Monday, 30 November 2015

BOHARI KUU KUDHIBITI WIZI WA DAWA HOSPITALI


Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imeanza kuweka alama maalum kwenye vidonge 45 vya magonjwa ya aina mbalimbali  kudhibiti tatizo la wizi wa dawa nchini.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu, alisema vidonge hivyo vimewekewa alama ya GOT ambayo ni nembo ya serikali. Aidha, alisema tatizo la wizi wa dawa litadhibitiwa kutokana na  MSD kufanya kazi za uagizaji, uhifadhi  na usambazaji kwa kutumia mfumo wa mtandao wa E9. 
 
“Zamani ilikuwa tunaweka kwenye vifungashio vya ndani na maboksi alama ya MSD, lakini sasa hata kila kidonge kitawekwa alama ya GOT,” alisema.
 
Alizitaja baadhi ya dawa zilizowekewa alama hiyo kuwa ni Diclofenac, Amoxillin, Ciprofloxacin, Contrimoxale, Paracetamol na Magnesium.
 
Aidha, Bwanakunu alisema MSD itaanzisha huduma ya kutoa taarifa kwa njia ya simu pale wananchi watakapoona kuna wizi wa dawa za serikali na wataelimishwa namna ya kutoa taarifa pale wanapoona dawa za serikali mitaani.
 
“Dawa nyingi zinaibwa kwenye vituo ambavyo dawa zinapelekwa na sasa tutakuwa tunatumia mfumo wa kompyuta kubaini wizi wa dawa ambazo zimekuwa zikiibwa mkoa moja na kupelekwa mkoa mwingine,” alisema. 
Kuhusu deni la MSD kwa serikali, Bwanakunu alisema bohari hiyo inaidai fedha nyingi licha ya kuanza kulipwa, ambapo hadi sasa wanadai Sh. bilioni 53 ambalo ni deni lililohakikiwa na wamelipwa Sh. bilioni 14. 
 
Mkurugenzi huyo alisema bajeti ya dawa ikiongezwa na kufikia Sh. bilioni 250  kila mtu anayehitaji kupata dawa atapata huduma hiyo bila ya matatizo.
 
Akizungumzia uanzishwaji wa maduka ya dawa karibu na hospitali za rufaa na kanda, Bwanakunu alisema agizo lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli la uanzishaji wa maduka hayo limeanza kutekelezwa, ambapo bohari hiyo inatarajia kufungua kesho duka lake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Ufunguzi huo utaenda sambamba na duka jingine la Kanda ya Mbeya, huku kwa Kanda ya Kati litafunguliwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!