Friday, 27 November 2015

KAMPENI YA ABIRIA PAZA SAUTI YAZINDULIWA RASMI JIJINI DAR ES SALAAM LEO‏

Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Abel Swai (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo, kuhusu kampeni ya Abiria Paza Sauti iliyozinduliwa Dar es Salaam leo asubuhi.



Na Dotto Mwaibale

MKUU wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna wa Polisi, Mohamed Mpinga amesema kila mwananchi anawajibu kuzuia ajali za barabarani badala ya kudhani kazi hiyo ni ya polisi pekee.

Mpinga alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Abiria Paza Sauti iliyozinduliwa Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam leo asubuhi, ambao ulikwenda sanjari na mabalozi wa Usalama barabarani  (RSA) ambao walitoa elimu  kwa abiria kuhusu usalama barabarani.

"Abiria pazeni sauti pale mtakapoona dereva anaendesha gari lake ndivyo sivyo na kama mtapaza sauti itasaidia kupunguza ajali hapa nchini" alisema Kamanda Mpinga.

Mwakilishi  wa Mwenyekiti wa Usalama Barabarani ambaye ni Mratibu wa kampeni hiyo , Jackson Kalikuntima, alisema kampeni hiyo itaendelea nchini kote kwa njia ya kutoa elimu, haki na wajibu wa raia wanapokuwa safarini.

Alisema abiria wanaowajibu wa kuzuia ajali wakishirikiana na mabalozi watakao kuwa ndani ya mabasi kuhimiza abiria kupaza sauti.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Abel Swai alisema kumekuwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya madereva kukiuka sheria na kusababisha ajali kwa makusudi.

Alisema kampeni hiyo inalengo la kutoa elimu kwa abiria waweze kujiamini na kutoa taarifa pale wanapoona dereva anakwenda kinyume na sheria kwa kutumia namba za kutoa taarifa kwa polisi na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ambazo ni 0800110019 au 0800110020.

Swai alisema madereva wanapaswa kutii sheria bila shuruti na kuwa wana amini kila mmoja atakuwa makini na kuzingatia sheria ajali zitapungua kama sio kuisha kabisa.


No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!