Saturday, 14 November 2015

MAGUFULI AIFUMUA UPYA IKULU, APUNGUZA OFISI NA WATENDAJI


Rais John Magufuli amezifumua na kuziunda upya baadhi ya ofisi za Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam pamoja na kuwaondoa baadhi ya watumishi ambao hawana ulazima katika mfumo wa utumishi wa Ikulu.



Taarifa za uhakika zilizotufikia kutoka ndani ya Ikulu zimeeleza kuwa Rais Magufuli alianza kufanya ukaguzi wa ofisi moja baada ya nyingine zilizo Ikulu huku akitaka maelezo ya kina kuhusu shughuli zake na aina ya watendaji waliopo.

Mmoja wa maofisa waandamizi wa Ikulu aliyezungumza  kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa, alisema katika ukaguzi huo, Rais Magufuli aliamuru kufungwa mara moja kwa baadhi ya ofisi alizobaini kuwa hazina tija na kwamba zina watumishi ambao ni mizigo.

Ofisa huyo alizitaja baadhi ya ofisi zilizofungwa kuwa ni pamoja na iliyokuwa ikishughulikia chakula cha rais na ile iliyokuwa ikijihusisha na kupokea wageni binafsi wa rais.

“Rais Magufuli alipoingia tu Ikulu alifanya ziara ya kukagua ofisi zote zilizopo Ikulu, alitaka kujua utendaji kazi wa ofisi hizo lakini alipofika kwenye kitengo maalumu cha lishe ya rais alisema haoni umuhimu wa kuwepo kwa ofisi hiyo kwa sababu suala la lishe yake siku zote linasimamiwa na mkewe Janeth. Akaamuru ifungwe na watumishi wake warejeshwe walikotoka.

"Ofisi nyingine aliyoamuru ifungwe ni kupokea wageni binafsi wa rais. Alisema haoni tija ya kuwepo kwa ofisi hiyo kwa sababu mgeni anatakiwa kufika Ikulu baada ya kutoa taarifa, nayo aliamuru ifungwe,”alisema ofisa huyo.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa aliyekuwa mkuu wa kitengo cha lishe Ikulu amerudishwa katika ajira yake ya awali Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, huku watumishi wengine wakipelekwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Alipotafutwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kupitia simu ya kiganjani kuzungumzia hatua hiyo, simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ulionyesha kupokelewa kwenye simu yake lakini haukujibiwa.

Alipoulizwa Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga kuhusu kuwepo kwa hatua hizo alisema ni kweli Rais Magufuli alipoingia ofisini alianza kuipanga upya Ikulu kulingana na matakwa yake wakati wa utawala wake.

Premi ambaye alizungumza kupitia simu yake ya kiganjani alisema wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya nne kulikuwa na ofisi maalumu ya lishe Ikulu ambayo hata hivyo ilikuwa haihusiani na uandaaji wa chakula cha rais.

Alisema ofisi hiyo ilikuwa mahususi kwa ajili ya ushauri kuhusu programu ya kimataifa ya urutubishaji wa vyakula kwa lengo la kupunguza tatizo la udumavu wa watoto.

“Ofisi hiyo ilikuwa inaongozwa na mtaalamu wa masuala ya lishe hata hivyo kabla ya Rais Kikwete kumaliza muda wake mtaalamu huyo aliacha kazi yake na kwenda kugombea ubunge huko kwao sasa ukiniambia amerudishwa Wizara ya Afya sitakuwa na jibu la uhakika kwa sababu sifahamu,” alisema Premi.

Alipoulizwa kuhusu kufungwa kwa ofisi ya wageni binafsi wa Rais, Premi alisema ilikuwa na kazi ya kupokea malalamiko ya wananchi lakini Rais Magufuli ameamua kuiondoa kwa sababu ameweka utaratibu wa malalamiko ya wananchi kupokewa kuanzia ngazi za chini.

“Kama unavyojua Rais amekuja na dira yake ya ‘hapa kazi tu,’ hivyo anataka watendaji wa ngazi zote wawajibike kwa ufanisi. Wakati wa utawala wa Rais Kikwete alifungua dawati hilo kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya wananchi, watu walitoka mikoa ya mbali kuleta kero zao hapa Ikulu lakini Rais Magufuli ameamua malalamiko ya wananchi yasikilizwe kuanzia ngazi za chini.

“Rais Magufuli anataka watendaji wote wa Serikali wawajibike kupokea kero za wananchi na kuzifanyia kazi. Zipo ofisi za madiwani, wabunge, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa ambao wote wanalo jukumu la kuwasikiliza wananchi na kuwatatulia kero zao,” alisema Premi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!