Wakati zikiwa zimebaki siku 23 kuanzia leo kabla ya kupiga kura Oktoba 25, wagombea urais wakiwamo Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaonekana wakichuana vikali katika kampeni huku kambi ya kila mmoja ikielekea kutumia mbinu za ziada kwa nia ya kujihakikishia kura nyingi za kuwaingiza Ikulu.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa hadi sasa, Magufuli na Lowassa wamekuwa wakibadili mbinu kila uchao kuelekea katika dakika za lala salama za kampeni zilizoanza rasmi Agosti 22, huku maeneo makuu yanayoangaliwa zaidi na kila kambi miongoni mwao ikiwa ni pamoja na ufafanuzi wa ahadi wanazotoa, mbinu zao katika kusafiri kutyoka sehemu moja hadi nyingine, maeneo ya kwenda kupiga kampeni na pia aina ya watu wanaowatumia katika kampeni zao.
Wagombea hao wanaonekana kuchuana zaidi katika kampeni kutokana na wingi wa watu wanaowaunga mkono karibu katika kila mikutano yao. Mbali na Magufuli na Lowassa anayewakilisha pia ushirikiano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), wengine wanaoendelea kupambana kwa nia ya kuingia ikulu ili kuwa warithi wa Rais Jakaya Kikwete baada ya uchaguzi ni Anna Mghwira (ACT-Wazalengo), Chifu Lutasola Yemba (ADC), Hashimu Rungwe (Chaumma), Janken Kasambala (NRA), Maximilian Lyimo (TLP) na Fahmy Dovutwa wa UPDP.
AHADI/ILANI
Katika mikutano yao ya mwanzoni mwa kampeni, Lowassa na Magufuli waligusia vipaumbele vyao kadhaa pindi wakiingia madarakani, huku wakihusianisha utekelezaji wake na ilani za vyama vyao.
Kati ya mengi aliyowaahidi Watanzania pindi akiingia Ikulu, Magufuli alisema atahakikisha kuwa elimu inatolewa bure kuanzia madarasa ya chini hadi kidato cha nne.
Alizungumzia pia malengo ya serikali yake katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinazimarishwa, kwa kujenga zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata, hospitali katika kila wilaya na pia hospitali ya rufaa katika kila mkoa. Pia aliutangazia umma juu ya dhamira yake ya kuhakikisha kuwa kila kijiji nchini kinapata mgawo wa Sh. milioni 50 zitakazotumika kusaidia harakati za maendeleo.
Wakati siku zikielekea ukingoni, Magufuli na timu yake wanaelekea kupiga hatua moja mbele kwa kuhakikisha kuwa hatoi tu ahadi hizo, bali pia anaeleza ni kwa namna gani yote anayoahidi yatafanyika. Kwa mfano, ili kushughulikia tatizo la ajira, Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake itahakikisha kuwa viwanda vinajengwa katika mikoa yote na pia tozo zinazokwaza shughuli za kujikwamua kiuchumi kwa vijana na kina mama zinasitishwa mara moja, baadhi zikiwa ni kwa waendesha bodaboda na mamalishe.
Badala yake, Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake itaongeza mapato maradufu kwa kuhakikisha kuwa mianya yote ya ufisadi inazibwa, anaanzisha mahakama maalum ya kushughulikia mafisaidi na kwamba, wafanyabiashara wakubwa wanalipa kodi kwa usahihi.
Lowassa na timu yake walianza kwa kutoa ahadi kuhusu utoaji wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, kutoa fursa kwa kila mwananchi kuwamo katika mpango wa bima za afya, kutoa fursa za ajira kwa vijana na pia kushughulikia kwa taratibu za kisheria kesi zinazohusiana na ugaidi dhidi ya kina Sheikh Faridi.
Kama ilivyo kwa Magufuli, hivi sasa Lowassa na timu yake wamekuwa wakienda mbali zaidi, wakieleza ni wapi fedha zitapatikana katika kutekeleza ahadi ya elimu bure na pia juu ya kutoa fursa za ajira kwa vijana.
Alipokuwa Mtwara, Lowassa alisema zipo fedha nyingi zinazopotea kupitia ununuzi na uendeshaji wa magari ya kifahari kama ya Toyota Land Cruiser maarufu ‘mashangingi’ na kwamba matumizi ya aina hiyo yakidhibitiwa, elimu bure itawezekana.
Pia alizungumzia jinsi serikali yake itakavyofumua mikataba ya gesi na mafuta ili inufaishe zaidi Watanzania. Kadhalika, kuanzisha benki maalum za kuwakopesha madereva wa bodaboda. mama lishe na wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga).
Kwa ufupi, wote wawili hivi sasa wamekuwa wakijikita zaidi katika kufafanua kwa kina ahadi wanazotoa karibu katika kila mkutano.
MATUMIZI YA CHOPA, MAGARI
Mwanzoni mwa kampeni, timu ya kampeni ya Magufuli ilitangaza kuwa itatumia zaidi usafiri wa magari ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. Hata hivyo, hivi sasa CCM wameanza pia kutumia helikopta (chopa) kusafiri katika baadhi ya maeneo.
Timu ya Lowassa ilitangaza kuwa mgombea wao angetumia zaidi chopa na hilo lilianza kushuhudiwa alipokuwa Sumbawanga. Hata hivyo, hivi sasa Lowassa ameanza pia kutumia magari na mwishoni mwa wiki alitumia gari kusafiri kutoka Tanga hadi jijini Dar es Salaam.
KIKOSI CHA KAMPENI
Kadri siku zinavyosonga mbele, timu za Lowassa na Magufuli zimekuwa zikijiimarisha kwa kuongeza watu wa kuzungumza kwenye mikutano yao. Mbali na kikosi chao cha watu 32, Magufuli ameongezewa nguvu katika mikutano yake na hadi sasa, tayari ameonekan akiwa na mawaziri wakuu wastaafu, Joseph Warioba na John Samuel Malecela.
MIKOA MUHIMU
Eneo jingine linaloonekana kuangaliwa kwa umakini katika mbinu za CCM na Ukawa ni maeneo ya kukamilisha kampeni zao. Hadi sasa, ipo mikoa kadhaa ambayo bado haijafikiwa kwa namna inayoonekana kuwa ni ya kimkakati. Hadi sasa, baadhi ya mikoa yenye wapiga kura wengi bado haijafikiwa kabisa na wagombea hao au imefikiwa na mmoja wao tu, baadhi ikiwa ni Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya na Zanzibar.
Vumbi linatarajiwa kutimka zaidi miongoni mwa wagombea hao katika mikoa ya kanda za kaskazini na Ziwa.
UKAWA, CCM WANENA
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya Uchaguzi ya CCM, January Makamba, aliiambia Nipashe jana kuwa chama chake kimejipanga kumaliza kampeni kwa nguvu zaidi katika wiki tatu zilizobaki, lengo likiwa ni kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Makamba alisema wataendelea kutumia usafiri wa gari kuwafikia wapiga kura, lakini hawataacha kutumia chopa pale inapobidi na ndiyo maana wapo makada wao wameshaanza kutumia usafiri huo (chopa) kuzunguka mikoa yote nchini, akiwamo katibu mkuu wao, Abdulrahman Kinana.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhwavi, alisema usafiri wa chopa ni muhimu katika kipindi hiki na wataendelea kuutumia ili kutimiza malengo waliyojiwekea katika kampeni.
“Tutafanya kampeni za nguvu na kasi kwa kuzingatia mahitaji, na tutaongeza chopa ili kumfikia kila mwananchi,” alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Chadema, Tumaini Makene, alithibitisha kuwa chama chao kimejipanga upya katika wiki tatu zilizobaki ili kuhakikisha kuwa Lowassa anaingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu.
Aliitaja mbinu mojawapo kuwa ni kuigawa nchi katika kanda maalum 10 ambazo watakuwa wakizishambulia kimkakati ili kufanikisha ushindi.
Makene alifafanua kuwa licha ya kutumia chopa kama walivyodhamiria kitambo ili kurahisisha usafiri na kupunguza gharama, pia wako tayari kutumia usafiri wowote ule hivi sasa ukiwamo wa magari kama walivyofanya wakati Lowassa akielekea Dar es Salaam kutoka Tanga na hata meli, pikipiki na baiskeli ikibidi watatumia ili kuwafikia wapigakura wengi.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika, alisema wamejiandaa pia kulinda kura zao dhidi ya hujuma zozote zile na njia mojawapo ni kuwataka wananchi kutokwenda mbali zaidi ya mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura ili kuhakikisha kuwa hakuna wizi unaofanyika dhidi ya kura zao.
“Tukimaliza kupiga kura hakuna kuondoka na kurudi nyumbani... tutahakikisha tunakaa mita 200 kutoka vituoni jambo ambalo siyo kosa kisheria kwani tukijidanganya kurudi nyumbani tutapigwa bao la mkono,” alisema Mnyika.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), vituo 72,000 vitatumika nchini kote kwa ajili ya uchaguzi huo na mshindi wa nafasi ya urais atatangazwa rasmi siku tatu baada ya kupigwa kwa kura.
*Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe na Richard Makore
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment