Wananchi, wasomi, viongozi wa dini na wanasiasa wamepokea kwa hisia tofauti hatua ya Rais John Magufuli, kufuta sherehe za kumbumbu ya uhuru na kuifanya kuwa siku ya usafi kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu, huku wengi wakipongeza.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofaut jana, walisema hatua hiyo imeonyesha jinsi Rais Magufuli alivyo na uwezo wa kufanya maamuzi kulingana na umuhimu wa jambo katika wakati husika kwa manufaa ya wengi.
Mkazi wa Tabata, wilayani Ilala, Joel Mrutu, alisema hatua hiyo kiutendaji ni jambo zuri kwani ameonyesha kukerwa na matumizi mabaya ya fedha za serikali.
“Hatua aliyoichukua kiutendaji ni jambo zuri kwani Rais ameonyesha anakerwa na matumizi mabaya ya fedha serikali,” alisema.
Alisema, Dk. Magufuli akiendelea na msimamo huo inawezekana ikapatikana Tanzania mpya wanayoitaka wananchi.
Mkazi wa Temeke, Ali Jabir, alisema Rais Magufuli ameonyesha mfano wa kuigwa kwa kujali maisha ya watu kwa kusisitiza fedha za umma kutumika kwenye masuala ya msingi.
Kwa upande wake, Bwana Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Mathias Kapiza, alisema kitendo alichokifanya Dk. Magufuli kitasaidia kuwaamsha kuhusu madhara na ukumbwa wa ugonjwa wa kipindupindu ulioyakumba maeneo mengi nchini na kushirikiana na serikali kupambana nao.
“Mabadiliko ya kweli yameanza kuonekana kwa kufuta siku ya Uhuru na kuifanya kuwa siku ya usafi, hii itawasaidia wananchi kutambua jukumu la kupambana na maradhi na kuchukua hatua kuutokomeza,” alisema Dk. Kapiza.
Naye Mhadhiri wa Kikuu cha Tumaini, tawi la Dar es Salaam (Tudarco), Danford Kitwana, alisema kinachoendelea kufanywa na Rais Magufuli ni namna ya kubana matumizi mabaya ya fedha za serikali na kupongeza siku hiyo kutumika kufanya usafi.
Alimtaka kuangalia sherehe nyingine ambazo hazina umuhimu wa kutumia fedha nyingi ili fedha hizo zielekezwa kwenye mambo yenye tija kitaifa. Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Kanda ya Dar es Salaam, Yasin Mleke, alisema anaunga mkono hatua hiyo kwani hali ya uchumi ni mbaya huku serikali ikiwa ina mambo mengi ya kufanya ikiwamo malipo ya mishahara ya watumishi, madeni ya wafanyakazi, uboreshaji wa huduma za afya na elimu.
Naye Msemaji wa Jumuiya za Taasisi za Kiislamu Tanzania ambaye pia ni Katibu wa jumuiya hiyo, Sheikh Rajab Katimba, alisema hadhani kama ni sahihi kufuta sherehe hizo kwa kigezo cha kuifanya siku ya usafi ndiyo nchi nzima itakuwa safi.
Alisema kufanya hivyo kunapoteza historia ya nchi na kutaka suala la usafi kuwekewa mikatati na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Aliyekuwa Mgombea ubunge Jimbo la Segerea, Julius Mtatiro, alisema yeye haamini katika matamko badala yake vitu vinavyofanyika kisheria na siyo mtu kufanya kwa ajili ya utawala wake.
Alisema sherehe za Uhuru zinatakiwa kuwapo kila mkoa pasipokuwapo mambo mengi yatayogharimu fedha, ikiwamo kurusha ndege za kivita hewani, magwaride na maonyesho ya makomando na posho.
Mtatiro alisema huenda hatua hiyo imefanyika kutokana Hazina kuishiwa fedha, akidai kuwa nchi nyingi za Afrika vyama tawala hutumia fedha za serikali kwenye uchaguzi.
Ijumaa iliyopita Rais Magufuli alizuia matumizi y Sh. milioni 265 zilizokusudiwa kutumiwa na Ofisi ya Bunge kwa ajili ya hafla ya wabunge kupongezana baada ya uzinduzi rasmi wa Bunge la 11, mjini Dodoma.
Aliamuru zitumike Sh. milioni 15 tu na fedha nyingine zilizobaki zitumiwe kununua vitanda kwa wagonjwa wanaolala chini katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Aidha, Jumatatu iliyopita aliagiza kufutwa kwa sherehe za Uhuru na kutaka siku hiyo itumike kufanya usafi nchi nzima.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment