Tuesday, 24 November 2015

BENKI YA STANDARD CHARTERED YATEUA MKURUGENZI WA KWANZA MTANZANIA‏

Sanjay - 3
Sanjay Rughani (pichani) anakuwa Mtanzania wa kwanza kuiongoza benki ya Standard Chartered Tanzania akipokea uongozi wa benki hiyo kutoka kwa aliyekuwa mkurugenzi wake, Liz Lloyd, ambaye amerudi katika makao makuu ya benki hiyo, London, kuchukua nafasi ya Mshauri wa Kisheria wa benki hiyo.


Sanjay alijiunga na benki ya Standard Chartered Tanzania mwaka wa 1999 akiwa kama Meneja msaidizi wa kitengo cha Fedha. Baada ya miaka miwili Sanjay alipata cheo cha Meneja wa kitengo cha Fedha kwa Bara la Afrika, kazi ambayo aliifanya akiwa katika makao makuu ya benki hiyo, London. Alirudi nyumbani Tanzania mwaka wa 2002 na kupata cheo cha Mkuu wa Kitengo cha Fedha nchini Tanzania, kazi ambayo aliifanya hadi mwaka wa 2006.
Mwaka wa 2007, Sanjay alipata tena cheo kingine, wakati huu akihamishiwa Ghana, ambapo aliongoza Kitengo cha Fedha nchini humo huku pia akisimamia Afrika Magharibi, yaani Gambia, Cote d' Ivoire na Sierra Leone, kazi ambayo aliifanya hadi Mei, 2013.
Juni, 2013 Sanjay alipandishwa tena cheo na kuwa Mkuu wa Operesheni za Kifedha na Mratibu wa Huduma za Kifedha kwa Bara la Afrika akiongoza kitengo hicho ambacho ni sehemu ya Kitengo Kikuu cha Fedha katika nchi kumi na tano za Afrika, akilenga kuboresha huduma za kifedha za benki hiyo zilingane na huduma zake za kimataifa katika nchi zilizoendelea. Sanjay alifanya kazi hii hadi alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Benki hiyo hapa Tanzania hapo mwanzoni wa mwezi huu wa kumi na moja.
Lamin Manjang, Mkurugenzi wa benki ya Standard Chartered Kenya na Afrika Mashariki, amesema, “Nafurahi kumkaribisha tena Sanjay nyumbani Tanzania na kwenye timu yangu ya Afrika Mashariki kufutatia umahiri wake katika kazi mbalimbali ambazo amezifanya katika benki yetu. Pia nafurahi kuwa sasa benki yetu nchini Tanzania ina Mkurugenzi wake wa kwanza wa Kitanzania. Hii inaonyesha ubora wa wafanyakazi wetu nchini Tanzania. Tunaendelea kuweka kipaumbele kwa kuwapa wafanyakazi wetu bora nyadhifa mbalimbali za uongozi barani Afrika ili kuweza kuboresha maendeleo katika nchi mbalimbali ambapo tunafanya shughuli zetu za kibenki.”
Tanzania inaendelea kupewa kipaumbele katika mipango ya benki hiyo katika bara la Afrika na Afrika Mashariki haswa kutokana na ukuaji wake wa kiuchumi na kuweko katika ‘Klabu ya 7%’, ambayo ni listi ya nchi ambazo uchumi wake unakadiriwa kuendelea kukua kwa kasi zaidi katika miaka kumi ijayo.
Kufuatia kuteuliwa kwake Mkurugenzi huyo mpya wa benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani alisema, “Tanzania ina fursa nyingi sana za kibiashara na ninafurahi kurudi nyumbani kuiongoza benki ya Standard Chartered kwenda kwenye hatua nyingine ya kimaendeleo. Nchi yetu inaendelea kuchangia mafanikio ya Umoja wa Afrika Mashariki kwa njia mbalimbali ikiwemo ukuaji mzuri wa uchumi. Pia ugunduzi wa hifadhi za gesi nchini Tanzania unatarajiwa kuleta maendeleo zaidi ya kiuchuni hapa nchini kwetu.”
Sanjay ana shahada ya udhamili ya Kifedha na Rasilimali watu, na shahada ya Uchumi. Pia ni mwanachama wa Chama cha Wahasibu, ACCA. Sanjay pia ni Mjumbe wa Bodi wa benki ya Standard Chartered Uganda. Ameoa na ana watoto wawili.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!