WAKWERE ni miongoni mwa makabila nchini, hupatikana wilaya ya Bagamoyo mkoani wa Pwani na katika maeneo ya Morogoro na Ngerengere.
Kabila hilo kwa miaka ya hivi karibuni limepata umaarufu mkubwa kutokana na kutoa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. Kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu watu wa kabila hilo hasa kutokana na kupenda kuishi kwenye nyumba za asili. Miaka ya nyuma kulikuwa na uvumi kuwa iwapo utajenga nyumba nzuri basi unaweza kutengwa na jamii jambo ambalo lilikuwa likionekana kama ni kweli kwa kuwa wananchi wengi wa kabila hilo waliendelea kuishi kwenye nyumba za asili.
Theophil Kandamsile maarufu kama mzee Kidibo mkazi wa kijiji cha Malivundo kata ya Pera, Chalinze anasema kabila hilo ni miongoni mwa makabili yanayotunza asili na utamaduni wa tangu kale. Anasema Wakwere wanapenda kutunza asili na kutekeleza yale ambayo wanaona yanawafaa wao bila kuiga yanayofanywa na makabila mengine. Anasema si kweli kwamba Wakwere ni watu wasio na maendeleo, kuna wasomi wengi na viongozi wengi wanaotoka katika kabila hilo.
“Ni watu wenye maendeleo na wanaopenda maendeleo angalia sasa hata vijiji vingi vinabadilika, watoto wengi wanakwenda shule, tuache dhana kuwa sisi si watu wa maendeleo, kama ni umasikini upo kwa kila mkoa wasitunyooshee tu sisi vidole,” anasema.
Mzee Kandamsile anasema, amezaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Malivundo na tangu wakati huo hajawahi kuona Wakwere wakisahau au wakiitupa asili yao. “Asili ya Wakwere ni Malivundo, sababu zake zilikuwa walikuja watu kutoka Uzigua miaka mingi iliyopita kabla hata ya ukoloni, walikuwa ni mtu na dada yake kutokana na eneo lile waliokuwemo kusukwa na msitu mnene waliamua kupanda juu ya mti kwa kuogopa wanyama wakali,” anasema.
Anasema, watu hao waliendelea kuishi juu ya mti kwa kuogopa wanyama wakali na baadaye alifika Msagara na kubaini kuna watu juu ya mti. “Naye akachagua mti wake akapanda juu na waliendelea kuishi lakini mwisho wa siku yule Msagara akaanza urafiki wa siri na dada wa Mzigua“ anasema mzee Kandamsile. Baadaye yule dada akapata ujauzito na alipoulizwa na kaka yake akasema mimba ile ni ya Msagara ambaye hata naye baadaye alikiri kuwa mimba ile ni yake.
“Akamwambia sasa huyo ndio anakuwa mkeo na akaamua kujenga nyumba, ndio maisha ya kujenga familia yalipoanza na kizazi hicho kikakua na wakatafuta maeneo kwa ajili ya kuishi ambapo pia walikuwa wakifanya shughuli za kilimo,” anasema. Mzee Kandamsile anasema, wageni bado walikuwa wakifika katika eneo hilo na walipokuta kuna watu nao walianzisha makazi. Mzee huyo anasema asili ya jina Wakwere linatokana na kukwea juu ya miti.
“Kwere imetokana na kwea” anasema na kubainisha kwamba shughuli kubwa za Wakwere ni kilimo na ufugaji. Utamaduni Ngoma za utamaduni wa kabila hilo ni pamoja na Digililo ikiwa na maana ya kuvaa njuga miguuni. Kuna utamaduni wa Bugi , wanavaa njuga miguuni wakati wa kucheza ngoma lakini kunakuwa na mashairi wakati wanaimba kwenye matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na baada ya kusikia mtu ameiba au amekamatwa ugoni na mume au mke wa mtu, wanatunga shairi la kucheza hiyo ngoma.
Chakula
Anasema chakula cha asili ni mtama na mboga zikiwemo kunde, choroko, njegere, mbaazi na fiwi. Mahindi ni chakula cha pili baada ya mtama.
Kuoleana/unyago
Zamani baba mzazi wa mwanaume akikuta msichana ambaye ataridhika naye kwa tabia na maadili anakwenda kuongea na baba wa msichana. Wazazi hao wanakubaliana kisha mvulana anakwenda kumuona msichana na kufuatia na kifunga uchumba. Umri wa msichana ulikuwa unaweza kuwa hata miaka 10.
“Kulikuwa na nguo nyekundu ukinunua unampelekea mchumba, akivunja ungo wakati wa kutoka ili achezwe ngoma ndiyo mahari inatolewa na mwanaume anakabidhiwa mke wake,” anasema mzee Kandamsile. Anasema katika hilo wasichana walikuwa wakichumbiwa wakiwa wadogo lakini hawakuruhusiwa kwenda kwa wanaume mpaka watakapovunja ungo na kufuata taratibu zote za kuwekwa ndani na kupewa mafunzo maalumu ikiwemo jinsi ya kuishi na mume.
Pia msichana anapokwenda kwa mume alikuwa akielekezwa kama hataona hedhi yake amwambie mama mkwe wake ambaye baadaye atakwenda kumuambia mama mzazi wa msichana. “Wasichana walikuwa wakichumbiwa wakiwa na miaka 10 na wakati huo mahari ya mwanamke ilikuwa ni fedha au ng’ombe,” anasema. Anasema jambo hilo lilisaidia kukuza maadili na heshima kwa wazazi kwa kuwa watoto walitakiwa kufuata taratibu zote ili waweze kuoana bila vikawazo vyovyote.
Anasema hadi sasa utamaduni huo upo katika baadhi ya maeneo. “Sasa msichana akivunja ungo anawekwa ndani hadi miaka miwili akisubiri ngoma ya kutoka na hufundishwa kuhusu maisha ya ndoa na usafi juu ya mwili wake”, anasema mzee Kandamsile. Anabainisha kuwa elimu ya unyago imekuwa ikimfanya msichana kujiandaa na maisha ya kuwa mama na kuweza kutunza familia. Kukaa ndani kwa msichana kunategemea na uwezo wa msichana kwani mwali anapokaa ndani siku ya kutoka lazima kuwe na pombe, ngoma na zawadi.
Anasema, kuna wanaokaa sana kwa kusubiri vitu hivyo na wengine wakikaa muda mfupi kutokana na kutimiza vitu hivyo mapema.
“Lengo la unyango tangu zamani ni kuonya, kuelimisha na kutoa burudani kutokana na sherehe zake kuambatana na vyakula na pombe mbalimbali hasa zile za kienyeji". Kwa mujibu wa mzee huyo, miaka ya nyuma utamaduni huo ulisaidia kwa kuwa ulitoa elimu ya jinsi ya kuishi na mume jambo lililowezesha ndoa nyingi kudumu kwa miaka mingi. Utamaduni huo upo pia kwenye makabila mengine na umekuwa ni njia kubwa ya kuwapa elimu vijana wa kike kufahamu mambo mbalimbali.
Tiba za asili “Kuna mkoba wa jadi unaitwa Kinyamkera, uko kama kikapu, unatiwa madawa na kila kabila wanao, baadaye akazaliwa shetani ni wa manyanga ndio maana kuna ngoma za mashetani” anasema mzee Kandamsile. Mzee huyo anasema hata yeye ni mganga, amerithi mikoba ya uganga miaka mingi na amekuwa akitoa tiba. “Kuna ngoma za mashetani madogori na ng’anga na inachezwa wakati mtu anaonekana ana shetani ambapo dalili zake ni kutetemeka kama anasikia baridi kali kama anakufa,” anasema.
Mzee Kandamsile anasema, mtu kama huyo akipigiwa ngoma hiyo anacheza na watu huenda kutafuta dawa na anapokuwa akicheza mapepo yote aliyokuwanayo yanatoka. Aidha ngoma ya dogoli inapopigwa mganga na mteja wake wote hucheza na ngoma hiyo mpaka sasa imekuwa ikitumika kupunga mashetani. Mzee huyo anasema mashetani mengi hutokea porini kwenye mibuyu kwani ngoma hiyo inapopigwa mashetani hutoka na kurudi kwenye mibuyu.
Tiba za jadi
Mitishamba imekuwa ikitumika kwenye tiba na imekuwa ikichimbwa porini na waganga wamekuwa wakiifahamu miti yenye tiba kulingana na walivyofundishwa. Anasema uganga mwingi ni wa kurithi ama kwa baba au kwa mama. “Vijana wa sasa wapende au wasipende lazima wajifunze tiba hizo kwani zina manufaa makubwa tangu kale na kuna magonjwa ambayo yamekuwa yakishindikana hata hospitali lakini yanatibika kwa tiba za asili,” anasema mzee Kandamsile.
Matambiko
Anasema matambiko yamekuwa yakifanyika kwa kukoroga pombe na kuchinja wanyama. Faida za kutambika ni asili ambayo imerithiwa kutoka kizazi na kizazi na hufanyika kila baada ya mwaka moja na husaidia kutibu magonjwa na kutatua matatizo ya kimaisha. “Asili ya Wakwere haiwezi kufa kutokana na utandawazi wengi wanapenda kuenzi mila,” anasema.
1 comment:
hiyo makala uliipata wapi ?
Post a Comment