Hata hivyo, hatari ipo. Ni kwa nini chakula kinafanya watu wawe wagonjwa, na tunaweza kufanya nini kupunguza hatari hiyo?
Jinsi Vyakula Vinavyosababisha Magonjwa
Jarida la Emerging Infectious Diseases linasema kwamba zaidi ya magonjwa 200 yanaweza kusababishwa na chakula. Hata hivyo, vijidudu vinavyosababisha magonjwa hayo yote si vingi sana. Dakt. Iain Swadling, afisa wa shirika la Huduma ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Chakula, anasema kwamba asilimia 90 hivi ya magonjwa yote yanayosababishwa na chakula, huenda yanasababishwa na jamii za vijidudu “zisizozidi 24.” Visababishi vya magonjwa kama vile virusi, bakteria, vimelea, sumu, na kadhalika, huingiaje katika chakula?
Dakt. Swadling anataja mambo matano ambayo kwa kawaida husababisha magonjwa: “Kula chakula kibichi chenye vijidudu; kula chakula kilichotayarishwa na watu wagonjwa au walioambukizwa viini; kutohifadhi vyakula vizuri na kutayarisha chakula saa kadhaa kabla ya kukila; kuchafua chakula safi kwa kukiweka pamoja na chakula chenye vijidudu wakati wa kukitayarisha; kutopika chakula vizuri au kutopasha moto vya kutosha chakula kilichopikwa kimbele.” Ingawa orodha hiyo inaweza kushtua, inaonyesha jambo zuri pia. Jambo hilo ni kwamba karibu magonjwa yote yanayosababishwa na chakula yanaweza kuzuiwa. Soma sanduku kwenye ukurasa wa 8 na 9 ili ujue kile unachoweza kufanya usiambukizwe ugonjwa unaosababishwa na chakula.
Kufanya Maamuzi Yanayofaa
Leo, watu fulani wanaoelewa kwamba vyakula vinaweza kusababisha magonjwa wameamua kununua, kutayarisha, na kula vyakula vilivyotolewa shambani karibuni. Endapo wewe unapendezwa na jambo hilo, nenda kwenye maduka na masoko yenye vyakula vilivyotolewa shambani karibuni na visivyotiwa dawa yoyote. Kitabu kimoja cha mwongozo kinaeleza: ‘Watu wengi wanawaendea wakulima moja kwa moja—ama sokoni au kwenye mashamba yao—ili wapate vyakula vilivyotolewa shambani karibuni, wajue jinsi vilivyokuzwa na mahali vinapokuzwa.’ Inafaa kufanya hivyo hasa unapotaka kununua nyama.
Hali kadhalika, afadhali ununue vyakula katika majira yake, kwa kuwa mara nyingi vyakula hivyo ndivyo vizuri zaidi. Hata hivyo, kumbuka kwamba ukifanya hivyo, utakosa matunda na mboga fulani wakati ambapo hazipatikani.
Je, unapaswa kula tu vyakula vilivyokuzwa bila kutumia dawa yoyote wala mbolea ya kikemikali? Wewe mwenyewe utaamua. Bila shaka wengi wanapenda vyakula vilivyokuzwa hivyo kwa sababu wanatilia shaka mbinu mpya za kukuza na kutengeneza vyakula. Lakini si wote wanaokubali kwamba vyakula vilivyokuzwa bila dawa za kuua wadudu na mbolea ya kemikali ni bora.
Hata iwe unapendelea vyakula gani, chunguza kwa uangalifu vyakula unavyonunua. Mtaalamu mmoja aliyenukuliwa katika gazeti la Die Zeit, alisema kwamba “watu huangalia bei tu wanaponunua vyakula.” Kufikiria bei ni jambo la maana, lakini chunguza pia maandishi yanayoonyesha vilivyomo. Inakadiriwa kwamba karibu nusu ya watu wa nchi za Magharibi hawachunguzi maandishi yanayoeleza ni virutubishi vipi vilivyomo katika vyakula wanavyonunua. Ni kweli kwamba katika nchi nyingine maandishi hayo hayaonyeshi habari nyingi. Lakini ukitaka vyakula vinavyojenga afya chunguza sana vyakula unavyonunua.
Hata uamuzi wako kuhusu vyakula uwe nini, bila shaka itakubidi kubadilika mara kwa mara kupatana na hali ya nchi unamoishi. Watu wengi leo hawana fedha za kutosha, wala wakati, wala uwezo wa kuhakikisha kwamba vyakula vyote wanavyokula ni vyenye kujenga afya kabisa.
Je, tunatia chumvi tunaposema hivyo? La, hivyo ndivyo ilivyo. Lakini, mambo yatabadilika karibuni.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Kile Unachoweza Kufanya
▪ Safisha. Nawa mikono kwa maji ya moto na sabuni kabla ya kuanza kutayarisha kila aina ya chakula. Nawa mikono baada ya kwenda chooni, na baada ya kushughulikia mtoto (iwe ni kumbadilisha nepi au kumpangusa makamasi), au kushika mnyama yeyote, hata mnyama-kipenzi. Osha vyombo, mbao za kukatia, na meza kwa maji ya moto na sabuni baada ya kutengeneza kila aina ya chakula—hasa baada ya kukata nyama, kuku, au samaki na vyakula vingine vinavyotoka baharini. Gazeti la Testlinapendekeza “kuosha matunda na mboga katika maji ya uvuguvugu” ili kuondoa wadudu na mabaki ya dawa ya kuua wadudu. Mara nyingi kutoa maganda na kuchemsha vyakula ni njia bora za kuvisafisha. Toa na utupe majani ya nje-nje ya kabichi na letusi (lettuce). Katika sehemu zenye maji machafu huenda ikawa muhimu kutia dawa ya kuua vijidudu, kama vile dawa ya kung’arisha, permanganate, au mvinyo wa siki, katika maji ya kuosha matunda au mboga zitakazoliwa zikiwa mbichi.
▪ Pika Vizuri. Karibu bakteria zote, virusi vyote, na vimelea vyote vitakufa ikiwa chakula kitapikwa kufikia nyuzi Selsiasi 70 (moto kabisa), na si lazima kupika kwa muda mrefu. Kuku anahitaji kupikwa hadi aive kabisa kufikia nyuzi Selsiasi 80. Chakula kinachopashwa moto chapasa kufikia nyuzi Selsiasi 75 au kuwa moto na kutoa mvuke. Usile kuku ambaye bado ni mwekundu au mayai yasiyopikwa vizuri. Samaki anapasa kupikwa hadi awe laini na kubadilika rangi.
▪ Usiweke Vyakula Pamoja. Usiweke kamwe nyama, kuku, au samaki mbichi pamoja na vyakula vingine unapofanya ununuzi, unapohifadhi vyakula hivyo, au unapovitayarisha. Usiache maji ya vyakula hivyo yatone wala kutiririka kwenye vyakula vingine. Usiweke kamwe chakula kilichopikwa kwenye chombo kilichokuwa na nyama, samaki, au kuku mbichi ila chombo hicho kiwe kimeoshwa vizuri kwa maji ya moto na sabuni.
▪ Hifadhi Vyakula Ifaavyo. Friji inaweza kuzuia bakteria zisiongezeke, lakini halijoto yake inapasa kuwa nyuzi Selsiasi 4 tu. Mashine ya barafu inapasa kuwa na nyuzi Selsiasi 17 chini ya kiwango cha kuganda. Weka vyakula vinavyoweza kuharibika kwenye friji kabla ya muda wa saa mbili kuisha. Ukiweka vyakula mezani mapema, vifunike ili kuzuia inzi.
▪ Ujihadhari Unapokula Kwenye Mikahawa. Inakadiriwa kwamba katika nchi fulani zilizoendelea, asilimia 60 hadi 80 ya watu waliopata magonjwa yanayosababishwa na chakula walikula vyakula vilivyopikwa mikahawani. Hakikisha kwamba mkahawa unamokula unafuata sheria za usafi zilizowekwa na serikali. Agiza nyama iliyopikwa vizuri. Unaponunua chakula mkahawani na kukileta nyumbani, kile kabla ya muda wa saa mbili kuisha. Endapo muda zaidi ungepita kabla hujala chakula hicho, kipashe moto vizuri kufikia nyuzi Selsiasi 75.
▪ Tupa Chakula Unachoshuku Kimeharibika. Afadhali utupe chakula ambacho unashuku kimeharibika. Si vizuri kutupa chakula kizuri, lakini matibabu ya ugonjwa uliosababishwa na chakula kilichoharibika yatakugharimu fedha nyingi hata zaidi.
No comments:
Post a Comment