Waliokuwa wagombea wa ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha Wananchi (Cuf), wameibuka wakiwa na hati za kuchaguliwa wakidai kuwa wao ndiyo washindi halali wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuwatambua na kuapishwa ili waanze kutekeleza majukumu yao.
Aidha, wajumbe hao wapatao 27 wamesema hawako tayari kurudia uchaguzi kwa mara ya pili na kuitaka Zec kutengua tamko lake la kufuta matokeo ya uchaguzi huo na kukamilisha taratibu za majumuisho ya kuhesabu kura za urais za Zanzibar ili Rais mpya za Zanzibar atangazwe na kuitisha Baraza la Wawakilishi jipya.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Aboubakar Khamis Bakari, alisema Zec inapaswa kutengua tamko la mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha la kufuta matokeo ya uchaguzi kwani ni kinyume na katiba na sheria.
Alisema wajumbe hao walichaguliwa wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kuthibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yao kwa mujibu wa kifungu cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka1984.
Alisema endapo Zec itakaidi kuwatambua kuwa ndiyo washindi halali wa uchaguzi huo na kutomwapisha kiongozi wao Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wa Zanzibar, watakutana na kufanya vikao vya kichama kisha kutoa tamko na mwelekeo na msimamo wa Cuf.
Bakari alidai uchaguzi wa Zanzibar ulikwenda vizuri na ulitoa nafasi kwa wananchi wa Zanzibar walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kuchagua viongozi waliowataka. Alisema baada ya upigaji kura kumalizika, kazi ya kuhesabu kura nayo ilikwenda vizuri na fomu za matokeo ya uchaguzi kwa kila kituo cha kupigia kura kusainiwa.
Alisema baada ya hatua hiyo ilifuata ya majumuisho katika ngazi ya majimbo ambayo nayo ilikwenda vizuri na kukamilishwa bila ya kuwapo malalamiko yoyote kutoka chama chochote kilichokuwa kinashiriki uchaguzi huo.
Bakari alisema kutokana na kukamilika kwa hatua zote na kufuata masharti ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka 1984, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Unguja na Pemba wakawatangaza washindi pamoja na kuwapa taarifa za maandishi.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar, uchaguzi wa wawakilishi na madiwani ulikuwa umeshakamilika na washindi kutangazwa kwa majimbo na wadi zote za Unguja na Pemba na kwamba wagombea walioshinda kutoka vyama vyote walipewa hati za uthibitisho rasmi wa kuchaguliwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment