RAIS John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Ufaransa, François Hollande, kutokana na tukio la kigaidi la mashambulizi kadhaa yaliyotokea nchini humo mwishoni mwa wiki jijini Paris.
Katika ujumbe aliotuma kwa Rais Hollande, Dk Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya wananchi wa Ufaransa na mashabiki wa mpira jijini Paris.
“Katika kipindi hiki kigumu, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa niaba yangu mwenyewe, naomba nikupe pole wewe na familia za walioathirika na shambulio hili pamoja na wananchi wa Ufaransa,” alisema Dk Magufuli.
Alisema Serikali ya Tanzania inaungana na mataifa mengine kulaani vikali wale wote waliohusika na mashambulizi hayo yaliyosababisha vifo vya raia wengi wasio na hatia. Alisema katika kipindi hicho kigumu, Tanzania inaungana na Ufaransa katika kuombeleza vifo vya watu wote waliopoteza maisha katika mashambulizi hayo ya kigaidi.
“Kupitia kwako Rais Hollande, naomba unifikishie salamu zangu za dhati kwa ndugu na familia zilizopoteza wapendwa wao katika mashambulio haya. Lakini pia napenda kuwatakia wale wote waliojeruhiwa kupona haraka,” alisema rais.
Katika hatua nyingine, mjini Dodoma, Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Tanzania imelaani tukio la shambulizi la kigaidi lililotokea Paris na kusababisha mauaji wa watu 160 huku takriban 200 wakijeruhiwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mratibu wa Jumuiya ya Ahmaddiya Muslim Jamaat Tanzania, Tahir Mahmood Chaudhry Amir, Jumuiya hiyo inatoa rambirambi za dhati kwa Taifa la Ufaransa, kwa watu na serikali kutokana na tukio hilo baya la kigaidi.
“Huruma zetu na maombi yetu yako juu ya wahanga wote wa tukio hili na wale wote waliobaki na huzuni au walioathiriwa na tukio hili kwa njia moja au nyingine na ni matumaini yetu kwamba wahusika wote wa tendo hili ovu watakamatwa na mkono wa sheria,” ilisema jumuiya hiyo.
No comments:
Post a Comment