Eneo la Uyole katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ni maarufu sana kihistoria, kwa ajili ya kilimo na biashara za ngazi ya kati.
Kwa zama zilizopita, kabla ya kuwa jiji la Mbeya, palijulikana kwa hadhi ya ‘pembezoni mwa mji,’ ila kwa sasa ni vigumu kuipa hadhi hiyo, kwa maana mji wa Mbeya umekua na aina ya shughuli na makazi nayo, yamekua maradufu.
Aidha, katika maendeleo ya mipngo miji ya Jiji la Mbeya, hivi sasa kunatarajiwa, baadhi ya miundombinu ya jiji, imeshaanza kuhamishiwa jirani na mahali hapo, ikiwemo sehemu iliyoandaliwa kuwa stendi kuu ya mkoa.
Pamoja na uhalisia huo, miinuko ya Uyole inafahamika vyema kwa uzalishaji wa bidhaa kama viazi mviringo inayolisha sehemu nyingi za nchi, mahindi, maharage, pareto nk
Kwa maana hiyo, jamii ya wakazi wa Uyole ni wakulima na wajasiriamali wadogo, ambao biashara zao kwa sehemu kubwa, wanategemea wateja wa makutano ya barabara kuu ya Dar es Salaam na Zambia na njia panda iendayo Tukuyu- Kyela hadi mpakani na Malawi.
Sarah John ambaye ni mkulima wa mbogamboga, pamoja na matunda katika bustani yake eneo la Uyole, nje kidogo na mkoa wa Mbeya, anasema alirithi kilimo hicho kutoka kwa wazazi wake.
Anasema, yuko mahali hapo tangu zama za miaka ya 1970, wazazi wake walikuwa wakulima wa mashamba makubwa yenye ekeri zaidi ya 10, walilima na kupanda mahindi shambani mwao kwa kutumia jembe la mkono.
Sarah ambaye ni mama wa watoto watatu, anasema kabla ya kuwa mkulima, alikuwa na hali duni ya maisha, ikilinganishwa na ilivyo sasa.
Anasema, ameweza kumudu kusomesha watoto wake kwa kuwalipia ada, pamoja na kuwahudumia ndugu zake kutokana na bustani yake.
Pamoja na kutaja changamoto ya upatikanaji wa soko la kuuzia bidhaa zao, bado anataja kuwa kilimo kimemkomboa maisha yake, kwa kuweza kujipatia kipato na kujikimu.
"Kilimo hiki kimenisaidia sana pia ninapata mboga za kutumia mi mwenyewe kila siku nyumbani, kwa kweli mimi simulizi kichwa kufikiri fedha ya mboga ya kila siku, ninaingia tu bustanini mwangu na kuchagua nile mboga ya majani ya aina gani," anasema Sarah.
Katika bustani ya Sarah ambayo inavutia kwa rangi ya kijani, kuna mboga za aina mbalimbali kama vile Mchicha, Chainizi, Sukuma Wiki, Spinachi, Nyanya, Ndizi, Kabeji, Karoti, Biringanya, bamia na nyinginezo.
Tathmini ya jumla ya mkoa wa Mbeya, unajulikana kwa umahiri wake katika kilimo na uzalishaji mazao mbalimbali.
Kwa mfano, Kyela ni wilaya inayojulikana sana kwa uzalishaji wa mpunga tena wa kiwango bora kitaifa.
Uzalishaji kama huo wa mpunga, unafanyika katika sehemu nyinginezo kama vile wilaya ya Mbarali ambako nako kuna uzalishaji mkubwa katika bonde la Rujewa.
Pia, Wilaya ya Rungwe ambako ni ardhi ya miinuko kama ilivyo Ileje, yenyewe ina umaarufu wa kulima mahindi nayo yanazalishwa kwa kiwango kikubwa na kulisha sehemu nyinginezo.
Uzalishaji huo wa mahindi kwa kiwango kikubwa, ndio unafanyika hata katika wilaya ya Mbozi.
Mtazamo mdogo wa uzalishaji kwa kiwango hiko, ndio kuna wakati uliipandisha hadhi mkoa wa Mbeya, ukawa hesabu ya mikoa iliyopewa hadhi ya kupandishwa daraja na kuitwa ‘The big four’ au mikoa minne vigogo wa kuzalisha chakula.
Hadhi kama hiyo ya uzalishaji nafaka kimataifa, hivi sasa imeifikia pia mkoa wa Morogoro, ambao una hadhi kubwa katika uwezi wa kuzalisha nafaka ya mahindi kwa kiwango kikubwa.
Maana ya hiyo ni kwamba, mikoa iliyokuwa inayongoza kitaifa katika uzalishaji wa chakula na hasa ambayo ni:Mbeya, Rukwa, Iringa na Ruvuma.
MAPATO
Sarah anasema, baada ya kuandaa bustani kwa ajili ya kupanda mbegu za mboga mboga, hununua mbegu hizo kwa gharama nafuu ikiwamo baadaye kununua dawa za kuulia wadudu.
Anasema kwa mwezi mara baada ya kuuza mboga, anakuwa ameweza kupata mapato ya fedha zisizopungua Sh. 600,000, fedha hiyo ni faida aliyoipata kwa mwezi baada ya kutoa gharama za mbegu, dawa na mbolea.
Sarah anasema, kutokana na kilimo hicho, ameweza kujenga nyumba ambayo anaishi yeye pamoja na watoto wake.
Anasema, pamoja na kilimo kumsaidia yeye binafsi, bado ameweza kuwapatia ajira wanawake wanne ambao ni wajane na kuweza kuwalipa Sh. 50,000 kwa mwezi.
Changamoto azipatazo Sarah katika kilimo, inajumuisha, ugumu wa kupata mikopo kutoka katika taasisi za kifedha, kwani taasisi nyingi zinapenda kukopesha wafanyabiashara, kuliko wakulima.
Pili, ni ugumu wa kupata masoko ya mazao yao yaanayoharibika kwa haraka, baada ya kuvuna. Hayo ni mazao kama vile nyanya, karoti, ndizi, machungwa na maembe.
Mama Thabitha Bugali, ni Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Kikristo, mkoani Mbeya. Anasema kuwa, wanachama walio katika umoja huo wameweza kujikwamua kiuchumi kutokana na kujishughulisha na shughuli za kilimo.
"Tunapokutana kila baada ya mwezi huwa tunajadili mafanikio ya kila mwanachama pamoja na kupeana mbinu za kukabiliana na changamoto, ambazo zinatukwamisha," anasema Mama Bugali.
Inasemekana, wanawake wengi nchini takriban asilimia 85, wanajishughulisha zaidi na kilimo kuliko hata wanaume.
Wanawake hao, ambao wapo katika sekta ya kilimo, hususan mazao ya chakula, yanayotegemea kilimo, wanachukua nafasi ya kuwa tegemeo katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kutoka ngazi ya familia hadi Taifa.
Licha ya wanawake hao kulima mazao ya chakula, wapo wengi nchini wanaowajibika katika kuvuna, kuhifadhi na kuuza mazao pamoja na kutayarisha nafaka kwa chakula.
Takwimu zinaonyesha kuwa, inapotokea ziada au umuhimu wa kuuza chakula kwa ajili ya kupata mahitaji ya nyumbani vile kama chumvi, sabuni, sukani, wanawake hunufaika nayo kwa kuuza mazao yao.
Hata katika marejeo ya kihistoria, inamrejea mwanamke kuwa ndiye aliyeanzisha kilimo, katika zama za kuishi mapangoni.
Ni jambo lililobuniwa na mfumo wa mgawanyo wa kazi wakati huo, kati ya wanaume na wanawake.
Enzi hizo, wanaume walikuwa wanakwenda kuwinda huku wanawake wakibakia nyumbani wakiwaangalia watoto, pamoja na kuandaa chakula.
Walifanya hivyo kwa kuokota mizizi ya matunda, iliyo karibu na mapango yao.
Baadaye, wanawake hao walitengenezea vijiti na kuanza kulima mazao ya chakula na ndio ukawa mwanzo wa wanadamu kuwa na makao ya kudumu, katika jamii nyingi za mwanzo.
Wanawake walio wengi walibaki nyumbani, wakilima na kulea watoto, hivyo tokea enzi hizo wanawake wamekuwa wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula.
KUMKOMBOA MWANAMKE
Kumkomboa mwanamke mkulima, ni pale viwanda vya usindikaji mazao ya chakula na matunda vitakapoanzishwa karibu na maeneo yanakolimwa mazao hayo wanayoyazalisha shambani.
Iwapo utafikiwa hatua hiyo ya viwanda kujengwa nchi nzima, vinakuwa mkombozi kwa mwanamke.
Hayo yote yanarejea juu ya anachokifanya mwanamama Sarah huo Uyole, Mbeya ni ishara kamaili kwamba ‘kilimo ni mkombozi wa familia na Taifa.’
Pia, inampa ishara kuwa mwanamke akiwa ndiye msaada mkubwa wa kuhakikisha chakula kinakuwapo nyumbani, ili kuleta amani na utulivu wa maisha katika jamii.
No comments:
Post a Comment