MATOKEO ya ubunge yameanza kutangazwa jana katika sehemu mbalimbali nchini huku kukiwapo na mabadiliko makubwa ya wabunge kati ya vyama vya CCM na Chadema. Katika matokeo yaliyolifikia gazeti hili na ambayo yamethibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi, CCM imewapoteza mawaziri watatu hadi jana.
Hao ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira aliyeshindwa Bunda, Mara, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwezeshaji na Uwekezaji Christopher Chiza aliyeshindwa Buyungu, Kigoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri aliyeshindwa Siha mkoani Kilimanjaro.
Aidha, CCM imepata majimbo kadhaa ambayo iliyapoteza kwa Chadema likiwamo la Ilemela ambalo Highness Kiwia ameshindwa na Angelina Mabula na Musoma Mjini ambalo Vincent Nyerere wa Chadema ameshindwa na mshindani wake mkubwa, Vedastus Mathayo wa CCM.
Pia jana CCM imesema hadi sasa imekwishapata majimbo 176 kati ya majimbo 264 ya uchaguzi ambayo tayari yamejumlishwa, huku majimbo mengine yaliyobakia kura zikiendelea kujumlishwa.
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, January Makamba alisema hayo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu tathmini ya upigaji na kuhesabu kura.
January alisema kwa mujibu wa matokeo yaliyobandikwa hadharani katika vituo vya kupigia kura na wasimamizi wa vituo na nakala kupewa mawakala wa chama hicho, majimbo hayo 176 yameenda kwa chama hicho, huku kikitarajia kupata majimbo mengine zaidi.
Mkoa wa Mara Jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo wa CCM amerejea bungeni baada ya kumshinda mpinzani wake mkubwa, Vincent Nyerere wa Chadema kwa kupata kura 32,836 (55.45%). Nyerere alipata kura 25,589 (43.14%).
Jimbo la Tarime Mjini Mgombea Ubunge wa Chadema wa Tarime Mjini, Esther Matiko ametangazwa mshindi kwa kupata kura 20,017 dhidi ya mgombea wa CCM, Michael Kembaki aliyepata kura 14,025. Kura zilizopigwa ni 35,172 na zilizoharibika ni 580.
Jimbo la Bunda Mjini Ester Bulaya wa Chadema ametangazwa mshindi katika Jimbo la Bunda Mjini kwa kupata kura 28,508 akimbwaga aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira aliyepata kura 16,126.
Serengeti Aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe ameshindwa na Ryoba Chacha wa Chadema. Mkoa wa Manyara Jimbo la Babati Mjini Paulina Gekul wa Chadema ameshinda baada ya kupata kura 21,970 kati ya kura 54,404 zilizopigwa juzi.
Amewashinda wagombea wa ACT, Bibiana Mallya kura 544, Kisyeri Chambi (CCM) kura 16,434, Rehema Minja (NCCR Mageuzi) kura 81 na Manase Boi (UPDP) kura 36. Mkoa wa Morogoro Ulanga Magharibi Dk Haji Mponda wa CCM ameshinda kwa kura 20,870 akimshinda Alphonce Mbassa wa Chadema kura 18,815, Hidaya Ussanga wa ACT Wazalendo kura 1,095.
Kilimanjaro
Moshi Mjini Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffari Michael ametangazwa mshindi wa Jimbo la Moshi Mjini (Chadema) kwa kupata kura 51,616 akimshinda mpinzani wake wa karibu Davis Mosha (CCM) aliyepata kura 26,620. Siha Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri (CCM) ameshindwa kutetea kiti chake katika Jimbo la Siha baada ya kushindwa na Dk Godwin Mollel wa Chadema.
Dk Mollel amepata kura 22,746 (55%) na Mwanri amepata kura 18,584 (44%). Chadema imeshinda kata tisa na CCM kata nane. Hai Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ametetea Jimbo baada ya kupata kura 51,124 dhidi ya mpinzani wa karibu mgombea wa CCM, Danstan Malya aliyepata kura 26,996.
Mkoa wa Pwani
Kisarawe Mbunge wa Kisarawe mkoani Pwani, Suleiman Jaffo ametetea kiti chake kwa kupata kura 28,554 na amemshinda msanii maarufu wa vichekesho, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ wa CUF aliyepata kura 8,863. Chalinze Ridhiwani Kikwete wa CCM ameshinda Chalinze kwa kupata kura 52,695 huku Mathayo Torongei kupitia Chadema akiambulia kura 23,470.
Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa kupitia CCM amepata kura 22,813 na Andrew Kasambala wa CUF amepata kura 13,997. Jimbo la Kibaha Mjini Mgombea wa CCM, Silvestry Koka ameibuka mshindi kwa kupata kura 31,462 na kumwacha mbali mgombea kupitia Chadema, Michael Mtari aliyepata kura 24,860. Mkoa wa Shinyanga Jimbo la Shinyanga Mjini Steven Masele (CCM) ameshinda kwa kupata kura 35,858 katika wapigaji kura zaidi ya 95,000.
Mgombea wa Chadema, Patrobas Katambi alipata kura 31,263 na mgombea wa APPT, Amelina Tambwe alipata kura 178. Mkoa wa Tanga Jimbo la Tanga Mjini Mgombea ubunge wa CUF, Mussa Mbaruku ameibuka mshindi kwa kupata kura 58,675 kati ya kura halali 119, 854 zilizopigwa dhidi ya Omar Nundu (CCM) aliyekuwa akitetea nafasi yake aliyepata kura 57,014.
Mkinga Mgombea wa CCM, Dastan Kitandula ameibuka mshindi kwa kupata kura 21,623 sawa na asilimia 54.192 akifuatiwa na mgombea wa CUF, Bakari Kassim aliyepata kura 13,547, mgombea wa Chadema, Recho Sadiki kura 3,789.
Mkoa wa Singida
Singida Mjini Mussa Sima (CCM) ameibuka mshindi kwa kura 36,690 kati ya jumla ya kura halali 54,937 zilizopigwa. Mgombea wa Chadema, Mgana Msindai alipata kura 16,702.
Msindai alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, kabla ya kuhama Chadema.
Mkoa wa Kigoma
Jimbo la Buyungu Mgombea wa Chadema, Kasuku Bilago ameibuka mshindi kwa kupata kura 23,041 akifuatiwa na Christopher Chiza (CCM) aliyepata kura 22,984, mgombea wa NCCR Mageuzi, Matusela Mawazo amepata kura 1,237 na wa ACT – Wazalendo, Leopold Muhamgaze ana kura 775.
Jimbo la Kigoma Mjini
Mgombea ubunge wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe ameshinda kwa kupata kura 31,546 na kumshinda mpinzani wake wa karibu, Dk Walid Aman Kabourou aliyepata kura 17,344 ambapo mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Daniel Rumenyera akipata kura 12,077. Mkoa wa Lindi Jimbo la Lindi Mjini Walioandikishwa kwa ajili ya kupiga kura ni 48,834 kati ya hao waliopiga ni 39,646.
Hassani Kaunje wa CCM alishindi kwa kura 20,733 dhidi ya mgombea wa CUF, Salum Baruany aliyepata kura 18,843.
Mkoa wa Ruvuma
Jimbo la Mbinga Mjini Sixtus Mapunda wa CCM ameshinda ubunge kwa kura 28,364, akifuatiwa na mpinzani wake, Mario Millinga wa NCCR Mageuzi aliyepata kura 13,102. Jimbo la Mbinga Vijijini Martin Msuha wa CCM ameshinda kwa kura 59,269 dhidi ya Benjamin Akitanda wa Chadema aliyepata kura 11,285.
Mkoa wa Dodoma
Jimbo la Dodoma Mjini Mgombea ubunge, Anthony Mavunde (CCM) ameibuka kidedea kwa kupata kura 84,512 na kumbwaga mgombea wa Chadema, Benson Kigaila aliyepata kura 42, 140. Mtwara Jimbo la Nanyumbu Mgombea wa CCM, Dua Mkurua ameshinda kiti hicho kwa kupata kura 36,175. Wananchi 59,431 walipiga kura ambapo kura halali ni 57, 424 na kura 2007 zikiharibika.
Wagombea wengine na kura zao katika mabano ni Majaribu Lupeto wa CUF (13,067) na Nyuchi Alfred wa Chadema (8,182). Jimbo la Ndanda CCM imepoteza Jimbo la Ndanda kwa mgombea wake, Mariam Kasembe kupata kura 26,215. Kasembe aliyekuwa Mbunge wa Masasi katika Bunge lililopita ameshindwa na Cecil Mwambe wa Chadema kwa kura 26,247 ikiwa ni tofauti ya kura 32.
Tandahimba Mshindi ni Ahmed Katani wa CUF alishinda kwa kura 55,156 dhidi ya Saidi Likumbo wa CCM aliyepata kura 41,088.
Mbeya
Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, ametetea kiti cha ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chadema baada ya kumshinda Mwalyego Shitambala wa CCM. Mbilinyi amepata kura 97,675 akifuatiwa na Shitambala kura 46,894, Amin Ashery wa ACT kura 696, Mary Komba wa Chausta kura 202 na Oswald Mwanyalu wa Makini kura 96.
Jimbo la Mbeya Vijijini Oran Njeza wa CCM ameshinda kwa kupata kura 56,301 akifuatiwa na Zella Abraham wa Chadema, aliyepata kura 52,298, na wa tatu ni Barikc Mwanyaru wa Makini kura 421. Waliopiga kura ni 110,983 kati ya 155,709 waliojiandikisha. Zilizoharibika ni 1,957.
Arusha
Arumeru Mashariki Joshua Nassari ameshinda tena kwa mara ya pili kiti cha ubunge kwa tiketi ya Chadema, akizoa kura 86,694 sawa na asilimia 72.6. Wagombea waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ni Batulo Ibrahim (ACT) kura 622, Mgina Mustafa (AFP) kura 236 na mgombea wa CCM kura 31,847.
Imeandikwa na waandishi Wetu Lindi, Tarime, Musoma, Mtwara, Fadhil Abdallah (Kigoma), Anold Swai (Moshi), Veronica Mheta (Arusha), Kareny Masasi (Shinyanga), Sifa Lubasi, Grace Chilongola (Dodoma), Teddy Challe (Manyara), Joachim Nyambo (Mbeya), Muhidin Amri (Ruvuma), Abby Nkungu (Singida), John Gagarini (Pwani), John Nditi (Morogoro).
No comments:
Post a Comment