Mchuano wa kuwania kwenda Ikulu baina ya wagombea urais wa Tanzania wakiwamo Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umefika katika hatua muhimu ya kufa au kupona.
Kila upande unatumia mbinu zake zote kuhakikisha kuwa unavuna kura nyingi zaidi katika kipindi hiki ambacho ni siku sita tu zimebaki, sawa na saa 144 kabla ya kupiga kura Jumapili ijayo ya Oktoba 25.
Nipashe imebaini kupitia uchunguzi wake kuwa hivi sasa, kambi za Magufuli na Lowassa zimekuwa zikibadili mbinu kukamilisha kazi walizoanza katika wiki ya mwisho ya Agosti. Kambi zote zimekuwa zikipigana vikumbo huku na huko, sura mpya zikiongezwa katika kampeni zao na pia vita nyingine imehamia katika kupigania masafa ya vituo vya redio na televisheni katika kujitangaza.
Kadhalika, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwapo kwa vita kali ya usimikaji wa bendera katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu katikati ya maeneo ya miji mikubwa kama Dar es Salaam.
Aidha, imebainika vilevile kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wenye asili ya Kiasia wamekuwa wakiondoka nchini na kwenda nje ya nchi kusubiri uchaguzi upite, huku Tume ya Taifa ya Uchgauzi (NEC) ikikumbwa na kiwewe juu ya namna ya kuelimisha umma kuhusiana na rai ya kuwataka watu wote kurejea kwenye nyumba zao baada ya kupiga kura na siyo kujiweka kwenye maeneo ya umbali wa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kupigia kura kama wanavyoelekezwa na baadhi ya wanasiasa, hasa wa upinzani.
Hata hivyo, kadri siku zinavyokaribia, Magufuli na Lowassa anayeungwa mkono pia na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF), NLD na NCCR-Mageuzi, ndiyo wanaoonekana kuchuana kwa karibu kutokana na wingi wa watu wanaojitokeza kwenye mikutano yao tangu kuanza kwa kampeni Agosti 21, 2015.
Mbali na Magufuli na Lowassa, wengine walio katika safari ya kuwania kuingia Ikulu ili kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya uchaguzi mkuu Jumapili ijayo ni Maximilian Lyimo wa TLP, Fahmy Dovutwa wa UPDP, Anna Mghwira (ACT-Wazalengo), Chifu Lutasola Yemba (ADC), Hashimu Rungwe (Chaumma) na Janken Kasambala wa NRA.
WAPIGANA VIKUMBO
Licha ya kuwapo kwa ratiba rasmi inayoratibiwa na NEC, bado Lowassa na Magufuli wameonekana mara kadhaa wakipigana vikumbo katika baadhi ya maeneo.
Kwa mfano, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa katika kampeni zao za mikoa ya kaskazini mwa Tanzania, wote walikuwa wakifuatana kwa karibu zaidi. Mmoja akipita siku ya kwanza na kutikisa kwa mkutano mzito, mwingine alionekana kufika eneo hilo au la jirani katika siku inayofuata na kufanya mkutano mkubwa zaidi katika namna inayoonekana ni kama kufuta nyayo za mtangulizi wake. Hili lilionekana zaidi katika ziara za Lowassa na Magufuli kwenye maeneo ya Babati, Monduli, Longido, Hanang, Arusha Mjini, Moshi, Siha, Same na hata Vunjo.
MASAFA YA REDIO, TELEVISHENI
Katika saa hizo 144 zilizobaki, CCM na Ukawa wamekuwa wakichuana kwa karibu katika kupata masafa ya kurusha matangazo yao kupitia vituo vya televisheni na redio. Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa hivi sasa, vituo vya redio na televisheni vimekuwa vikivuna fedha za kutosha kutokana na vita hii ya aina yake baina ya timu ya Magufuli inayojinadi kwa kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ na Lowassa inayojinasibu kwa kauli mbiu ya ‘mabadiliko’.
Kwa mfano, Magufuli ana tangazo lake la televisheni lililoshiba kwa ujumbe na ahadi kuhusu kuboresha huduma za jamii kabla ya kuomba kura, sawa na Lowassa ambaye pia ana tangazo lake la kujipigia debe kali kuwataka Watanzania wampigie kura nyingi za ndiyo ili alete mabadiliko nchini. Na wote wawili wana matangazo kadhaa pia kwenye redio.
WACHUANA KUSIMIKA BENDERA
Vita ni vita, wahenga walinena. Hivi sasa, timu za kampeni za Magufuli na Lowassa zinachuana pia katika kuweka mabango kwenye kuta za majengo ya umma na kusimika bendera za vyama vyao katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na pia kwenye makutano ya barabara kuu.
Kwa mfano, katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, kunako mataa yenye makutano ya barabara za Mandela na Morogoro, mashindano haya ya bendera huonekana wazi. Hali hiyo ipo pia kwenye maeneo ya biashara kama Mtaa wa Kongo, Manzese, Ubungo, Sinza Palestina na Kijiweni, Tandika na Buguruni jijini Dar es Salaam; Makoroboi Mwanza na Soko la Matola jijini Mbeya.
KIWEWE CHAIKUMBA NEC
Wakati vyama, hasa CCM na vile vinavyounda Ukawa vikihaha kutumia kila mbinu kuhakikisha kuwa wagombea wao wanazoa kura nyingi baada ya saa 144 kupita kuanzia leo, NEC iko katika kibarua cha aina yake kuhakikisha kuwa watu hawakai karibu na vituo vya kupigia kura siku ya uchaguzi na badala yake, wote wanarejea nyumbani ili kusubiri matokeo.
Kibarua hiki kwa NEC kimekuwa kizito kutokana na kile kinachohubiriwa na viongozi wa Ukawa kwa wafuasi wao, kwamba kwa vyovyote vile, wahakikishe hawarudi nyumbani na badala yake wanakaa kuanzia mita 200 kutoka vituo vya kura ili kuhakikisha kile wanachodai kuwa ni kulinda kura na mwishowe kuzuia mbinu za chama tawala kufanya hila kupitia kauli maarufu ya ‘ushindi hata kwa bao la mkono’ aliyowahi kukaririwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. Vigogo wa NEC, wakiwamo Mwenyekiti, Jaji mstaafu Damian Lubuva na pia Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhani, wamekuwa wakisisitiza kuwa wananchi waondoke na kurejea kwao baada ya kupiga kura kwani kazi ya kulinda kura zao itafanywa na vyombo vya usalama, wakisisitiza kuwa jambo hilo ni muhimu kuzingatiwa na atakayekaidi atachukuliwa hatua kwa vile kinyume chake, kunaweza kuibua vurugu kwani uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuhusisha wapiga kura wengi zaidi kulinganisha na chaguzi zilizopita.
WATANZANIA WENYE ASILI YA KIASIA
Katika kipindi hiki kifupi kilichobaki, Nipashe imebaini kuwa kuna Watanzania kadhaa wenye asili ya Kiasia wamekuwa wakiondoka wao na hata familia zao na kwenda nje ya nchi ili kupisha uchaguzi ufanyike. Uchunguzi umebaini kuwa kati ya wale wanaoondoka, wengi wamekuwa wakiingiwa hofu kutokana na ushindani mkali unaoonekana hivi sasa baina ya wagombea wa CCM na Ukawa, tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita.
“Ushindani uliopo sasa ni mkali sana... hili kila mmoja analitambua. Ndiyo maana baadhi ya Watanzania hawa (wenye asili ya Kiasia), wamekuwa wakiondoka wao wenyewe na familia zao pia ili kupisha uchaguzi,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina.
AHADI, ILANI
Baada ya kutoa ahadi kemkem kila waendako huku pia wakijielekeza katika ilani za vyama vyao, Lowassa na Magufuli wameongeza nguvu pia katika kufafanua ni kwa namna gani watatimiza yote wanayoahidi.
Akiwa katika mkutano wake mmojawapo wa kampeni mkoani Mtwara, Lowassa anayejivunia ahadi yake ya kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania kuanzia chekechea hadi chuo chuo kikuu, aliwaeleza wapiga kura ni kwa namna gani ahadi yake hiyo inaweza kutekelezeka kirahisi pindi dhamira ikiwapo.
Maeneo mawili makuu ya mfano aliyoyataja kuwa ni chanzo cha mapato ni matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo nchini kama za madini na gesi ambazo aliahidi atazifuatilia kwa kuhakikisha kuwa serikali inapitia upya mikataba yote iliyosainiwa ili kuhakikisha kuwa mwisho wa siku inakuwa na manufaa kwa Watanzania na siyo kwa viongozi wachache waliosaini mikataba hiyo.
Kadhalika, alisema kuwa serikali yake itazingatia nidhamu ya matumizi ya kila kinachopatikana, ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya magari ya kifahari kama Toyota Landcruiser (mashangingi) ili fedha zitakazookolewa zielekezwe katika kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania.
Kadhalika, Magufuli anayeahidi mabadiliko ya kweli kwa nia ya kuneemesha Watanzania ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bure hadi kidato cha nne, kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata, kuongeza mtandao wa barabara za lami nchini na kugawa milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa; anasema namna mojawapo ya kupata fedha za kutekeleza ahadi zake hizo ni kuongeza mapato yatokanayo na kodi walau mara mbili ya kiwango cha sasa na pia kubana mianya yote ya ufisadi na rushwa serikalini, hasa kutokana na kile anachosema kuwa kwa muda mrefu, ‘mafisadi wamelelewa sana’ na kuwaumiza Watanzania kwa kiasi kikubwa.
SURA MPYA ZA KAMPENI
Kadri siku ya uchaguzi inavyokaribia, timu za kampeni za Magufuli na Lowassa zimezidi kuimarishwa kwa kuongeza sura mpya kwenye mikutano yao. Kwa mfano, mbali ya kuwa na kikosi chao cha watu 32, Magufuli ameongeza nguvu katika timu yake ya kampeni kwa kuwahi kuwatumia mawaziri wakuu wastaafu, Joseph Warioba na John Malecela. Kadhalika, katika maeneo tofauti, marais wastraafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wamekuwa wakitumiwa kuongeza nguvu.
Timu ya Lowassa imeendelea pia kutumia mbinu hii ya kuongeza sura mpya. Hivi sasa, timu hii imeongezewa nguvu kubwa na aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru na pia hivi karibuni wamempata aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu. Hata hivyo, Mwapachu bado hajapanda jukwaani, ingawa ameshawaambia waandishi wa habari kuwa mgombea pekee mwenye sifa ya kuwa rais ajaye ni Lowassa.
CCM, UKAWA
Alipoulizwa kuhusu mikakati yao katika saa 144 zilizobaki kuanzia leo, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hivi sasa mashambulizi yao yataongezwa nguvu na timu mbalimbali ziatazokwenda kwenye kanda kumi za Magharibi, Kati, Pemba, Unguja, Pwani, Kaskazini, Victoria, Serengeti, Nyasa na Kusini.
“Tunakwenda kusambaza majeshi kila kona ya nchi. Tutashambulia kila kanda, kwetu kila kanda ni kitovu cha mapambano... kila kanda kuna vifaa vyote muhimu kama rasilimali watu na magari, tutafika maeneo yote kwa wakati mmoja,” alisema.
Makene alisema kwa saa hizi ni sawa na kula ng’ombe na wanakwenda kumalizia mkia au kupondaponda kichwa cha adui.
“Kawaida watawala wanapokwenda kushindwa wanakunjua makucha yao, na tunaona nchini kwa sasa wameanza kueneza hofu kwa Watanzania, watu wanapigwa na kunyanyaswa, sisi tunaondoa hofu na kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi, wakati wao wanafanya hayo sisi tunawatia moyo wananchi kuwa uchaguzi ni wao. Watumie haki yao ya msingi kuchagua viongozi bora wa kuleta mabadiliko, ujumbe utapelekwa na timu hizo,” alibainisha.
Alisema Lowassa amemalizia kampeni zake katika mikoa yote, baada ya mkutano wa jana jijini Mbeya na sasa anakwenda kupiga kampeni kwenye maeneo wanayoamini kuwa yana nafasi kubwa ya kuamua mshindi na pia hali ya kisiasa kwa kila eneo nchini, kwa maana ya kuongeza nguvu kila sehemu.
Kwa mujibu wa NEC, mikoa yenye wapiga kura wengi ambayo ni ngome muhimu kwa ushindi wa chama chochote ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Kagera, Tabora, Tanga, Dodoma na Arusha.
“Timu zote zitasambaa nchi nzima , tunatambua umuhimu wa kila eneo na ndiyo maana tumesambaza watu,” alisema.
Alipoulizwa jana kuhusiana na kampeni zao katika wiki hii iliyobaki kabla ya uchaguzi, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CCM, Godfrey Chongolo, alisema atafutwe Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba au Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Makamba alipotafutwa, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms), pia hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment