Utaratibu huo mpya uliotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, unafuta rasmi utaratibu wa awali ambao Serikali iliwataka wanafunzi wanaofeli mtihani huo kukariri darasa wakishindwa kufikisha wastani wa alama 30.
Dk Msonde alisema utaratibu huo mpya utawahusu pia wanafunzi wa darasa la nne ambao nao hawatalazimika kurudia darasa, bali watakuwa na muda wao wa ziada wa kusoma.
"Lengo la kuweka utaratibu huo ni kusimamia kwa karibu viwango vya ufundishaji. Wanafunzi wanaofanya vibaya wanahitaji ukaribu wa walimu na siyo kuwarudisha darasa tu," alisema.
Akizungumzia mtihani huo ulioanza jana, alisema watahiniwa 397,250 walisajiliwa nchi nzima, wakiwamo wanafunzi 67 wasioona na 224 wenye uoni hafifu.
Mwaka 2008, Serikali ilifuta makali ya mtihani wa kidato cha pili, hali iliyotoa fursa kwa wanafunzi wengi hata wasio na uwezo kuingia kidato cha tatu na hatimaye kupata nafasi ya kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne.
Baada ya matokeo mabaya yaliyotokana na uamuzi huo na pia kelele za wadau wa elimu na jamii kwa jumla, hatimaye mwaka 2012, Serikali iliurudisha mtihani huo na kutangaza kuwa wanaofeli watakariri darasa, utaratibu ambao sasa umefutwa.

Maoni ya wadau

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo nchini (Tamongsco), Benjamin Nkonya alisema kuzuia wanafunzi wasikariri darasa ni kuwaondolea ari na hamasa ya kusoma kwa bidii, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya elimu nchini.
Alisema ili mwanafunzi asome kwa bidii lazima ajue kwamba akifeli ataondolewa kwenye mfumo rasmi wa elimu. Aliongeza kuwa Taifa litakuwa na watu wengi waliokwenda shule lakini hawana uwezo kwenye soko la ajira.
"Huu ni msumari wa mwisho kwenye jeneza la elimu. Serikali ikizuia wanafunzi kurudia darasa, elimu itaporomoka kama ilivyokuwa miaka 40 iliyopita na shule za binafsi zitakuwa kwa kasi," alisema na kuongeza: "Hiyo elimu wanayosema ya bure itakuwa hamna kitu. Mwanafunzi akija kwenye shule zetu za binafsi na kushindwa kufikisha wastani tunamfukuza. Tunataka watu ambao wanasoma na kujua kwamba wakicheza wataondoka."
Meneja Mipango na Utafiti wa shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventure alisema masomo ya jioni siyo suluhisho la kuzuia kiwango cha wanafunzi kufeli.
Alisema Serikali inapaswa kujua sababu inayochangia wanafunzi kufeli na kisha kutengeneza njia mbadala za kuwasaidia.
"Tatizo ni kwamba Serikali siku zote inaogopa neno kufeli, ndiyo maana wanafanya mabadiliko mengi ambayo hayana tija ili tu kuondoa neno kufeli. Remedial classes (masomo ya ziada) siyo njia mbadala ya kuzuia kufeli kwa wanafunzi," alisema Boniventure.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!