Sunday, 18 October 2015

WIKI YA KAMPENI ZA LALA SALAMA



JUMAPILI ijayo Watanzania wote wenye sifa ya kupiga kura, watatumia haki yao hiyo kuchagua viongozi wa Taifa hili katika nafasi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani nchi nzima. Kutokana na umuhimu huo wa kitaifa, wiki hii ndiyo ya mwisho kwa kampeni za wagombea wa nafasi hizo kutoka vyama mbalimbali kunadi sera zao, na kuandaa mawakala wao watakaoshiriki kuhesabu kura zao.



 Moja ya ajenda kuu iliyoanza wiki iliyopita mpaka siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi, inatarajiwa kuwa amani, amani, amani, kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa lote na kila Mtanzania mmoja mmoja. Tayari baadhi ya viongozi mbalimbali wa Serikali na wa kijamii, wamewasihi Watanzania na wanasiasa, kuhakikisha Taifa linakuwa salama na amani inatunzwa wakati wote wa kampeni, wakati wa kupiga kura, kuhesabu kura, matokeo na baada ya uchaguzi. Kauli ya Lubuva Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva alielezea kushangazwa na hatua ya baadhi ya vyama vya siasa nchini, kukiuka makubaliano waliyoingia na Tume kabla ya kupitishwa kwa wagombea wao. “Niwakumbushe vyama vya siasa vinavunja makubaliano tuliyoafikiana na wagombea wao kabla ya sisi kuwapitisha kuwania nafasi wanazowania za uchaguzi huu, tulikubaliana kwenye fomu namba 10, ambayo walijaza na kusaini na hili la kuwahimiza wapiga kura wao kupiga kura na kuondoka limo,” alisema Jaji Lubuva. Akifafanua, Lubuva alisema Sheria ya Uchaguzi inasema wapigakura mara baada ya kupiga kura wanatakiwa wakae umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura na Sheria ile ya Serikali za Mitaa inasema umbali wa mita 300. Alifafanua kuwa pamoja na kuwepo kwa mkanganyo huo wa sheria hiyo, lakini hali halisi ya uhamasishaji kwa wapiga kura waliojiandikisha mwaka huu wapatao milioni 22.7, kila mmoja akiamua kulinda kura hali haitakuwa ya amani. “Tuliona uhamasishaji wa mwaka huu ni mzuri na watu wengi wamejitokeza kujiandikisha na wana hamasa ya kupiga kura, sasa kama kila mtu atapiga kura na kubaki, je si tunatengeneza mikusanyiko isiyo ya lazima na pia kwa upande mwingine kama ni kusema unalinda kura, utazilindaje kwa umbali huo?” Alihoji Lubuva. Alisisitiza katika makubaliano hayo walisema mara baada ya wananchi kupiga kura warejee katika kazi zao za kila siku, ili kura kuhesabiwa na matokeo yakishabandikwa kwenye vituo, wananchi wanaweza kwenda vituoni kuangalia matokeo. *Upotoshaji wa Mbowe Katika hatua nyingine, Jaji Lubuva aliwaonya wananchi kuepuka kupotoshwa na baadhi ya wanasiasa kuhusu jinsi ya kupiga kura kwenye karatasi ya kupigia kura na kusisitiza kura ni siri na inapaswa kukunjwa kwa maelekezo ya NEC. “Nimemsikia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwafundisha wapiga kura namna ya kupiga kura na kukunja karatasi ya kura, ila anawapotosha, karatasi ya kura inatakiwa kukunjwa kwa maelekezo ya NEC, vinginevyo inaweza kuharibu kura yako,” alisisitiza Lubuva. Akifafanua hilo Jaji Lubuva, alisema karatasi ya kupigia kura inapaswa kukunjwa kwa urefu na kisha kukunjwa tena katikati na sio kama Mbowe anavyoelekeza, kwani kufanya hivyo kutasababisha kuzuia eneo la kupiga mhuri kutokana na kukunjwa vibaya. Kauli ya JK Kauli hiyo ya Lubuva, inaweka msisitizo wa kauli ya Rais Kikwete, ambaye wiki iliyopita aliwakumbusha wananchi kuwa shughuli za uchaguzi, zinasimamiwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi ambazo zinaelekeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndizo pekee zenye mamlaka ya kuendesha na kusimamia uchaguzi. “Nawaomba ndugu zangu tuheshimu kauli na maelekezo ya tume hizo. Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wametoa maelekezo kwa wafuasi wao kutaka wakishapiga kura wakae mita mia kulinda kura zao. Tume ya Uchaguzi imetoa tamko kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria,” alikumbusha. Rais Kikwete alisema kuwa Nec imeeleza kwa usahihi kabisa kwamba wanaosimamia na kulinda kura za wagombea na vyama vyao kwa mujibu wa sheria, ni mawakala wa wagombea na si mtu mwingine yeyote. Alisema mawakala hao wapo ndani ya vyumba vya kupigia kura kwa ajili hiyo, hivyo wafuasi wa vyama vya siasa wasikubali kuchuuzwa na viongozi wao kwa kuwaambia wasiondoke vituoni kwa madai ya kulinda kura na kuhoji watazilindaje, wakati kura zinapigwa na kuhesabiwa ndani ya chumba cha kupigia kura? “Narudia kusisitiza: Unailindaje kura yako ukiwa umbali wa mita mia moja wakati kura zinapigwa na kuhesabiwa ndani ya vituo vya kupigia kura? Mlinzi wa uhakika wa kura ni wakala wa chama chake aliyeko ndani ya chumba cha kupigia kura. “Sisi kwa upande wetu wa vyombo vya ulinzi na usalama tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa agizo la Tume linatekelezwa kwa ukamilifu. Wale wanaotaka kufanya fujo watadhibitiwa ipasavyo bila ajizi wala kuonewa muhali,” alionya.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!