WAGENI wa kimataifa zaidi ya 50 wanatarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli zitakazofanyika keshokutwa jijini Dar es Salaam.
Ofisa Uhusiano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rosemary Malale, alisema orodha hiyo ya wageni walioalikwa, inajumuisha mashirika ya kimataifa, mashirika ya kikanda, wakuu nchi na mabalozi.
Rais mteule Dk Magufuli alitangazwa kuwa mshindi, baada ya kushinda katika uchaguzi, uliofanyika wiki iliyopita kwa kupata asilimia 58.46 ya kura zote zilizopigwa. Ofisa huyo alisema wizara pia imetuma mialiko kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inayoundwa na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Nchi nyingine zilizoalikwa ni za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU).
Aidha, sherehe hizo pia zinatarajiwa kuhudhuriwa na Muungano wa nchi za Amerika (ISSR), Misri, Ghana, Sweden, Uingereza, Marekani, Ufaransa, Japan, China na Umoja wa Mataifa.
Maandalizi ya sherehe hizo zitakazofanyika katika uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam yanaendelea, yakihusisha wanajeshi ambao pamoja na mazoezi mbalimbali, pia zilionekana ndege za kivita angani.
Dk Magufuli aliwaangusha wagombea wengine saba, akiwemo mpinzani wake mkuu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Wakati rais huyo mteule akisubiri kuapishwa, kumekuwa na ushauri tofauti kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, wakitaka atekeleze ahadi zake na pia kujenga umoja wa Watanzania.
Akizungumza jana na mwandishi wa habari hizi, mmoja wa waliogombea urais, MacMillan Lyimo (TLP), alisema alimtaka Magufuli akiingia madarakani, ahakikishe anajenga umoja miongoni mwa Watanzania kwa kuepuka kujenga chama chake pekee.
No comments:
Post a Comment