Tuesday, 10 November 2015

DK MAGUFULI AVAMIA MUHIMBILI, ATIMUA MKURUGENZI NA BODI


Rais  Dk. John Magufuli, ameifuta Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kumuondoa aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi.

Dk. Magufuli alichukua uamuzi huo jana baada ya kufanya ziara ya ghafla hospitalini hapo na kukuta mazingira yasiyoridhisha.
Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Dk. Magufuli amemteua Profesa Lawrence Mseru, kukaimu nafasi hiyo na aliyekuwapo amepelekwa wizarani.
Balozi Sefue alithibitisha kwamba Dk. Magufuli alifanya ziara hiyo ya ghafla majira ya saa tisa mchana na hakuridhishwa na namna huduma zilivyokuwa zikitolewa hospitalini hapo.
Alisema Dk. Magufuli alikuta mashine za vipimo mbalimbali kama MRI na CT - Scan hazifanyi kazi na kuagiza kuwa ndani ya wiki moja ziwe zimetengenezwa.
“Rais  amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-Scan zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika hospitali binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko,” alisema Balozi  Sefue. 
Alisema Dk. Hussein Kidanto, ambaye alikuwa akikaimu, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.
Balozi Sefue alisema Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.
Alisema tayari Wizara ya Fedha imetoa Sh. bilioni tatu kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi alisema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote.
Balozi Sefue pia alitumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.
“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa umma wasiojali wananchi na mahitaji yao,” alisisitiza Balozi Sefue.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!