Monday, 9 November 2015

DK: MAGUFULI: NINA DENI KUBWA KWA WATANZANIA


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema ana deni kubwa kwa Watanzania baada ya wananchi kuonyesha imani kwake, huku akiwaambia wapinzani kuwa uchaguzi umekwisha na yeye ndiye Rais.


Katika hotuba yake ya kushukuru ya takriban dakika 10 baada ya kuapishwa, Dk Magufuli alisema ana kazi kubwa ya kuendeleza Taifa baada ya wananchi kuonyesha imani kwake huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii kutekeleza ahadi alizotoa kwenye kampeni.
“Nina deni kubwa la kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania,” alisema Dk Magufuli mbele ya maelfu ya watu waliojitokeza kwenye Uwanja wa Uhuru kushuhudia tukio hilo la kihistoria la kumsimika Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.

“Ninatambua kwa dhati kwamba tuna jukumu kubwa la kuwafanyia kazi Watanzania. Tunawaomba wote katika dini mbalimbali tumtangulize Mungu na kutuombea ili tutekeleza tuliyo yaahidi.”
Katika hotuba hiyo, Dk Magufuli, aliyegombea urais kwa tiketi ya CCM, hakuvibeza vyama vya upinzani na badala yake akavitaka kushirikiana naye kuendeleza Taifa.
“Na kwa ndugu zangu wa vyama vya upinzani ambao kwa bahati nzuri wengi wako hapa. Tutafanya kazi kwa ajili ya kuliendeleza Taifa, uchaguzi umekwisha. Rais ni John Pombe Joseph Magufuli, hapa kazi tu,” alisema Rais Dk Magufuli huku akishangiliwa.
“Nchi yetu daima ni kubwa kuliko vyama vyetu, mapenzi yetu na matakwa yetu. Uchaguzi Mkuu umekwisha, sote tushikamane kama watu wa taifa moja kuijenga nchi na kusonga mbele. Ndiyo maana nimekuwa nikisema ‘hapa kazi tu’, lakini tutangulize amani na kumtanguliza Mungu.”
Pia alikuwa na ujumbe kwa wagombea walioshindana naye kuwania urais.
“Ninyi mlikuwa washindani wenzangu, siyo wapinzani wangu maana sote tulikuwa na lengo la kujenga nchi moja,’’ alisema Dk Magufuli.
“Ninawashukuru kwa changamoto mlizotupa. Nimejifunza mengi kutoka kwenu. Lakini nimejifunza mengi mema ambayo tutayafanyia kazi ili kujenga Tanzania bora. Nawashukuru pia wananchi kwa kunichagua.”
Alisema kutunukiwa kwake ni ushindi kwa Tanzania kwa kuwa yeye ndiye ameshinda.
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Chato, pia aliwapongeza wabunge wateule, akiwaahidi kushirikiana nao.
“Tumepokea dhamana hii kwa unyenyekevu mkubwa sana. Tunatambua wajibu na deni kubwa la kutekeleza ahadi tulizotoa kwa Watanzania. Tutafanya kazi kwa juhudi na maarifa yetu yote kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
“Ninataka niwahakikishie, nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote kwa kumtanguliza Mungu mbele ili yale tuliyoyaahidi tuyatimize bila kubagua vyama vyetu, dini zetu wala makabila yetu. Sasa ni kazi tu.”
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na marais wote wastaafu pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, isipokuwa Edward Lowassa, aliyeshika wadhifa huo kwa miaka miwili (2005-08), na Frederick Sumaye, ambaye alishika wadhifa huo kwa kipindi chote cha miaka kumi ya Serikali ya Awamu ya Tatu.
Wawili hao waliihama CCM mwezi Julai, Lowassa akijiunga na Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais, na Sumaye akijiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi bila ya kutaja chama.
Dk Magufuli aliwashukuru marais hao kwa kuchangia safari yake ya kuelekea Ikulu kwa vipindi tofauti na hatimaye kumpa nafasi ya kugombea urais.
Alimshukuru Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kwa kumuongoza na busara zake, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa kumuibua kwa kumpa unaibu Waziri wa Ujenzi akiwa na umri wa miaka 35, na Jakaya Kikwete kwa kumuamini zaidi na kumpa uwaziri ambao alisema anaamini ndiyo leo umempa urais.
“Mimi ni nani hata wanione na kunipa nafasi hii,” alisema Dk Magufuli ambaye muda mwingi wa hotuba yake alizungumza kwa unyenyekevu.
Aliwashukuru marais waliofika kushuhudia uapisho wake na kusema kuwa wana shughuli nyingi katika nchi zao, lakini wamemjali na kuja kwenye hafla yake.
Dk Magufuli aliamsha kicheko aliposema: “Ninawashukuru mawaziri wenzangu wastaafu tuliokuwa wote.”
Kwa upande mwingine, Dk Magufuli aliwashukuru Wazanzibari kwa uvumilivu wao hadi sasa na kusema kuwa watahakikisha wanalimaliza suala la Zanzibar.
Alirudia kusema kuwa kuchaguliwa kwake ni zaidi ya Watanzania na pamoja na hayo, aliwataka kufanya kazi ili Taifa lisonge mbele.
Hakuacha kuizungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC, na kusema kuwa pamoja na kasoro zilizojitokeza, wamefanya kazi kubwa sanjari na majeshi ya ulinzi na usalama na waandishi wa habari kuhakikisha Taifa linabaki salama.
“Ninakosa maneno ya kuwashukuru kila mmoja. Ninachosema, sasa tufanye kazi. Uchaguzi umekwisha na Rais ni John Joseph Pombe Magufuli.”

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!