Askofu wa Kanisa la FPCT Jimbo la Tabora Kusini, Mchungaji Isaya Ilumba akimkabidhi mwanafunzi Nassoro Ally kiti cha magurudumu.
Mwanafunzi Nassoro Ally (miaka 10), wa darasa la kwanza, Shule ya Msingi Chemchem akiwa na bibi yake Joha Mhanuka baada ya kukabidhiwa kiti chake.
Sabbas Prosper, mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mlimwa B mkoani Dodoma akiwa kwenye kiti alichopewa.
Said Maganga wa Shule ya Msingi Chemchem, Tabora akiwa kwenye kiti chake.
Jeremiah Deo Deus (miaka 15) mwenye ulemavu wa miguu na mikono baada ya kukabidhiwa kiti chake.
Mtoto mwenye ulemavu, Sabbas Prosper baada ya kukabidhiwa kiti cha kutembelea akiwa na maafisa kutoka mkoani Dodoma.
Mwanafunzi Nassoro Ally (miaka 10) wa darasa la kwanza, Shule ya Msingi Chemchem, akiwa na bibi yake, Joha Mhanuka ndani ya ofisi ya mwalimu mkuu akisubiri kukabidhiwa kiti cha magurudumu.
Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) kupitia mradi wa kuwasaidia watoto wenye ulemavu nchini kwa msaada wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Sweden, ERIKS Development wamekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia watoto wenye ulemavu ambapo hivi karibuni walifanya tukio la kuwapa baadhi ya watoto hao viti vya magurudumu ‘wheel chairs’.
Mratibu wa mpango huo, Lucas Mhenga amesema kuwa dhamira ya FPCT na ERIKS Development ni kuona watoto wenye ulemavu nao wanakuwa na maisha mzuri kama wengine kwa kuhakikisha wanawasaidia kadiri ya uwezo wao.
“Tumekuwa tukiguswa sana na changamoto zinazowapata watoto wenye ulemavu na hivi karibuni tumekabidhi viti vya magurudumu kwa watoto mbalimbali wenye ulemavu kutoka mikoa ya Tabora, Dodoma na Arusha ili nao waweze kwenda shule kusoma bila shida ya kusafiri,” alisema Mhenga na kuongeza:
“Tutaendelea kufanya hivyo lakini tunahitaji sapoti, sisi wenyewe hatuwezi kwa kuwa watoto hawa ni wengi na wana mahitaji mengi, kwa hiyo tukiungana pamoja tunaweza kuwafanya nao waishi kwa amani na furaha.”
Wakizungumzia msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chemchem iliyopo Tabora, Hafsa Salum Juma na Mjumbe wa kamati ya shule, Yusufu Juma Risasi ambao baadhi ya wanafunzi wao wamepata viti hivyo walilishukuru sana Kanisa la FPCT kwa msaada wao.
“Tunawashukuru sana FPCT na ERIKS Development kwa namna ambavyo wamejitoa kuwasaidia watoto hawa wenye ulemavu, kwa msaada wa viti hivi watoto hawa wataweza kwenda shuleni bila usumbufu kwao na wazazi wao.
“Hii iwe changamoto kwa watu wengine kuona wana jukumu la kuwasaidia watoto hawa ambao bila kusaidiwa hawawezi kuishi maisha ya furaha kama wengine,” alisema Mwalimu Hafsa.
Siku chache baada ya watoto hao kupatiwa vifaa hivyo, mwalimu huyo amesema mahudhurio yao yamekuwa mazuri na wanafunzi hao wanafurahia masomo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Wazazi wa watoto wanasemaje?
Kufuatia msaada wa viti hivyo vya magurudumu kwa watoto wenye ulemavu, wazazi wao wamesema, hawana cha kuwalipa FPCT na washirika wake kwani wamefarijika sana na wanaamini watoto wao watapata elimu katika mazingira rafiki.
Kufuatia msaada wa viti hivyo vya magurudumu kwa watoto wenye ulemavu, wazazi wao wamesema, hawana cha kuwalipa FPCT na washirika wake kwani wamefarijika sana na wanaamini watoto wao watapata elimu katika mazingira rafiki.
”Tulikuwa tukipata tabu sana kuwabeba watoto wetu kuwapeleka shuleni, kwenda na kurudi, hata walipokuwa shuleni walikuwa wakipata tabu sana lakini baada ya kupewa viti hivi, ile adha imeondoka. Tunawashukuru sana FPCT na ERIKS kwa misaada yao,” alisema Joha Mhanuka, bibi wa Nassoro Ally aliyepata msaada wa kiti.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Tabora, Robert Kampambe alisema kuwa anawashukuru sana FPCT na ERIKS kwa misaada yao kwani wameonyesha njia kwa wadau wengine kuwasaidia watoto hawa.
“Msaada wa FPCT na ERIKS kwa watoto hawa walemavu ni changamoto kwetu hivyo natoa wito kwa watu wengine ndani ya manispaa kuunga mkono jitihada hizi. Tukiwaachia wao tu itakuwa mzigo mkubwa,” alisema Kampambe.
No comments:
Post a Comment